Thursday, May 9, 2019

MRADI WA LDFS UMEKUJA NA UFUMBUZI WA TATIZO LA UKAME NA USALAMA WA CHAKULA NCHINI


index

Na Ismail Ngayonga,MAELEZO
DAR ES SALAAM
UHARIBIFU wa mazingira umeendelea kuathiri kila sekta ya uchumi na maisha ya Watanzania, ambapo katika kipindi cha miaka 10 iliyopita kasi ya upoteaji wa misitu imezidi kuongeza kutokana na matumizi makubwa ya nishati itokanayo na misitu.
Kutokana na uharibifu huo, inaelezwa kuwa vyanzo vingi vya maji kwa sasa vimeharibiwa,
mvua zimekuwa hazitabiriki, ukame umeongezeka, rutuba ya ardhi imepungua, maporomoko ya ardhi katika maeneo ya milima yameongezeka, mafuriko yanaharibu miundombinu na mali na kupoteza maisha ya watu.
Utafiti umebaini kuwa kila mvua inapopungua kwa asilimia 10, pato la taifa linalotokana na kilimo hupungua kwa asilimia 2 na makisio hayo ya kitaalamu yanaeleza pia joto la dunia likiongezeka hadi kufikia nyuzijoto 2 za sentigredi juu ya wastani, mavuno ya mahindi hupungua kwa asilimia 13 na mavuo ya mpunga hupungua kwa asilimia 17.
Kwa msingi huo, Serikali ya Awamu ya Tano kuanzia mwaka wa fedha 2016/17 imedhamiria kuyaweka masuala ya mazingira kama sehemu ya mhimili wa ajenda ya uchumi na Maendeleo ya Taifa.
Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira inaratibu Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza Uzalishaji wa Chakula (LDFS) unaotekelezwa katika nchi 12 za Bara la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania, Kenya, Malawi, Ethiopia, Uganda, Burundi, Swazland, NigerIa ,Ghana, Bukinafaso, Niger na Senegal.
Mradi huo unatarajia kuipa serikali fursa ya kutambua teknolojia na maeneo yanayofaa kwa uvunaji wa mvua na  maeneo ya vyanzo vya maji kupitia teknolojia itakayosaidia kupunguza upotevu wa maji na kuongeza uzalishaji hasa kipindi cha kiangazi.
Aidha wananchi na vikundi mbalimbali vya wazalishaji wanatarajia kuwapatia mafunzo ya shamba darasa wananchi  kuhusu kilimo hifadhi na mbinu bora za kilimo rafiki kwa mazingira, uboreshaji na urutubishaji wa udongo, mbinu za kilimo misitu, kilimo cha makinga maji, kilimo cha mzunguko na usimamizi shirikishi wa kudhibiti wadudu na magonjwa ya mazao.
Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya mapato na matumizi kwa mwaka 2019/20, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Waziri Makamba anasema Serikali inatekeleza mradi wa LDFS katika kipindi cha  miaka mitano kuanzia Julai, 2017 hadi Septemba, 2022 na kutekelezwa katika maeneo yenye changamoto za ukame zilizopo katikati ya nchi na pwani.
Kwa mujibu wa Waziri Makamba anasema mradi huo unaofadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF) kupitia Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) utagharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 50 ambapo dola za Marekani milioni 7.156 zinatoka GEF na mchango wa nchi ni kiasi cha dola za Marekani milioni 42.94.
“Fedha zinazotolewa na GEF zinalenga kuchangia katika kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi, na Hifadhi ya Bioanuai na Usimamizi Endelevu wa Ardhi na utatekelezwa katika Kata ya Haubi katika Halmashauri ya Kondoa, Kata ya Sigili katika Halmashauri ya Nzega, Kata ya Mpambala Halmashauri ya Mkalama, Kata ya Sukuma, katika Halmashauri ya Magu na Shehia 8 katika Wilaya ya Micheweni Kaskazini Pemba” anasema Waziri Makamba.
Akifafanua zaidi Waziri Makamba anasema jumla ya Tsh. Bilioni 1.2 ziliidhinishwa katika mwaka 2018/19. Hadi kufikia Machi, 2019 kiasi cha Tsh. Milioni 667.9 kilitumika Tanzania Bara na kiasi cha Tsh. Milioni 158. 5 kwa upande wa Zanzibar.
Kwa ufupi hakuna sekta yoyote ya kiuchumi na kijamii isiyoathiriwa na uharibifu wa mazingira, na kwa msigi huo bila kuwekeza katika hifadhi ya mazingira, jitihada za uwekezaji katika sekta nyingine za kiuchumi na kijamii hazitazaa matunda tuliyoyatarajia.

No comments :

Post a Comment