Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Muhammad Kambi (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu kuwepo kuendelea kuwepo kwa ugonjwa wa Homa ya Dengue nchini.
Baadhi ya waandishi wa habari waliojitokeza kusikiliza tamko la kuhusu kuwepo kwa ugonjwa wa Homa ya Dengue nchini wakati likitolewa na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Muhammad Kambi Jijini Dodoma.
…………………………
NA WAJMW-DODOMA
Serikali kupitia Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imezidi kutoa tahadhari ya
kuwepo kwa ugonjwa wa homa ya Dengue nchini hususani katika Jiji la Dar
Es Salaam na Tanga.
Tahadhari hiyo imetolewa leo na
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Muhammad Kambi wakati akizungumza na
waandishi wa habari katika ofisi za wizara hiyo zilizoko jijini Dodoma.
Prof. kambi amesema hadi kufikia
tarehe 6 Mei 2019, kati ya watu waliopimwa, wagonjwa 1237
wamethibitishwa kuwa na virusi au walikwishapata ugonjwa wa Dengue na
kati yao 1150 ni kutoka Dar Es Salaam, 86 ni kutoka Tanga na mtu mmoja
kutoka Singida.
Aidha, Prof Kambi amesema
takwimu za ugonjwa wa Dengue kwa kipindi cha Januari hadi Aprili 2019
zinaonesha mwenendo wa ugonjwa huu kuwa na idadi ya wagonjwa 1237, vifo
vya watu wawili na kuongeza kuwa waliofariki walikua na maradhi mengine.
Pamoja na hayo Mganga Mkuu huyo
wa Serikali amelipongeza jiji la Dar Es Salaam kwa kuanza kunyunyizia
dawa viuadudu (Biolarvicides) kwa ajili ya kuangamiza mazalia ya mbu ili
kupambana na ugonjwa huu.
Vile vile amesema Wizara
inaelekeza Mikoa na Halmashauri zote nchini kuendelea kuchukua hatua
katika kudhibiti ugonjwa huu ikiwa ni pamoja na kufukia madimbwi ya
maji, kunyunyizia dawa ya kuua viluwiluwi, kuondoa vitu vinavyosababisha
mazalia ya mbu, kufyeka vichaka, kufunika mashimo ya maji taka kwa
mifuniko pamoja kusafisha gata za paa la nyumba na kutoruhusu maji
kusimama.
Prof. Kambi amesema Wizara kwa
kushirikiana na Mikoa na Halmashauri zote nchini itaendelea kuchukua
hatua mbalimbali za kudhibiti ugonjwa huu ikiwa ni pamoja na kuendelea
kuangamiza mazalia ya mbu na viluwiluwi, kuweka mpango wa dharura wa
miezi sita kuanzia Mei mpaka Oktoba ili kukabiliana na ugonjwa huu. Pia
amesema Serikali imenunua Vitendanishi vyenye uwezo wa kupima wagonjwa
1870 na vimesambazwa kwenye vituo maalum vya ufuatiliaji wa ugonjwa huu
nchini kote.
Mwisho Prof. Kambi amewataka
wananchi kuendelea kuchukua hatua za kujikinga kuumwa na mbu kwa kuvaa
nguo ndefu, kutumia vyandarua vyenye viuatilifu, kutumia dawa za
kufukuza mbu na kuweka nyavu kwenye madirisha na milango ya nyumba za
kuishi ili kukabiliana na ugonjwa huu.
No comments :
Post a Comment