Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa
Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bw. Bernard Konga (kushoto) akizungumza na
waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam (hawapo pichani) kuhusu
maboresho yaliyofanywa na Mfuko. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Uhai wa
Mfuko Bw. Baraka Maduhu.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Bw.
Bernard Konga akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari. Kushoto ni
Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti Bi. Angela Mziray na kulia ni
Kaimu Mkurugenzi wa Uhai wa Mfuko Bw. Baraka Maduhu.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa
Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bw. Bernard Konga (kushoto) akizungumza na
waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu ushiriki wa Mfuko katika
kupunguza magonjwa yasiyoambukiza . Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Masoko
na Utafiti Bi. Angela Mziray.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa
Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bw. Bernard Konga (wa pili kutoka kushoto)
akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu ongezeko la
usajili wa vituo vya kutolea huduma kwa wanachama wa Mfuko. Kulia ni
Kaimu Mkurugenzi wa Uhai wa Mfuko Bw. Baraka Maduhu.
Baadhi ya waandishi wa habari wakifuatilia maelezo ya Kaimu Mkurugenzi wa NHIF Bw. Bernard Konga .
(Picha na Frank Mvungi-Maelezo
…………..
Na Grace Michael
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya
(NHIF) umefanikiwa kufikia makundi mbalimbali wakiwemo Wabunge wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari
leo Jijijini Dar es salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard
Konga amesema kuwa mafanikio haya yamefikiwa chini ya Serikali ya Awamu
ya Tano ambayo imejipanga kuhakikisha zaidi ya asimilia 85 ya Watanzania
wanakuwa kwenye Mfumo wa Bima ya Afya ifikapo mwaka 2020.
“Sisi kama Mfuko tunajivunia sana
kufikia makundi mengi ya wananchi na kuyahudumia hususan kundi la
waheshimiwa wabunge ambao awali hawakuwemo lakini pia kundi la watoto
ambalo nalo ni muhimu sana,” alisema Bw. Konga.
Alisema kuwa kitendo cha Wabunge
kuwa ndani ya huduma za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya utasaidia kwa
kiasi kikubwa kwa kuwa wao ndio wawakilishi wa wananchi hivyo watasaidia
kuwahamasisha wananchi kujiunga na Mfuko.
Bw. Konga alieleza kuwa pamoja na
kuwepo kwa ongezeko la wanachama, Mfuko pia umeongeza usajili wa vituo
vipya 92 na kufanya idadi ya vituo vinavyohudumia wanachama kuwa ni
6,998 hivyo kuwezesha kuwa na mtandao mpana wa huduma kwa wanachama wa
NHIF.
Alitumia fursa hiyo pia kusema
kuwa Mfuko umeshiriki kwa kiasi kikubwa kupunguza magonjwa hususan
magonjwa yasiyoambukiza kutokana na kujikita katika utoaji wa elimu kwa
wananchi ya namna ya kujikinga na magonjwa hayo lakini pia kuendesha
zoezi la upimaji wa afyua bure katika maeneo mbalimbali vijijini.
“Tunao mpango wa elimu ya kata kwa
kata ambapo kwa mwaka 2016 jumla ya kata 560 zilifikiwa na mpango huo
hivyo sisi kama Mfuko tumetekeleza jukumu hili na tunaendelea kulifanya
kupitia ofisi zetu za mikoani,” alisema.
Akizungumzia suala la uboreshaji
wa miundombinu ya afya pamoja na ujenzi wa hospitali, Bw. Konga alisema
kuwa, Mfuko umewekeza katika Vituo vya Kisasa vya uchunguzi wa magonjwa
vilivyoko Dodoma na kutokana na uwekezaji huu umekwenda sambamba na
mkakati wa Serikali wa Dodoma kuwa Makao Makuu ya nchi.
Alisema kuwa ujenzi wa Hospitali
kubwa iliyopo Chuo Kikuu cha Dodoma inayojulikana kama Benjamin Mkapa
imelenga kusaidia Serikali hasa katika kuondokana na gharama za
kusafirisha wagonjwa nje ya nchi hivyo uwekezaji huo unayo manufaa
makubwa kwa Watanzania kwa ujumla.
Aliwahakikishia wanachama wa Mfuko
kuwa Mfuko uko imara na utawahudumia kwa kiwango kinachotakiwa
kulingana na dhamana kubwa iliyopewa ya kutoa huduma za matibabu kwa
wanachama wake.
“Mfuko uko imara kabisa, wanachama
wajue hilo na sisi tunayo dhamana ya kulinda uhai wa Mfuko hivyo rai
yetu ni kwa kila mwanachama ama Mtanzania kulinda huduma za Mfuko ili
ziweze kutoka kwa walengwa na hatimaye kutimiza lengo lake.
No comments :
Post a Comment