Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) Charles Kichere akizungumza wakati wa hafla fupi
ya uzinduzi rasmi wa utoaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo
walio kwenye sekta isiyo rasmi iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Afisa wa Kodi wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) akimuonesha Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo (Mwenye
suti nyeusi kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Sophia Mjema namna
ya kuingiza taarifa za mfanyabiashara mdogo kwenye komputa hadi
kupatikana kwa kitambulisho cha mfanyabiashara husika. Hayo yamejiri
wakati wa hafla fupi ya uzinduzi rasmi wa utoaji wa vitambulisho vya
wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi iliyofanyika leo
jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Shirikisho la
Wamachinga wa Kariakoo jijini Dar es Salaam Steven Lusinde akizungumza
wakati wa hafla fupi ya uzinduzi rasmi wa utoaji wa vitambulisho vya
wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi iliyofanyika leo
jijini hapa.
Mmoja wa wamachinga akipokea
kitambulisho wakati wa hafla fupi ya uzinduzi rasmi wa utoaji wa
vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi
iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wamachinga
waliohudhuria uzinduzi rasmi wa utoaji wa vitambulisho vya
wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi iliyofanyika leo
jijini Dar es Salaam.
……………………………………………………………………………………….
Na Veronica Kazimoto,-Dar es Salaam,
Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) leo imezindua rasmi utoaji wa vitambulisho vya
Wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi ikiwa ni pamoja
na Wamachinga.
Akizungumza
wakati wa hafla fupi ya uzinduzi huo iliyofanyika jijini Dar es Salaam,
Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo Charles Kichere amesema kuwa, utoaji wa
vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo unatokana na marekebisho ya
Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya
Mwaka 2015 yaliyofanywa na Bunge la
Bajeti la Mwaka wa Fedha 2017/2018 ambapo moja ya marekebisho hayo ni
kuwatambua na kuwapatia vitambulisho maalum wafanyabiashara wadogo walio
kwenye sekta isiyo rasmi.
“Baada
ya marekebisho ya Bunge la Bajeti la Mwaka wa Fedha 2017/2018, zoezi
hili la kuwatambua wafanyabiashara wadogo lilianza kutekelezwa na
Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama
vile Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini
(RITA) pamoja na Idara ya Uhamiaji”, alisema Kichere.
Kichere
alieleza kwamba, TRA kwa kushirikiana na wadau hao, ilianza kutekeleza
jukumu hilo kwa kuutambua Umoja wa Wamachinga wa Kariakoo jijini Dar es
Salaam na kufanikiwa kuwapatia vitambulisho vya Taifa na Namba ya
Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) ambapo leo hii baadhi yao wamepatiwa
vitambulisho maalum vya wafanyabiashara wadogo kama ishara ya uzinduzi
wa utoaji wa vitambulisho hivyo.
Ameongeza
kuwa, zoezi la kutambua vikundi mbalimbali vya wafanyabiashara wadogo
na kuwapatia Kitambulisho cha Taifa na Namba ya Utambulisho wa Mlipa
kodi linaendelea kufanyika nchi nzima na kubainisha kuwa, ili
wafanyabiashara wadogo waweze kupata vitambulisho hivyo maalum,
wanatakiwa kujiunga katika vikundi vinavyotambuliwa kisheria na
Serikali, kuwa na Kitambulisho cha Taifa, kuwa na Namba ya Utambulisho
wa Mlipakodi ya kikundi alichojiunga nacho pamoja na kuchangia shilingi
10,000.
“Zoezi
la kuwatambua wafanyabiashara wadogo linaendelea kufanyika nchi nzima
na vitambulisho maalum vinavyotolewa kwa wafanyabiashara hao vitadumu
na kutumika kwa kipindi cha miaka mitatu (3). Maelezo ya mfanyabishara
mdogo yaliyopo kwenye kitambulisho hicho maalum ni pamoja na jina na
picha ya mfanyabiashara, jina la eneo analofanyia biashara, Namba ya
Utambulisho wa Mlipakodi na Sahihi ya mfanyabiashara husika”, Alifafanua
Kichere.
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam Mhe. Sophia Mjema
ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais John
Pombe Magufuli kwa kuwatambua wafanyabiashara wadogo ili waweze kupiga
hatua kiuchumi kutoka daraja la chini hadi la kati na hatimaye kuweza
kuchangia maendeleo ya nchi kupitia ulipaji wa kodi mbalimbali.
“Lakini
kwanza naomba nimshukuru Mhe. Rais wetu John Pombe Magufuli kwa hii
ndoto yake ya kuwasaidia wanyonge waliokuwa wanafanya biashara ndogo
ndogo kutambulika na Serikali na kisha waondoke katika hali ya daraja la
chini na kufikia daraja la kati. Nafurahi kuwaeleza kwamba, ndoto ya
Mhe. Rais wetu imetimia”, alisema Mjema.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la Wamachinga wa Kariakoo jijini
Dar es Salaam Steven Lusinde amesema kuwa, wamefurahishwa na azma ya
Serikali ya kuwatambua wafanyabiashara walio kwenye sekta isiyo rasmi
kwa kuwa wamekuwa na hamu ya kuchangia maendeleo ya Taifa kwa muda
mrefu.
“Sisi
wamachinga tumekuwa na hamu kubwa sana ya kuchangia Taifa letu kwa
sababu tunaamini chochote tunachokiona katika nchi hii bila sisi
kuchangia hakiwezi kwenda”, alieleza Lusinde.
Moja
ya majukumu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania ni kukusanya mapato ya
Serikali sambamba na kutoa elimu kwa walipakodi na watanzania kwa ujumla
ili kuongeza uhiari wa ulipaji kodi na kuongeza mapato ya Serikali
ambayo yanahitajika katika kuleta maendeleo ya nchi pamoja na wananchi
wake.
No comments :
Post a Comment