Sehemu ya huduma mbalimbali kwa
Wasafiri iliyopo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataiafa Julius Nyerere
Terminal 3, Jijini Dar es Salaam ambao ujenzi wake umekamilika hivi
karibuni.
Sehemu ya Ukaguzi mizigo kwa
abiria yenye miundombinu ya kisasa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataiafa
Julius Nyerere Terminal 3, Jijini Dar es Salaam ambao ujenzi wake
umekamilika hivi karibuni.
Moja ya majengo yanayotumika kwa
Abiria wanaondoka na wanaofika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
Julius Nyerere, Terminal 3, Jijini Dar es Salaam, ambao ujenzi wake
umekamilika hivi karibuni.
Sehemu inayotumika kwa abiria
kuingia na kutoka kwenye ndege yenye miundombinu ya kisasa katika Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam, kama
inavyoonekana kwenye picha.
…………………………
Na Lilian Shirima Maelezo
Tanzania mpya imedhihirishwa na
Ujenzi wa Jengo la Tatu la Abiria (Terminal 3) katika
uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)
Akizungumza na Idara ya Habari
Maelezo hivi karibuni Msimamizi wa mradi wa ujenzi wa uwanja huo kutoka
Wakala wa Taifa wa Barabara TANROADS, Mhandisi Barton Komba amesema:
“Jengo la tatu la Abiria
limesanifiwa kwa viwango vya Kimataifa vya daraja C vya Usafiri wa Anga –
IATA. Hivyo linatarajiwa kwa sasa kuwa kituo kikuu cha usafiri wa anga
na kuleta tija kwa Tanzania”.
Mhandisi Komba ameongeza kwa
kusema, asilimia 70 ya gharama ya mradi zimetumika kwenye usimikaji wa
miundombinu ya mifumo maalum ndani ya jengo (airport special systems).
“Nasema ukizungumzia uwanja wa
ndege, unazungumzia usalama wa abiria na mizigo, gharama iliyotumika
katika usalama wa eneo la ndani ya jengo (Mechanical Eletrical Plumbing
– MEP) pamoja na kufanyia kazi eneo la uhamiaji ambapo ni zaidi ya
asilimia 70 ya mradi, mitambo ndio imechukua sehemu kubwa ya gharama.”
Aidha, Mhandisi Komba amesema kuwa, katika eneo hilo sehemu ya uhamiaji kumefungwa madawati 10 yenye sehemu za kufanyia kazi 40 zenye uwezo wa kuhudumia abiria arobaini wanaowasili au kuondoka kwa wakati mmoja.
Mhandisi Komba amesisitiza kwa kusema kuwa kwa abiria ambao wanaotumia hati za kusafiria za kieletroniki (E Passport) hawatalazimika kupita kwenye huduma za uhamiaji bali kwenye lango la kieletroniki ( E-Gate) ambapo watahakiki hati zao za kusafiria na alama za vidole.
Pia, kwa upande wa ukaguzi wa mizigo (Baggage Handling System HBS)
umesimikwa mfumo wa kisasa wenye uwezo wa kukagua mizigo katika
madaraja matano tofauti pamoja na mashine za kukagua mizigo midogo ya
mkononi . Ameainisha Mhandisi Komba
Komba amesema kuwa daraja la kwanza mzigo utaangaliwa kwa mashine (scanner)
ili kubaini taswira ya kitu kilichomo ndani ambapo daraja la pili mzigo
huo utachunguzwa tena kwa kutumia mashine (scanner) zenye nguvu zaidi
ya kuona kwa kina.
Daraja la tatu mzigo utachunguzwa
kwa kutumia mashine zenye uwezo wa kuchanganua picha ya mzigo
iliyoonekana kwenye daraja la pili kwa vipande mia moja tofauti (3 Dimention).
Hatua itakayofuata ni mzigo utaingia daraja la nne sehemu ya wataalamu
wenye uwezo wa kutasiri picha iliyoonekana katika madaraja yote
yaliyotangulia.
Mhandisi Komba amesema, endapo
mzigo hautakuwa na dosari ukifika daraja la nne utapata kibali na hivyo
kuingizwa kwenye ndege. Aidha, mzigo wenye dosari utaingia daraja la
tano ambapo hatua za kisheria zitachukuliwa na vyombo vya usalama.
Akifafanua Mhandisi Komba ameeleza
kuwa eneo la kupokea mizigo lenyewe linayo mikanda minne yenye urefu wa
mita 95, ukiwemo mmoja kwa ajili ya mizigo hatarishi inayotoka sehemu
zisizokuwa na uhakika wa usalama kuingia kwenye nchi yetu.
Akielezea miundombinu mingine
Mhandisi Komba amesema “Miundombinu iliyosimikwa kwa viwango vya
kimataifa ndani ya jengo hili ni mifumo ya tahadhari ya zima moto,
utandazaji wa nyaya , ufungaji wa lifti na escalator pamoja na kazi nyingine za ndani ambazo kwa ujumla wake zimekamilika kwa asilimia 96.8”.
Kwa mujibu wa Mhandisi Komba, eneo
la maegesho ya ndege na viungio vyake lenye ukubwa mita za mraba
227,000, limekamlika kwa asilimia 99.9 na kwamba ndege 19 za daraja C
ambazo ni ndogo na ndege 11 za daraja E ambazo ni kubwa kama vile
Boieng 787, Dreamliner zinaweza kuegeshwa kwenye eneo hilo. Tofauti ya
ndege za daraja C na daraja E pia inatokana na urefu wa ndege, upana wa
mabawa yake na vilevile ukubwa na idadi ya abiria.
Amesema, Mhandisi Komba kuwa, kazi
nyingine iliyokamilika na kuupa uwanja huu muonekano wa kimataifa ni
usimikaji wa vivuko vya abiria 12 (Passanger Boarding Bridges)
pamoja na ujenzi wa barabara za viungio kuingia na kutoka kwenye
maegesho ya ndege. Kukamilika kwa mradi huu kunatarajiwa kuwa chaguo la
ndege nyingi zinazoruka kwenda nchi za Afrika na bara Asia na Ulaya.
Eneo la nje ya jengo ambalo ni
maegesho ya magari ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 98.6 na ipo
nafasi ya kuegesha magari 2,000 kwa ajili ya abiria wanaokuja na
kuondoka nchini. Katika eneo hili imesimikwa mifumo ya kupoozea hewa na
mifumo ya maji ya mvua na maji taka.
Aidha, taa nyingi zimefungwa kwenye maegesho ya magari, jenerata 7 kwa ajili ya dharura kila moja ikiwa na uwezo wa 2MVA ili kuhakikisha huduma zinapatikana wakati wote hata inapotokea hitilafu ya umeme.
Akielezea historia ya uwanja wa
ndege wa Kimatafa wa Julius Nyerere Mhandisi Komba amesema kuwa, ujenzi
wa jengo la tatu la abiria ni mwendelezo wa majengo mawili ya abiria ya
zamani yaani Terminal 1 na Terminal 2. Kilianza kufanya kazi mwaka 1959
kikiwa na jengo moja la abiria lenyw uwezo wa kuhudumia abiria laki 5
kwa mwaka na barabara moja ya kuruka na kutua ndege.
Jengo la Pili la Abiria (Terminal
2) lilijengwa mwaka 1984, likiwa na uwezo wa kuhudumia abiria Milioni
1.5 kwa mwaka, idadi iliyofikiwa katikati ya miaka ya 2000. Hadi hii leo
idadi ya abiria wanaohudumiwa katika uwanja wa JNIA imeongezeka na
kufikia abiria Milioni 2.5 kwa mwaka.
Kutokana na kuzidiwa kwa uwezo wa
Jengo la Pili la abiria na kuzorota kwa huduma za abiria na mizigo
kwasababu ya uchakavu wa jengo, mwaka 2000 wakati serikali ikiwa katika
zoezi la uboreshaji wa miundombinu mbalimbali ya viwanja vya ndege
ilionekana dhahiri hitaji la ujenzi wa jengo jipya la abiria.
Aidha, wastani wa ongezeko la
ongezeko la abiria wanaotumia kiwanja hiki ni asilimia 12.5 kwa mwaka.
Ongezeko hili ndilo chimbuko la mradi wa ujenzi wa Jengo la Tatu la
Abiria ambalo litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria Milioni 6 kwa mwaka.
Kukamilika kwa mradi huu
kutawezesha uwanja huu kuwa kitovu cha usafiri wa anga kutokana na
ukweli kwamba majengo yote mawili terminal one na two yalikuwa yamezidiwa na wingi wa abiria wanaofikia Milioni 2.5 kwa mwaka. Amefafanua Mhandisi Komba.
Amemalizia, kwa kusema kuwa ujenzi
wa Jengo la Tatu la Abiria (Terminal 3) katika Kiwanja cha Ndege cha
Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) unajengwa na Kampuni ya BAM
International ya Uholanzi kwa gharama ya Euro milioni 276.7, sawa na
zaidi ya shilingi Bilioni 560 za kitanzania.
Uwanja wa JNIA umefikia asilimia
97.6 ya ujenzi na unatarajiwa kukabidhiwa rasmi kwa serikali mwishoni
mwa mwezi Mei, 2019 ambapo uwanja una uwezo wa kuhudumia abiria
milioni 6 kwa mwaka.
No comments :
Post a Comment