Wataalam wa masuala ya
upimaji ardhi pamoja na maafisa mbalimbali kutoka katika ofisi za
Serikali za nchi zote mbili waliojumuika pamoja wilayani Tarime mkoani
Mara kupanga namna ya kutekeleza kazi ya uhakiki na uimarishaji wa
mipaka ya kimataifa kwa pamoja. Wa tatu kutoka kulia (walioketi) ni
Mkuu wa Msafara wa wataalam kutoka Tanzania Bw. Huruma Lugala na kulia
kwake ni Mkuu wa Msafara kutoka Kenya Bw. Julius Rotich.
Mkuu wa zoezi la Uhamasihaji
katika kazi ya kuhakiki na kuimarisha mipaka ya Kimataifa kati ya
Tanzania na Kenya Bw. Raymond Bagenda kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi akizungumza wakati wa kikao cha pamoja cha wataalam
wa masuala ya upimaji ardhi kutoka katika ofisi za Serikali za nchi zote
mbili. Kikao hiko kilichofanyika wilayani Tarime mkoani Mara kinapanga
namna ya kutekeleza kazi hiyo kwa pamoja. Kushoto ni Mkurugenzi
Msaidizi kutoka Ofisi ya Rais nchini Kenya inayohusika na Usimamizi wa
Mipaka ya Kimataifa (KIBO) Bw. Joseph Rotich.
Baadhi ya Wataalam wa masuala
ya upimaji ardhi pamoja na maafisa mbalimbali kutoka Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi na katika ofisi zingine za Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakifuatilia mazungumzo kuhusu namna
ya kutekeleza kazi ya uhakiki na uimarishaji wa mipaka ya kimataifa
kati ya Kenya na Tanzania.
…………………………………………………………………….
Na Rehema Isango, Tarime, Mara
Timu za watalaamu wa upimaji
ardhi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Tanzania na
taasisi za usimamizi wa Ardhi nchini Kenya zimekutana wilayani Tarime
mkoani Mara kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa kazi ya kuhakiki na
kuimarisha mpaka wa Kimataifa baina ya nchi hizi mbili.
Mapema mwezi Machi, Naibu Waziri
wa Adhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula alitangaza
azma ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanza kuimarisha
mipaka yake kwa nchi jirani za Kenya na Uganda baada ya ziara yake ya
kukagua mpaka wa Tanzania na Kenya katika Mbuga ya Wanyama ya Taifa ya
Serengeti iliyopo mkoani Mara.
Hatua ya uhakiki na uimarishaji
wa alama za mipaka ya mikataifa inatokana na mpaka huu kuwa wa siku
nyingi na haukuwa wazi katika maeneo mengi pia baadhi ya alama hizo
kuharibiwa, kung’olewa au kuchakaa na hivyo kusababisha Serikali pande
zote kushindwa kusimamia kwa ufanisi shughuli za mipakani, rasilimali za
nchi pamoja na ulinzi na usalama.
Katika uimarishaji wa alama hizo
za mipaka hivi sasa, kutaongezwa alama mpya ndogo zinazoonana kwa umbali
wa mita 100 pamoja na kubainisha eneo la ardhi huru kwa kila upande wa
nchi (buffer zone).
Mpaka kati ya Tanzania na Kenya
una jumla ya urefu wa Kilommita 760 kuelekea bahari ya Hindi ambapo
awamu ya kwanza ya kazi ya uimarishaji mpaka inayofanyika hivi sasa
itahusisha urefu wa Kilomita 238 kutoka kando ya Ziwa Victoria mkoani
Mara hadi Ziwa Natron mkoani Arusha.
Baadaye, kazi ya uhakiki na
uimarishaji wa mipaka itaendelea katika mikoa ya Kilimanjaro na Tanga na
kisha itafanyika katika maeneo yote yanayohusika na mipaka ya
kimataifa nchini.
Uimarishaji wa mipaka ya
kimataifa nchini umefanyika mara ya mwisho mwaka 1975 kwa kurudishia
alama ambazo ziliondolewa na kuongeza nyingine mpya kwa kuzingatia
alama zilizopo.
Mbali na Kenya nchi nyingine
zinazopakana na Tanzania ni; Msumbiji, Malawi, Zambia, Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Kongo, Burundi, Rwanda, Uganda pamoja na visiwa vya
Komoro na Shelisheli.
No comments :
Post a Comment