Viongozi mbalimbali wakifurahia maadhimisho ya miaka mitano ya Taasisi ya SPRF yenye makao yake makuu mkoani Singida.
KatibuTawala wa Wilaya ya Singida, Wilson Shimo, akipata ‘champaign’ kwenye maadhimisho hayo.
Mgeni rasmi wa maadhimisho hayo Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu akihutubia.
Mkurugenzi Mtendaji wa SPRF, Dkt Suleiman Muttani akizungumza.
Viongozi
mbalimbali wakishiriki kukata keki kuashiria maadhimisho ya kimafanikio
ya miaka 5 ya SPRF na Jamii. Kulia ni Padri Gilbert Mwilu, Mbunge wa
Singida Mashariki Miraji Mtaturu na Mkurugenzi wa taasisi hiyo Dkt
.Suleiman Muttani.
Afisa ufuatiliaji wa SPRF, Mwedinuhu Beleko akizungumza kwenye hafla hiyo.
Baadhi ya washiriki wakifuatilia tukio hilo.
Watoto
yatima na waishio kwenye mazingira magumu wakifurahia muda mfupi baada
ya kupata chakula cha mchana na watendaji wa taasisi hiyo.
Mkurugenzi
Mtendaji wa SPRF, Dkt Suleiman Muttani akikabidhi zawadi ya taulo za
kijani kwa watoto njiti ndani ya Hospitali ya Rufaa ya Mandewa.
Mwonekano
wa taulo za kijani kwa matumizi ya watoto wachanga zilizotolewa na SPRF
kama zawadi kwenye maadhimisho ya miaka 5 ya taasisi hiyo.
Na Mwandishi Wetu, Singida
………………………………………………………………………….
TAASISI
isiyo ya kiserikali ya Jiokoe na Umasikini yaani ‘Stars of Poverty
Rescue Foundation’ (SPRF) hatimaye imetimiza miaka mitano ya utume na
utumishi wake kwa jamii tangu kuanzishwa kwake huku Mgeni rasmi wa
maadhimisho hayo Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu
akiyataka mashirika mengine kuiga mfano wa juhudi za SPRF kama chachu ya mabadiliko dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa mwanamke na mtoto
SPRF
ilianzishwa Desemba 2014 kwa malengo kadhaa, ikiwemo kuweka mazingira
wezeshi katika kuchukua hatua za kuondoa umaskini wa kipato, kusaidia
uimarishaji wa mifumo yenye kusaidia makundi ya watu walio katika
mazingira magumu na hatarishi, na kuanzisha programu za elimu na afya
ili kusaidia makundi athirika.
Malengo
mengine ya taasisi hiyo, ambayo kwa sasa inafanya kazi zake chini ya
ufadhili wa Foundation for Civil Society (FCS), ni kukuza ushirikiano
miongoni mwa wadau na jamii, taasisi za kitaifa na kimataifa kwa lengo
la kutokomeza umaskini wa kipato nchini na kwingineko, sambamba na
kuimarisha uwezo wa kitaasisi katika kukua na kutekeleza program
endelevu.
Akitoa
simulizi ya kusisimua ya sababu iliyowapa msukumo wa kuanzisha SPRF,
wakati wa hafla ya kusherehekea tukio hilo, mkoani hapa jana, Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi hiyo, Dk Suleiman C. Muttani, alianza kwa kusema
umasikini una gharama kubwa!
“Ilikuwa
kipindi cha majira ya kiangazi mwezi Julai mwaka 2014, wakati alipoitwa
kumuona binti wa miaka 19 akiwa na tatizo linalojulikana kama uzazi
pingamizi, na nilipomchunguza niligundua ana uambukizo mkali sehemu ya
kondo la mtoto na kwenye via vya uzazi,”
Alisema
binti huyo alikuwa hajaolewa akiishi na mama yake mzazi aliyekuwa
mkulima mwenye kipato kidogo sana huko maeneo ya Merya..huku akiwa
anajiuliza huenda binti huyo ametelekezwa na familia, lakini ukweli ni
kwamba mama yake hakuwa na nauli ya kumpeleka hospitalini.
Muttani
alieleza kwamba ukosefu wa fedha ukichagizwa na uelewa mdogo wa
vidokezo vya hatari katika ujauzito, vilipelekea wazazi wamuite Mkunga
wa jadi ili binti azalie tu nyumbani lakini mwisho wa siku pale nyumbani
ilishindikana kujifungua.
“Hatimaye
familia iliamua kumpeleka hospitali akiwa hoi, hajitambui. Alipofika
hospitali tuligundua uzazi pingamizi na kumfanyia upasuaji ili kutoa
mtoto na kuokoa maisha yake,” alisema Muttani.
Pamoja
na juhudi zote zilizofanywa lakini siku ya tatu binti alipata fistula,
akivuja mkojo hovyo bila kujitambua na alifariki dunia siku ya 9 akiwa
hospitalini “Katika kujadili kifo hicho mimi na wataalam wenzangu wa
afya tuligundua kwamba kifo hicho kingeweza kuzuilika ila alicheleweshwa
kuja kwenye matibabu, uzazi pingamizi na uambukizi mkali ndizo sababu
kuu za kifo chake,” alieleza
Alisema
wao kama wataalamu hawakuwa na jibu la moja kwa moja la jinsi ya
kukabili umaskini wa kipato cha familia yake, kama sababu kuu ya
iliyopelekea binti huyo kupoteza maisha. Kifo hicho kinamaanisha kwamba
“umaskini una gharama kubwa!…ya kwamba sadaka ya maskini ni kifo.
“Hivyo
taasisi ya SPRF ilianzishwa kwa msukumo wa kifo hiki cha msichana kwa
lengo la kusaidiana na serikali kutekeleza MKUKUTA kama suluhisho la
gharama za umaskini, azma hasa ikiwa ni kujenga mazingira wezeshi katika
kukabili umaskini wa kipato; na huo ndio ulikuwa mwanzo wa safari
yetu,”
Kwa
upande wake, Mtaturu akisisitiza juu ya madhara ya mila zilizopitwa na
wakati, ukeketaji, na ukatili wa kijinsia hususan unaofanywa bila huruma
kwa mwanamke na mtoto,…alisema vitendo hivyo bado vipo na ili
kutokomeza inahitajika uwepo wa viongozi imara na jasiri hasa katika
ngazi za vijiji.
“Naipongeza
taasisi hii ya mfano ambayo siku zote imekuwa ikijielekeza kwenye
baadhi ya malengo endelevu ya kitaifa na dunia kwa vitendo….mnatekeleza
kikamilifu lengo namba moja la dunia ambalo linasema kusiwe na umaskini,
lengo la tatu linahusu afya na ustawi na lengo la tano ni usawa wa
kijinsia,” alisema Mtaturu.
Mbunge
huyo ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo alisema sio
jambo jepesi kuhamasisha masuala ya usawa wa kijinsia, haki za wanawake
na watoto, na jamii kuachana kabisa na mila potofu, ukeketaji, ndoa na
mimba za utotoni ndani ya jamii ya watu wenye mitazamo na mapokeo
tofauti tena ukiwataka kuacha mila zao wenyewe, na zaidi kuwafanya watu
wenyewe wapinge mila zao.
Alisisitiza
kwamba sio kazi ndogo kuwakusanya watu mahala pamoja na kuzungumza
lugha yao, na hatimaye wao wenyewe kukubali, kubadilika na kugeuka kuwa
kipaza sauti dhidi ya mila potofu na kandamizi…sio jambo jepesi hata
kidogo!
“Kuna
ustadi mkubwa katika mpangilio wa kazi zao na mawasiliano katika ngazi
zote wanapotekeleza mradi, hufanya kazi zao bila kumwacha yoyote nyuma,
nalisema hili kwa dhati kwa kuwa naifahamu vizuri taasisi hii tangu
mwaka 2017 wakati nikiwa Mkuu wa Wilaya pale Ikungi,” alisema
Huku
akionesha kufurahishwa na utendaji wa taasisi, Mtaturu alisema “Binafsi
nimependezwa sana na mbinu zao za ushirikishaji viongozi wa serikali,
wazee wa mila, viongozi wa dini na wazee mashuhuri katika kufikia
malengo yao na zaidi kwenye uanzishwaji wa vikundi vya hamasa vya sauti
ya mwanamke na sauti ya mwanafunzi kama mawakala wa mabadiliko kwenye
kupinga ukatili wa kijinsia.”
Alisema
pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na Rais John Magufuli katika
kuimarisha na kuitegemeza sekta ya afya katika kila nyanja nchini, bado
vifo vitokanavyo na uzazi imekuwa ni tatizo huku akitoa rai kwa jamii
kuungana na kuwa watekelezaji wakuu wa kupinga vitendo vyote vya ukatili
na viashiria vinavyoweza kuzuia vifo hivyo nje ya sababu za kimatibabu
Mtaturu
ambaye muda mwingi alitumia kupongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya
Tano katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kitaifa, hususani suala
linaloendelea la kasi ya usambazaji wa nishati ya umeme vijijini,
alisema anaamini muda mfupi ujao jamii itabadilika kabisa na wimbo huo
wa umaskini itakuwa historia.
Alisema
mtu mwenye tashwishi ya utaifa na mwenye kujitoa ipasavyo katika
kufanya kazi za kijamii ni lazima awe mtu mwenye kuguswa na changamoto;
na falsafa zake zijengwe kwenye kuamini katika maslahi mapana ya utu,
tunu na heshima.
Aidha,
anapaswa kuwa mtu aliojiwekea nadhiri ya kuwa mtumishi wa jamii ajuaye
tofauti ya umuhimu wa kutoa na kupokea, kuwa mwaminifu, anayeishi
misingi ya ubinadamu na siku zote aliye tayari kujitoa, mbunifu na
mwenye kujichunguza kama majivuno uliyonayo hayana nguvu kuliko hekima
na unyenyekevu wako
Mtaturu
aliwataka SPRF kutochoka wala kukata tamaa kutumikia jamii hata kama
dhoruba ni kali, tofauti za kitamaduni zisiwatikise, huku akiwasihi siku
zote kuendelea kuwa wavumilivu, wastahimilivu, wasiokimbia migogoro
wala kujitengenezea migogoro na kukwepa kuendeshwa kwa matamanio ya
utajiri na umaarufu usio na tija.
Alisema
maadhimisho hayo yatukumbushe tulipotoka, tulipo na tuendapo. Tunaweza
kuwa na historia na mitazamo tofauti lakini jambo la hakika kwa wote ni
umoja wetu.
“Ni
muhimu mno kujiuliza kwanini wewe uko hai na unafanya unayoyafanya
sasa, mwisho wa siku hatutazamwi kwa yale tunayojifanyia sisi wenyewe
bali pia kwa yale ambayo tulipaswa kuyafanya kwa wengine na
hatukuyafanya,” alisema Mtaturu.
Awali
Afisa Ufuatiaji wa SPRF, Mwedinuhu Beleko, alisema pamoja na mambo
mengine taasisi hiyo kwa sasa inatekeleza mradi wa “AWARE,’’ kwa
ufadhili wa FCS ambao azma yake ni utetezi wa haki kwa mwanamke na mtoto
wa kike, kupinga mila potofu, masuala ya ukeketaji, ndoa na mimba za
utotoni, na ukatili kwa mtoto-huku idadi ya walengwa takribani 6000
kutoka kata 5 za Ikungi na vijiji 12 wamefikiwa.
Beleko
alisema, ukeketaji hufanyika kwa siri sana kwa baadhi ya maeneo hasa
nyakati za usiku, huku mtindo unaotumiwa kwa sasa ukiwageukia zaidi
watoto wachanga hali inayohatarisha mustakabali mzima wa ukuaji wa mtoto
kiafya, kimwili na kiakili.
Kuhusu
mimba za utotoni Beleko alisema asilimia 7 ya wasichana nchini
wanaolewa wakiwa na miaka 15, na asilimia 37 huolewa wakiwa na miaka 18.
Wasichana wa umri huo bado hawajakomaa kukabili majukumu ya ndoa,
uchungu na kujifungua.
Hata
hivyo mradi huo wa ‘AWARE’ kwa mkoa wa Singida mpaka sasa umewafikia
walengwa wa moja kwa moja 1875 kati yao 1336 walikuwa wanawake na 539 ni
wanaume, wanajamii wengine wapatao 105,000 walifikiwa kwa njia ya
vyombo vya habari.
“Sauti
ya Mwanamke na Sauti ya Mwanafunzi ni vikundi tulivyovianzisha ndani ya
maeneo ya utekelezaji wa mradi kama sehemu ya juhudi ya SPRF
kushirikiana na jamii, lengo likiwa ni kuhamasisha na kuleta mabadiliko
endelevu ndani ya jamii ile ile inayowazunguka kwa kuzingatia makundi
rika, mathalani wanafunzi kwa wanafunzi wenzao kutoa ujumbe kupitia
ngoma, mashairi, ngonjera, maigizo na midahalo,” alisema Beleko.
Maadhimisho
ya miaka mitano ya SPRF yalikwenda sanjari na shughuli mbalimbali
ikiwemo utoaji wa zawadi za taulo za kijani za kuwafunika watoto
waliozaliwa kabla ya muda “njiti” ndani ya Hospitali ya Rufaa Mandewa,
kupata chakula cha mchana na watoto yatima na waishio katika mazingira
hatarishi na kuwapatia vyeti na zawadi baadhi ya marafiki na wanufaika
wa mradi.








No comments :
Post a Comment