Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Sekta ya Kilimo inachangia ajira
takribani asilimia 70 ya Watanzania ambapo imekuwa ikitegemewa kusaidia
kufanikisha juhudi za kupunguza umaskini hasa Vijijini na kuchochea
mapinduzi ya Viwanda. Kwa mwaka 2015 ukuaji wa sekta hiyo ulikuwa ni
asilimia 3.0.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Bajeti Josephat Kandege
ameyasema hayo leo Bungeni,
Mjini Dodoma alipokuwa akisoma taarifa ya utekelezaji ya kamati hiyo kwa
kipindi cha mwezi Januari 2016 hadi Januari 2017.
Kandege amesema kuwa sekta hiyo
imekuwa ikitegemewa na watanzania wengi katika kuwaingizia kipato na
hata kuinua uchumi wa Nchi, lakini wakulima wamekuwa wakipata changamoto
mbalimbali katika Sekta hiyo kama vile gharama kubwa ya pembejeo,
ukosefu wa masoko ya uhakika na idadi ndogo ya wataalamu wa Kilimo.
“Kamati inaishauri Serikali kuanza
kutekeleza mikakati madhubuti ya kuinua sekta hii kwa kuboresha kilimo
cha umwagiliaji, kuboresha teknolojia ya Kilimo, kuwezesha uanzishwaji
wa viwanda vingi vya usindikaji wa mazao ya kilimo na kusambaza maafisa
ugani wa kutosha katika maeneo yote ya nchi,” alisema Kandege.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo
la Sumve, Richard Ndasa amesema kuwa Kilimo kinahitaji uwekezaji mkubwa
hivyo ni vyema Serikali ikawekeza katika sekta hiyo kikamilifu ili
kuinua uchumi wa Nchi na mtu mmoja mmoja.
Akijibu hoja hizo, Naibu Waziri wa
Kilimo Mifugo na Uvuvi Ole Nasha amesema kuwa Wizara hiyo imejipanga
kupambana na changamato za pembejeo ambazo zimekuwa zikipatikana kwa
gharama ya juu maeneo mengi nchini.
Hata hivyo amesema kuwa wizara
hiyo iko katika mkakati wa kuanza kuzalisha mbolea ndani ya nchi ili
kupunguza gharama ya mbolea na ili iweze kuuzwa kwa bei moja nchi nzima.
No comments :
Post a Comment