Tuesday, April 12, 2022

Serikali yavuna Sh143 bilioni kutoka Airtel

airtel pic

By Mwandishi Wetu

Dodoma. Wakati Kampuni ya Mawasiliano ya simu ya Airtel Tanzania Plc ikiikabidhi Serikali Sh...

143 bilioni kama gawio, mchango wa uwezeshaji na mauzo ya minara, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amezitaka taasisi binafsi ambazo Serikali imewekeza hisa hata kama ni asilimia moja kuhakikisha zinajiendesha kwa ufanisi na kulipa gawio stahiki serikalini.
Aidha, amezitaka taasisi zisizotoa gawio kujitathmini kwa kuwa Serikali iliwekeza ili faida itumike kwa maendeleo ya wananchi.
"Taasisi ambazo bado zinatoa gawio dogo na zile ambazo bado zinajiendesha kwa faida, lakini hazitoi gawio stahiki zinatakiwa kujitathmini na kuhakikisha zinafanya vizuri na kulipa gawio serikalini," amesema Dk Mpango.
Dk Mpango ametoa maagizo hayo wakati akipokea hundi ya Sh143 bilioni iliyotolewa na Airtel Tanzania Plc kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ikiwa ni gawio, mchango wa uwezeshaji na mauzo ya minara, Jumanne, Aprili 12, 2022. Airtel Tanzania inamiliki asilimia 51 ya hisa zote wakati Serikali ni mmiliki kwa asilimia 49.
Kampuni hiyo ya pili kwa ukubwa ikimiliki wa soko la mawasiliano ya simu nchini, imesema kati ya fedha hizo, Sh88 bilioni ni gawio, Sh12 bilioni mchango wa uwezeshaji (Support Services Agreement (SSA) na Sh43 bilioni ni kutokana na mauzo ya minara ya mawasiliano ya Airtel kwenda kwa Minara Tanzania Limited.
Akikabidhi hundi hiyo ya mfano kwa Dk Mpango, Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi  Airtel Tanzania Plc , Gabriel Malata amesema Sh88 bilioni ambacho Serikali imelipwa kimeweka rekodi ya kuwa kiasi cha juu kulipwa kama gawio kwa makampuni ambayo Serikali inamiliki hisa.
"Tunapongeza juhudi za Serikali za kuweka mazingira bora ya uwekezaji kwa mfumo wa ubia, ambapo leo hii tunashuhudia mafanikio mazuri ya Airtel Tanzania" amesema Malata.
Amesema kwa miaka mitatu sasa, Airtel Tanzania Plc imelipa kwa Serikali zaidi ya Sh200 bilioni zinazotokana na gawio, mchango wa uwezeshaji wa huduma pamoja na malipo mbalimbali. Pia, imeweza kulipa ada na tozo zilizowekwa kwa mujibu wa sheria jumla ya Sh97 bilioni kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
Akizungumzia maendeleo ya kampuni hiyo, Malata alisema; "Ninayo furaha kukufahamisha kuwa Airtel Tanzania imekuwa mstari wa mbele kwenye kuunga mkono juhudi mbalimbali za serikali kulingana na hali ya biashara yetu.
Kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021 Airtel imetoa fursa za ajira zaidi ya 350,000, kati ya hizi zipo ajira za moja kwa moja na zile ambazo sio za moja kwa moja. Nia yetu ni kuendelea kutengeneza fursa nyingi za ajira kwa manufaa ya Watanzania."
Aidha, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa mafanikio chanya ya kampuni hiyo kufikia kiasi cha kulipa serikalini gawio hilo.
Dk Mpango ambaye alimwakilisha Rais Samia amesema Serikali  itaendelea kuweka mazingira mazuri na endelevu ya kufanya biashara.
Aidha, Dk Mpango amempongeza Msajili wa Hazina  kwa kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa makubaliano yanayowezesha kupatikana kwa fedha na  Airtel kuendelea kulipa Sh1 bilioni kila mwezi.
"Tukio hili la leo linaashiria uwepo wa mazingira mazuri ya kiutendaji na mahusiano thabiti ya kibiashara baina ya wabia.  Mapato haya yaliyopatikana yana faida kubwa katika kuchangia miradi mikubwa ya maendeleo nchini na kuboresha huduma za jamii ikiwemo afya, elimu na maji kwa Watanzania wote. Niwasihi tena tuendeleze jitihada hizi ambazo ndiyo chachu ya maendeleo ya nchi yetu na manufaa kwa kila mwananchi," amesema Dk Mpango.
Naye Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto akizungumza katika hafla hiyo amesema  mikataba iliyosainiwa baina ya Serikali na Bharti Airtel ambayo ilikuwa na mambo makubwa na yenye tija kwa wabia wote na wananchi kwa ujumla wamesimamia vyema na matokeo yanajidhihirisha katika ufanisi wa mapato na michango isiyo ya kodi ambayo wameitoa.
Ofisi ya Msajili wa Hazina ikifuata Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 pamoja na mambo mengine inashauri na kusimamia uwekezaji katika mashirika, taasisi za umma, wakala za serikali na kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache sambamba na kuhakikisha uwekezaji unaleta tija kwa kutoa gawio na michango mingine serikalini.
Aidha, amesema Ofisi ya Msajili wa Hazina imeendelea kupata mafanikio katika ukusanyaji wa fedha za Serikali.
"Kwa mwaka huu unaoendelea 2021/22, ambapo katika kipindi cha miezi tisa hadi kufikia Machi 2022, Ofisi imefanikiwa kukusanya Sh556 bilioni ikiwa ni ufanisi wa asilimia 106 ya lengo la kukusanya Sh525.49 bilioni katika kipindi hicho," amesema.

No comments :

Post a Comment