Saturday, April 9, 2022

Mara kinara uvamizi hifadhi za Taifa

mara pic

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula akifungua mkutano kwaajili ya utengenezaji wa mpango wa utekelezaji wa maazimio ya baraza la mawaziri kuhusu migogoro ya ardhi mkoani Mara. Picha na Beldina Nyakeke

By Beldina Nyakeke

Musoma. Mkoa wa Mara umetajwa kuwa mkoa unaoongoza nchini kwa wakazi wake

kuvamia maeneo ya hifadhi za Taifa hali ambayo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa migogoro ya ardhi mkoani humo.

Hayo yamesemwa mjini Musoma leo Aprili 9, 2022 na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula wakati akifungua kikao cha kamati ya mawaziri wa kisekta kujadili namna ya kutekeleza maazimioya Baraza la MawaIri kuhusu maamuzi yaliyotolewa kuhusina na migogoro ya ardhi nchini katika vijiji 975 nchini.

Amesema kuwa hali hiyo imesababishwa na sababu mbalimbali ikiwemo viongozi wanaohusika kutokutimiza wajibu wao pamoja na uvunjaji wa sheria kwa makusudi uliofanywa na wananchi.

Kutokana na hali hiyo, Waziri Mabula ametoa onyo kwa wananchi kutotumia hisani iliyofanwa na Rais ambayo itapelekea umegwaji wa baadhi ya maeneo kutoka hifadhini na kurejeshwa kwa wananchi kwaajili ya matumizi yao.

"Leo Baraza la Mawaziri liliamua kuwa baadhi ya vijiji vimegewe maeneo kutoka hifadhini baada ya kazi iliyofanywa na kamati iliyoundwa na Rais sasa msitegemee kuwa mwaka kesho tena kutakuwa na umegaji wa maeneo naomba tuzingatie sheria na taratibu maana hii hisani haitarudi tena" amesema

Amewataka wakuu wa mikoa, wilaya pamoja na viongozi wa kisekta kuanzia ngazi ya mkoa hadi vijiji kutimiza wajibu na majukumu yao kwa mujibu wa sheria ili kuepuka migogoro ya matumizi ya ardhi ambayo amesema kuwa inatokana na  kutokuwajibika kwa baadhi ya viongozi.

Kufuatia kamati ilyoundwa na Rais wa awamu ya tano Hayati John Magufuli mwaka 2019 vijiji 20 mkoani Mara ambavyo vilikuwa na migogoro kati yao na hifadhii, wakala wa misitu na mamlaka zingine maamuzi yametolewa ambapo kutakuwepo na masuala kadhaa ikiwepo urekebishwaji wa mipaka na umegaji wa maeneo ya hifadhi.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi,  Nyumba na Maendeleo ya Makazi,  Dk Allan Kijazi alisema kuwa mpango wa utekelezaji wa maazimio hayo utasimamiwa na wakuu wa mikoa kwa kushirikiana na kamati za ulinzi na usalama za mikoa na wilaya katika eneo husika.

"Hapa leo tunaweka mipango lakini utekelezaji wake upo chini ya wakuu wa mikoa na kamati zao za ulinzi na usalama pamoja na wakuu wa wilaya sisi Wizara tutafanya ufuatiliaji na tathmini " amesema Dk Kijazi

Ametaka ushirikishwaji kwa viongozi wa kisekta wakati wa utekelezaji mpango wa maazimio ya Baraza la Mawaziri katika vijiji husika ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza tena.

No comments :

Post a Comment