
Waziri wa Afya,Ummy Mwalimu akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya miaka mitano ya kampeni ya Nyumba ni Choo jijini Dar es Salaam leo Jumatatu Aprili 11, 2022.Picha na Michael Matemanga
Dar es Salaam. Serikali imetaja eneo ambalo kwa sasa linakwenda kupewa kipaumbele katika usafi wa
afya na mazingira kuwa ni uboreshaji wa hali ya vyoo mashuleni utakaohusisha kuongeza matundu na upatikanaji wa maji safi na salama.Hayo yanakwenda kufikiwa wakati Serikali ikiwa imetoa kiasi cha Sh150 bilioni katika awamu ya pili ya kampeni ya Nyumba ni Choo, huku uboreshaji huo ukitazamiwa kufanyika katika shule za msingi na sekondari.
Hayo yamesemwa leo Jumatatu Aprili 11, 2022 na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati wa maadhimisho ya kilele cha miaka mitano ya kampeni ya Nyumba ni Choo.
“Eneo tunalokwenda kulipatia kipaumbele ni vyoo shuleni, tuongeze matundu na kujenga vyoo bora, kuna shule unatembelea zina watoto 2000 mpaka 3000 ina matundu matano.
“Mwongozo wa Wizara ya Elimu unasema tundu moja kwa wasichana 20 hivyo ni lazima tuhakikishe tunafanya kazi kwa nguvu zote kujenga vyoo mashuleni,” amesema Waziri Ummy.
Pia ametaja upatikanaji wa maji kwenye shule nyingi kuwa bado haukidhi mahitaji ya watoto waliopo hivyo bado kunakuwa na changamoto katika masuala ya afya.
“Bado shule zetu hazina maji, lakini pili vyoo vilivyopo ni vichafu awamu hii lazima tuhakikishe shule za msingi na sekondari zinakua na vyoo bora na maji ya kutosha hivyo kupitia awamu hii ya pili tunaendelea kuhakikisha tunaboresha hali ya vyoo mashuleni,” amesema.
Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, David Concar amesema wamekuwa wakifadhili kampeni hiyo wakifanya kazi kwa kushirikiana kati ya Tanzania na Uingereza kupitia UKaid.
“Leo tumefikia asilimia 72 kazi kubwa sana imefanyika. Kufanikiwa kwa kampeni hii kumetokana kwa kufanya kazi kwa pamoja kati ya Sekta ya umma na sekta binafsi kwa pamoja na hii imesaidia kwa kiasi kikubwa kubadilisha mtazamo wa wananchi walio wengi,” amesema Balozi Concar.

No comments :
Post a Comment