Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa George Simbachawene amesema kuwa
Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria za Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
Simbachawene ameyasema hayo leo
Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa
Jimbo la Chemba Juma Nkamia kuhusu Wakuu wa Wilaya na Mikoa kuwa wababe
katika maeneo yao ya kazi.
“Wakuu wa Mikoa na Wilaya
wanasimamia maeneo yao kwa mujibu wa sheria na wana haki ya kuwachukulia
hatua watumishi ambao hawatekelezi majukumu waliyopewa,” alifafanua
Simbachawene.
Aliendelea kwa kusema kuwa, hata
kama kuna Wakuu wa Mikoa na Wilaya ambao ni wababe katika maeneo yao ya
kazi hauwezi kusema kila Mkuu wa Mkoa au Wilaya aliyechukua hatua dhidi
ya mtumishi ambaye hawajibiki katika kazi yake ni mbabe au muonevu.
Aidha, Simbachawene amesema kuwa
ni wakati sasa wa watumishi wa Umma kutekeleza wajibu wao na kuacha
kufanya kazi kwa mazoea. Kwani hakuna kiongozi ambaye ataweza kumchulia
hatua mtumishi ambaye anawajibika na kazi zake kama alivyopangiwa.
Vile vile amesema kuwa, wakuu hao
wa Mikoa na Wilaya wamekuwa wakifanya kazi nzuri katika maeneo
wanayoyasimamia, kutokana na watumishi wengi wa Serikali walikuwa
wamejisahau kutekeleza wajibu wao na kufanya kazi kimazoea.
No comments :
Post a Comment