
Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limepoteza wastani wa Sh1.2 trilioni ndani ya kipindi cha miaka minne iliyopita, sawa na Sh300 bilioni kwa
mwaka, kutokana na uchakavu wa miundombinu inayosababisha umeme kuvuja njiani kabla ya kufika kwa mteja, Mwananchi imebaini.Hasara hiyo ya kuvuja umeme wakati wa usafirishaji na usambazaji, inakaribia bajeti ya Sh1.219 trilioni ya mwaka kwa mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (JNHPP)-MW 2,115 iliyokuwa imetolewa hadi kufikia Aprili 2020.
Pia, fedha hiyo ni sawa na zaidi ya asilimia 90 ya mkopo wa Sh1.3 trilioni kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa kwa ajili ya Uviko-19.
Takwimu za Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) zinaonyesha umeme uliopotea katika vipindi vinne tofauti vya mahitaji ya juu ya umeme ilikuwa ni asilimia 17.72 ya megawati 1,045.7 mwaka 2017/18, asilimia 16.22 ya megawati 1,116.58 mwaka 2018/19 na asilimia 15.3 ya megawati 1,151.66 mwaka 2019/20.
Pia, asilimia 16.24 ya megawati 1,201.02 zilipotea mwaka 2020/21.
Takwimu hizo zinafanyika ikiwa ni wiki moja imepita baada ya Waziri wa Nishati, Januari Makamba kuondoa matumaini ya uhakika wa nishati ya umeme nchini, akiomba kupewa muda katika kipindi hiki hadi utakapokamilika ukarabati wa miundombinu ya kusafirisha nishati hiyo.
Kwa msingi wa takwimu hizo, kuna makadirio ya upotevu wa Sh1.206 trilioni kati ya mwaka 2017/21, sawa na wastani wa Sh299 bilioni kila mwaka katika upotevu wa asilimia 16.37 ya megawati 1,129.
Mwaka 2020/21 umeme unaopotea uliongezeka kutoka asilimia 15.3 ya 2019/20 hadi asilimia 16.24.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Godfrey Chibulunje alisema mamlaka hiyo inafikiria kuanzisha mwongozo maalumu ili kudhibiti umeme unaopotea, ikiwa ni siku chache baada ya kuzindua miongozo mitatu, ukiwamo wa kudhibiti upotevu wa maji kabla ya kufika kwa mteja.
Chibulunje alisema kwa sasa mamlaka hiyo imekuwa ikitoa masharti ya kupunguza kiwango cha umeme unaovuja kwa Tanesco na kampuni nyingine za huduma hiyo kila inapowasilisha maombi ya kurekebisha bei za umeme ili kuimarisha huduma zake kwa wananchi.
“Kila baada ya miaka mitatu huwa wanakuja kuomba tariffs (tozo) ndio tunawapa targets kupunguza losses (umeme unaopotea) kwa kiwango fulani, mipango ya kupunguza kiwango cha umeme unaopotea inakuwa juu yake, tofauti na sekta ya maji tuliowapatia mwongozo mwaka huu,” alisema Chibulunje.
Ripoti ya Utendaji wa Udhibiti wa Sekta Ndogo ya Umeme katika mwaka wa fedha ulioishia Machi 2021, inaonyesha asilimia 64 ya mapato ya Tanesco hupatikana mikoa saba, huku asilimia 36 ikipatikana mikoa 22.
Mkoa unaoongoza kwa mapato ni Kinondoni Kusini asilimia 18, ikifuatiwa na Ilala asilimia 13.
Umeme huo unapotea katika mazingira ya shirika kutegemea asilimia 50 ya mapato kupitia matumizi ya kawaida, hasa wateja wa nyumbani, biashara ndogondogo na viwanda vidogo na asilimia 32 kupitia wateja wakubwa kama inavyoelezwa katika ripoti kama hiyo iliyotoka mwaka 2020.
Tatizo la msingi
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mtandao wa njia za usafirishaji umeme unahusisha 670km msongo wa 400kV; 3,011km msongo wa 220kV; 1,673km msongo wa 132kV na 543km msongo wa 66kV.
Mtandao wa usambazaji unahusisha 139,092.86km chini ya Tanesco na 421km za Mwenga Power Services Limited.
Hata hivyo, Waziri Makamba alisema kwa viwango vya kimataifa, laini ya 32KV inayosambaza umeme mitaani umbali wa kilomita 100, Tanesco imekuwa ikitumia kusafirisha umbali wa kilomita 1,600, huku laini ya 11KV inayotakiwa kusambaza umeme umbali kilomita 30 ikipeleka umeme hadi kilomita 206.
Mikakati ya udhibiti
Ripoti kama hiyo kwa mwaka jana inaonyesha juhudi zilizochukuliwa na Serikali ili kudhibiti changamoto hiyo ni pamoja na ukarabati wa mitambo ya kuzalisha umeme, ikiwamo Hale na Nyumba ya Mungu.
Pia, kutekeleza ujenzi na ukarabati wa vituo vidogo vya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Arusha na Dodoma, Iringa, Singida, Shinyanga na Geita pamoja na matumizi ya mita za kisasa.
Ripoti hiyo inaonyesha malengo ya shirika hilo kupitia Mkakati wa Mageuzi ya Sekta ya Usambazaji wa Umeme na Mpango ujao (ESI-RSR) wa 2014, ni kupunguza kiwango cha upotevu wa umeme kutoka wastani wa asilimia 18 iliyorekodiwa Julai 2015 hadi kufikia wastani wa asilimia 12 ifikapo 2025.
Hata hivyo, changamoto za upotevu wa nishati hiyo zimekuwa zikihusishwa na shirika kuelemewa na majukumu matatu ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa huduma, hatua iliyoibua hoja za kulipunguzia mzigo huo na kuwekeza kampuni nyingine kama ilivyopendekezwa kwa muda mrefu.
Kutokana na mitazamo hiyo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema tayari Tanesco imeshaanza utafiti ili kubaini mfumo sahihi utakaosaidia uendeshaji wa shirika hilo, huku akitoa tahadhari ya changamoto za kuligawanya shirika kwa wawekezaji wanaoweza kuathiri huduma hizo kwa makusudi.
“Tumewapa kazi Tanesco ya kufanya utafiti, wanaweza kuja kwenye hatua hiyo iliyopendekezwa, nani tunampa jukumu la kuzalisha, nani asafirishe na nani asambaze, zinaweza kuwa taasisi za Serikali, lakini lengo lake ni moja, tukifikia hapo kupitia utafiti huo, tutaweza kufikia hatua nzuri,” alisema Majaliwa.
Umeme kiuchumi
Wachumi na wafanyabiashara nchini wamesema sekta ya nishati ni muhimili na msingi wa maendeleo ya Taifa.
Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Stephen Chamle alisema wafanyabiashara wengi wamekuwa wakikatishwa tamaa na gharama za umeme wakati wa uwekezaji, hatua inayoendelea kudumaza juhudi za kuongeza uzalishaji wa bidhaa za ndani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa, Dk Donald Mmari alisema upotevu wa nishati ya umeme unapunguza ukuaji wa mapato ya shirika na kuchochea ongezeko la gharama za uendeshaji wa shirika.
“Kama hasara hiyo haitadhibitiwa, maana yake itafanya shirika kuwa na mahitaji ya kuongeza tozo au bajeti kwa ajili ya utoaji wa huduma, sasa ukiongeza tariffs (tozo), maana yake gharama kwa mteja zitaongezeka, kwa hiyo Serikali inatakiwa kuwekeza juhudi za kuondoa upotevu huo,” alisema Dk Mmari.
Changamoto za ufanisi zimeendelea kugharimu Serikali baada ya Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2020/21 kuonyesha changamoto za kukatika umeme kumesababisha mkandarasi wa mradi wa JNHPP kudai fidia ya Sh19.51 bilioni kati ya Januari 2020 hadi Oktoba 2021.

No comments :
Post a Comment