* Asema wasitumie nafasi zao kunyanyasa wengine, akemea ubaguzi
*Ataka wajitoe kusaidia wasionacho kama njia ya kumuenzi Dk. Mengi
MKUU wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Mkuu Dk. Ferdinand Shoo amewaonya
viongozi wa Tanzania na kuwataka watumie nafasi zao kuwasaidia wengine
hasa wale wenye uhitaji.
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi,
Mei 9, 2019) wakati akitoa mahubiri kwenye ibada ya mazishi ya aliyekuwa
Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni za IPP, Dkt. Reginald Mengi iliyofanyika
kwenye kanisa la KKKT, Usharika wa Moshi mjini.
Amesema kuna watu wakipata vyeo
ama utajiri kidogo tu, wanatumia nafasi zao kunyanyasa wengine na
akaonya Watanzania wasie wepesi wa kuhukumu, kunyanyasa wengine au
kubagua wengine.
Katika mahubiri yake, Dk. Shoo
amesema kama kuna dhambi ambayo binadamu anapaswa kuifanyia toba ni ile
ya kubaguana na kama Watanzania wanahitaji Taifa lipokee baraka kutoka
kwa Mungu, ni vema wakaacha kufanya hivyo. Amesema dhambi nyingine
inayopaswa kufanyiwa toba ni ile ya watu wenye nafasi kuwakanyaga
wengine.
“Ndugu zangu tukiwa na cheo,
tukiwa matajiri, tukiwa na uwezo tuvitumie kuwasaidia wengine, tuache
ubinafsi, tuache kiburi, tuache kujitutumua hasa kwa viongozi wa umri
mdogomdogo. Kuna mahali mmefika mnajitutumua kama chatu, acheni kabisa.
Naomba tuwe unyenyekevu ndugu zangu.”
“Wale wanaopata utajiri, acheni
kukumbatia mali zenu, toeni na kuwasaidia wenye uhitaji kwani mnapata
satisfaction kwa kufanya hivyo. Huu ni ujumbe kwetu sote na Mungu
atusaidie tulishike hili. Muendelee kuiombea familia na yale mazuri
mengi tuliyojifunza kwake tukayatende tukayatende, tuyaenzi,” amesema.
Akimuelezea Dkt. Mengi, Askofu
Mkuu huyo amesema: “Aliwahi kusema kuwa, mali na utajiri ambao Mungu
amempatia siyo kwa sababu yeye ni bora kuliko wengine, bali alimpa ili
awe kama bomba la kufikisha baraka kwa wengine.”
“Leo mtu anapata vimilioni kadhaa
tu anataka atembee juu ya migongo ya watu, anapata ka-cheo sijui ni
diwani, Mkuu wa Mkoa au wa Wilaya, halafu unaona wenzako si kitu. Tuache
na tutubu, acha kiburi namuomba Mungu atujalie roho hiyo ya
unyenyekevu,” amesema.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali,
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Dkt. Mengi atakumbukwa kwa kitendo
chake cha kuuchukia umaskini na zaidi kwa kazi mbalimbali ambazo
alishiriki.
“Bila shaka kila mmoja wetu
ameguswa kwa namna ya kipekee na mchango wa Dkt. Mengi. Kiukweli,
marehemu Dkt. Mengi, atakumbukwa kama mwanahabari, mwanaviwanda na
mfanyabiashara maarufu ambaye alitumia elimu, maarifa na utajiri wake
kwa ajili ya manufaa ya wote hususan watu wenye mahitaji maalum,”
amesema Waziri Mkuu.
Amewaomba wanafamilia wasimamie
makampuni ambayo Dkt. Mengi aliyaanzisha na kama watakwama wasisite
kuomba msaada serikalini kwani iko pamoja nao.
Akielezea wasifu wa baba yake,
mtoto wa marehemu, Bw. Abdiel mengi alisema siyo rahisi kuyazungumzia
yote kwa wakati mmoja mambo ambayo yamefanywa na Dkt. Mengi bali
aliwashukuru waombolezaji wote, viongozi wa Serikali na wafanyakazi wa
makampuni ya IPP kwa upendo wao.
“Mambo yote aliyoyafanya naweza
kumwelezea katika sifa tatu kubwa ambazo ni alikuwa mzalendo, mwenye
uthubutu na mwenye kupenda breakthrough. Alikuwa nafikiria tofauti na
wengine. Kwanza anajiuliza kwa nini nifanye jambo hili, na nifanyeje
ilikuwa ni suala la pili,” alisema.
Dkt. Mengi ambaye alifariki dunia
alfajiri ya Mei 2, mwaka huu akiwa kwenye matibabu huko Dubai, Falme za
Kiarabu, amezikwa katika makaburi ya familia huko Nkuu Sinde – Kisereni,
Machame, wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro. Ameacha mke na watoto wanne.
No comments :
Post a Comment