Tuesday, April 12, 2022

Majaliwa aipa kazi NMB ikizindua Teleza Kidijitali

NMB PIC

By Mwandishi Wetu

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezitaka taasisi za fedha kubuni mikakati na mbinu zitakazowezesha watanzania wengi zaidi kupata huduma rasmi za kibenki kwa

gharama nafuu ili kujiongezea kipato na kujikwamua na umasikini.
Ametoa wito huo Jumatatu Aprili 11, 2022 katika hafla ya huduma mpya ya Teleza Kidijitali ya benki ya NMB, iliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Morena jijini Dodoma. Amezishauri taasisi nyingine za kifedha kuiga kutoka kwa NMB katika utoaji wa huduma kwa njia hiyo.
Majaliwa amesema taasisi hizo hazina budi kuiunga mkono Serikali kwa kubuni mikakati mbalimbali ya kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika kukuza uchumi sambamba na kubuni masuluhisho rahisi kwa watumiaji wa kawaida.
Amesema benki nchini hazina budi kubuni zaidi namna ya kutafuta suluhisho katika sekta za kifedha.
“Hongereni NMB kwa ubunifu huu ambao utavutia makundi yote ya kijamii, huduma hii itawezesha wateja wenu kupata huduma ya mikopo kiganjani,” amesema Majaliwa.
Amesema amevutiwa na huduma hizo ikiwemo ya MshikoFasta ambayo inakwenda kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa haraka kwa mama lishe na baba lishe, bodaboda, wafanya biashara wadogo na wananchi wote wa kawaida.
Amesema wakati Rais Samia Suluhu Hassan alipozungumza na wamachinga hivi karibuni aliziasa taasisi za fedha kulizingatia kundi hilo muhimu na zihakikishe huduma za kifedha zinakuwa rafiki kwao, hivyo ameipongeza NMB kwa utekelezaji huo.
 “Ninaipongeza NMB kwa kuja na suluhisho hili, naamini asilimia kubwa ya Watanzania watanufaika sana na huduma hii katika kipindi hiki ambacho dunia inapambana na changamoto ya ajira kwa vijana. Hii ni fursa ya vijana kujipatia mitaji.”
Amesema huduma hiyo ya mikopo ya kidigitali inakwenda kumaliza kabisa tatizo la ugumu wa kupata mikopo.
“Hii ni hatua kubwa sana kwenye sekta ya kibenki Tanzania. Tukio hili linapeleka ujumbe kwa Watanzania wa kuwataka wasihangaike kupata mikopo ya kuanzisha biashara  zao kwa kuwa fedha ipo NMB.”
Pia, Majaliwa amesema Serikali kwa upande wake inaendelea kuimarisha usalama wa mtandao kwa kuwajengea uwezo watalaamu wa TEHAMA pamoja na kujenga mazingira wezeshi ya kisera, sheria, mifumo, miundombinu na kuhakikisha uwepo wa wataalamu hao kwenye nyanja zote muhimu za ubobezi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande amesema huduma ya Teleza Kidijitali ni ishara kuwa benki hiyo imejipanga kupanua wigo wa huduma kote nchini.
Amesema kuwa maboresho yaliyofanyika katika sekta ya fedha yameleta matokeo chanya ambapo mikopo kwa sekta binafsi imeendelea kuimarika na kuongezeka kutoka Sh20.31 trilioni mwaka 2020 hadi kufikia Sh22.34 trilioni kwa mwaka 2021.
Aidha, katika mwaka 2021, amana za benki za biashara ziliendelea kuongezeka hadi kufikia Sh26.81 trilioni ikilinganishwa na Sh23.81 trilioni kwa mwaka 2020, sawa na ukuaji wa asilimia 13.0.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Profesa Florence Luoga amesema malengo ya BOT ni kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata huduma jumuishi za kifedha za uhakika chini ya kilomita 15.
Amesema uzinduzi wa huduma hii unakidhi malengo ya BOT ya kuhakikisha mabenki yanajenga uwezo wa kuwafikia wananchi pale walipo na kwa namna rafiki inayoweza kuongeza ari kwa wananchi kutumia huduma za kifedha. Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna amesema lengo la kuanzisha Teleza Kidijitali ni kuendelea kuchagiza ukuaji wa teknolojia kwa kuwa huduma hizo zinakwenda kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi kwa jamii.
Amesema mbali na huduma hiyo, pia benki ya NMB imetenga Sh200 bilioni kwa ajili ya mikopo kwa wafanyabiashara wadogo maarufu machinga ili kuwawezesha kukuza mitaji yao.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NMB, Dk Edwin Mhede amesema malengo ya benki hiyo ni kuwafikia Watanzania kwa kasi na ubora wa huduma na uzinduzi wa Teleza Kidijitali ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati huo.

No comments :

Post a Comment