Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya
ya Nzega kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo Agosti 17, 2018.
NA OWM,
NZEGA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza
wakuu wa wilaya nchini washirikiane na Madiwani katika halmashauri zao wafanye
tathmini ya mali zote zinazomilikwa na halmashauri vikiwemo vibanda vya
biashara ili kujiridhisha kama viwango vinavyotozwa vinalingana na hali halisi
ya uchumi kwa sasa.
Amesema licha ya tathmini hiyo kuwawezesha
kufahamu viwango vinavyotozwa, pia itasaidia halmashauri kubaini watu wa kati
ambao wanawatoza wafanyabiashara fedha nyingi na kuilipa halmashauri fedha
kiduchu, jambo linalochangia kuikosesha Serikali mapato inayostahili.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Ijumaa,
Agosti 17, 2018) wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri ya Mji wa Nzega
na wa Halmashauri ya wilaya ya Nzega pamoja na Madiwani katika ukumbi wa
Halmashauri ya Mji wa Nzega akiwa kwenye ziara yake ya kikazi wilayani Nzega,
Tabora.
Ametoa agizo hilo baada ya Mbunge wa Nzega
Mjini, Husein Bashe kuomba Serikali iingilie kati mgogoro uliopo baina ya
halmashauri na wafanyabiashara kuhusu mradi wa vibanda vya biashara katika eneo
la Soko Kuu la Nzega ambavyo vimejengwa na wafanyabiashara katika ardhi ya
halmashauri kwa makubaliano ya kulipa kodi.
Uongozi wa halmashauri ya Mji wa Nzega
uliamua kupitia upya mkataba wa mradi huo kwa sababu ulikuwa hauinufaishi,
hivyo ilianzisha mpango wa maboresho ambapo ilibaini kuwepo kwa watu wa kati
waliokuwa wakiwatoza wafanyabiashara zaidi ya sh 150,000 kwa mwenzi na kuilipa
halmashauri sh. 30,000 kwa mwezi.
Pia ilibaini kwamba baadhi ya wamiliki wa
awali wa vibanda waliviuza kwa wafanyabiashara wengine kwa bei kubwa bila ya
kuishirikisha halmashauri na ilivyotaka kuvichukua ili wafanyabiashara
waendelee kuwa wapangaji kwa lengo la kuondoa mtu wa kati, ndipo ulipoibuka
mgogoro wa umiliki wa vibanda hivyo.
Waziri Mkuu amesema migogoro ya aina hiyo
huwa haiishi kwa wakati katika maeneo mengi kwa sababu baadhi ya vibanda hivyo
vinamilikiwa na Wakuu wa Idara, Madiwani na baadhi ya watumishi katika
hailashauri husika, jambo linalozikosesha halmashauri mapato. “Wakuu wa wilaya
shughulikieni hili,”.
Pia, Waziri Mkuu amezishauri halmashauri
zinazomiliki vibanda vya biashara hususani kwenye maeneo yenye migogoro watumie
leseni za biasahara zinazofanyakazi kwa kuzitambua na kuingia mikataba na
wamiliki wake ili kuondoa uwepo wa mtu wa kati.
Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka watumishi
wa umma wanaomiliki vinanda vya biashara kwenye eneo hilo watoe taarifa za
umiliki wao ili kuondoa mgongano wa kimaslahi pindi wanapokuwa kwenye vikao vya
kujadili namna bora ya kuipatia ufumbuzi migogoro ya vibanda vya biashara
vinavyomilikiwa na halmashauri katika maeneo yao
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa
halmashauri na wilaya wawahamasishe wananchi kwenye maeneo yao juu ya umuhimu
wa kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), hivyo watakuwa wamejihakikishia
upatikanaji wa huduma za afya bure kwao na familia zao
Pia amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Tabora,
Bw. Agrey Mwanri kwa jitihada kubwa za kupanua wigo wa kuboresha huduma za afya
kupitia CHF, ambapo kwa mkoa huo wanachama wa mfuko huo wanaweza kutibiwa
kwenye hospitali zote za Serikali tofauti na maeneo mengine ambayo huduma hiyo
inaishia kwenye hospitali za wilaya tu.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Mbunge wa Bukene Selemani Zedi katika
mkutano wa hadhara aliouhutubia kwenye Uwanja wa Taifa wa Bukene Agosti
17, 2018. Katikati ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Tabora, Hassan
Kasubi.
Wananchi
wa Bukene wilayani Nzega wakimshangilia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
wakati alipowasili kwenye Uwanja wa Taifa wa Bukene kuhutubia mkutano
wa hadhara Agosti 17, 2018.
Wananchi
wa Bukene wilayani Nzega wakimshangilia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
wakati alipowasili kwenye Uwanja wa Taifa wa Bukene kuhutubia mkutano
wa hadhara Agosti 17, 2018.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa
Taifa wa Bukene wilayani Nzega, Agosti 17, 2018. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
No comments :
Post a Comment