Wednesday, December 1, 2021

CRB Yataka Makandarasi Wasiwe Waoga Kudai Haki Zao

Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Injinia Consolatha Ngimbwa akizungumza mara baada ya kufungua mafunzo ya siku tatu ya usimamizi wa mikataaba kwa makandarasi wazalendo. Kushoto ni Mratibu wa Mafunzo wa bodi hiyo, Neema Fuime. Kulia ni mkufunzi Emmanuel Kachuchuru na Msajili Msaizidi wa CRB, Injinia David Jere

Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Injinia Consolatha Ngimbwa akizungumza kwenye mkutano wa mafunzo kwa makandarasi wazalendo unaoendelea jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Msajili Msaidizi wa bodi hiyo Injinia David Jere, Mratibu wa Mafunzo wa bodi hiyo, Neema Fuime na Mkufunzi wa mafunzo hayo Emmanuel Kachuchuru.
Msajili Msaidizi wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Injinia David Jere akizungumza kwenye mafunzo ya siku tatu kwa makandarasi wazalendo unaoendelea jijini Dar es Salaam. Anayefuata ni Mwenyekiti wa bodi hiyo, Injinia Consolatha Ngimbwa na Mratibu wa Mafunzo kwenye bodi hiyo, Neema Fuime na Mkufunzi wa mafunzo hayo, Injinia Emmanuel Kachuchuru.

BODI ya Usajili wa Makandarasi (CRB), imewataka makandarasi kuacha woga kwenye kudai haki zao pale mikataba yao inapokiukwa kwa kuhofia kuharibu uhusiano na wateja wao.

Wito huo umetolewa  jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mhandisi Consolatha Ngimbwa, wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kuhusu usimamizi wa mikataba kwa makandarasi wazalendo.

Amewaasa watumie ujizi watakaoupata badala ya kuishia kwenye vitabu tu kwani uzoefu unaonyesha kwamba wapo makandarasi ambao pamoja na kuwa na ujuzi, bado wanashindwa kusimamia haki zao eti kwa kuogopa kuharibu uhusiano na waajiri.

“Msifanye hivyo kwa sababu katika mikataba mkandarasi ana wajibu na haki zake na mwajiri vivyo hivyo. Hebu jiulize kwa nini mkandarasi akikiuka makubaliano mwajiri hasiti kumchukulia hatua? Mbona Mwajiri haogopi kuharibu uhusiano,” amesema.

Kadhalika, amewataka  makandarasi wazalendo kutokurupuka wakati wa kusoma mikataba ya ujenzi ili kuepuka hasara wanayoweza kupata na wakati mwingine kukimbia kazi wanazopewa.

Amesema usimamizi mzuri wa mikataba ni ujuzi wa muhimu na wa lazima kwa makandarasi kwa sababu kimsingi kazi ya ukandarasi ni mikataba na kwamba nyakati zote, mkandarasi anashughulika na mikataba.

“Kazi yenu ni mikataba, mkandarasi atashiriki zabuni ili akifanikiwa apewe mkataba wa utekelezaji, atatekeleza ili kutimiza makubaliano yaliyomo katika mkataba husika na mwishowe akikamilisha ataufunga mkataba husika, na kadhalika. Hakuna biashara ya ukandarasi bila mkataba na hivyo hakuna mafanikio katika biashara hii bila ujuzi wa kusimamia mikataba,” alisema.  

Amesema kwenye mafunzo hayo watajifunza vitu muhimu katika mikataba ya ujenzi, haki na wajibu wa pande zote za mkataba, nyaraka za mikataba, hatua katika usimamizi wa mikataba, utatuzi wa migogoro, madai katika mikataba na mengineyo mengi.

Amesema lengo kubwa ni kuwajengea misingi itakayowasaidia kusimamia mikataba yenu mbalimbali vizuri zaidi.

“Nina uhakika kwamba haya yote mnayafanya katika shughuli zenu za kila siku za ukandarasi hususan mnapotekeleza miradi yenu mbalimbali. Kazi ya mafunzo haya itakuwa ni kuboresha namna ya kufanya usimamizi huo kwa kuzingatia misingi ya kitaalam. Kupitia mafunzo haya, nina uhakika mtaongeza ujuzi wenu kwa kiwango kikubwa katika eneo la usimamizi wa mikataba,” alisema.

Amewataka makandarasi kujua umuhimu wa mafunzo ya manunuzi kwa njia ya kielektroniki TANEPS kwa sababu mfumo huu ndiyo njia pekee ya kuwasilisha zabuni za miradi ya Serikali na kwamba serikali na taasisi zake mbalimbali ndiyo mwajiri mkubwa wa makandarasi.

Amesema CRB inazo taarifa kwamba katika TANEPS  wapo makandarasi ambao huwatafuta watu kutoka nje ya kampuni zao ili kuwasilisha zabuni zao katika mfumo na  bahati mbaya sana ni kwamba hao watu wa nje ya kampuni wanatumiwa pia na makampuni ambayo ni washindani wao.

“Matokeo yake ni kwamba ule usiri wa zabuni yako hasa bei unakuwa haupo tena na hivyo kuwepo uwezekano mkubwa wa kukosa zabuni husika,” amesema.

Msajili Msaidizi wa CRB, David Jere amewataka makandarasi hao kuhakikisha wanalipa ada za mwaka ili kuepuka kufutiwa usajili na kwamba kulipa ada ni wajibu wa kisheria hivyo mkandarasi asisubiri kusukumwa sukumwa kulipa.

No comments :

Post a Comment