Dodoma, Ijumaa, 3 Februari, 2017:
Serikali imetolea ufafanuzi kuhusu kero
mbalimbali za Wabunge ikiwemo kuhusu maslahi ya walimu nchini na kadhia
ya riba kubwa katika mabenki. Ufafanuzi huo umetolewa leo wakati wa
vikao vya Bunge vinavyoendelea mjini hapa.
Stahili za Walimu
Serikali imesema kuwa ni kweli
inadaiwa na walimu madeni yasiyo ya mishahara yanayofikia shilingi
26,042,581,697 hadi kufikia Desemba,2016. Naibu Waziri, Ofisi ya Rais
(TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo amesema deni hilo litaanza kulipwa hivi
karibuni kwa kuwa deni hilo lote limeshahakikiwa.
Kuhusu madeni ya mishahara, Naibu
Waziri Jafo ameliambia Bunge kuwa uhakiki wa deni la shilingi
10,034,495,540 umekamilika na kinachosubiriwa ni kulipwa kupitia akaunti
ya mtumishi anayedai. Ameongeza kuwa, deni linalobaki ni shilingi
8,067,922,773 ambalo linaendelea kuhakikiwa ili nalo liweze kulipwa.
Upungufu wa Vyumba vya Madarasa na Maabara
Akijibu hoja kuhusu mkakati wa
Serikali wa kupunguza tatizo la vyumba vya madarasa na maabara, Naibu
Waziri Jafo amesema kuwa, Serikali katika bajeti ya mwaka 2016/17
imetenga jumla shilingi bilioni 29.3 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya
madarasa 3,306 kwa shule za msingi na shilingi bilioni 16.3 zimetengwa
kujenga vyumba vya madarasa 1,047 kwa shule za sekondari.
Ameliambia Bunge kuwa utekelezaji wa
malengo hayo pia utafanywa kupitia Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya
Sekondari (MMES II) ambako pia zimetengwa shilingi bilioni 23.6 kwa
ajili ya ujenzi na ukarabati wa vyumba 1,642. Upande wa maabara Serikali
imetenga shilingi bilioni 18.9 kwa ajili ya ukamilishaji wa vyumba
2,135.
Kumuinua Mwanamke Kiuchumi
Serikali imesema kuwa hadi kufikia
Desemba, 2016 Benki ya Wanawake imeshafungua matawi katika mikoa saba
(7) ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Iringa, Njombe, Mbeya na Ruvuma
ambapo huduma mbalimbali za kuwainua akina mama kiuchumi zimetolewa.
Katika huduma hizo, dirisha la kuhudumia maeneo ya Iringa na Makambako
pekee hadi kufikia Desemba, 2016 jumla ya Wajasiliamali 6,850, wanawake
5,350 na wanaume 1,500 walipatiwa.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Hamis
Kigwangalla ambapo aliongeza kuwa Benki hiyo imefungua vituo vya kutolea
mikopo 252 kufikia Desemba 2016.
Riba Kubwa katika Mabenki
Serikali imesema kuwa Benki Kuu ya
Tanzania (BOT) haiwezi kuweka ukomo wa riba za mabenki kwani si tu
inapingana na jukumu lake la msingi la kusimamia mabenki, bali pia hilo
liinapingana na mfumo wa uchumi wa soko huria. Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango, Mhe.Dkt. Ashatu Kijaji ametoa kauli hiyo wakati akijibu hoja
inayohusu uwepo wa riba kubwa katika mabenki.
Dkt.Kijaji ameeleza kuwa, suala la
Benki Kuu kutoa maelekezo kwa mabenki kutumia viwango fulani vya riba
katika biashara zao, kutaifanya Benki Kuu kukosa nguvu na mamlaka ya
kuyachukulia mabenki hatua endapo yatapata hasara kwa kutumia riba
ambayo Benki Kuu imeelekeza. “Benki Kuu haina mamlaka kisheria ya kuweka
ukomo wa riba au riba elekezi itakayotumiwa na mabenki katika kutoa
mikopo,” alisema.
Hali ya Kituo cha Biashara cha Taifa Nchini Uingereza
Serikali imesema kuwa imekifunga rasmi
Kituo cha Biashara cha Taifa kilichopo mjini London, Uingereza kutokana
na changamoto mbalimbali za kituo hicho ikiwemo ufinyu wa bajeti pamoja
na upungufu wa rasilimali watu.
Akijibu hoja hiyo Bungeni leo kwa
niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Naibu Waziri wa Fedha
na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema, badala yake, shughuli zote
za kituo hicho zimehamishiwa Ubalozi wa Tanzania uliopo mjini London.
Imetolewa na:
Idara ya Habari-MAELEZO.
No comments :
Post a Comment