Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa akiwaarifu Watanzania mafanikio ya Sekta ya Ujenzi na Uchukuzi nchini katika Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania kupitia mkutano na waandishi wa habari leo Novemba 12, 2021 jijini Dodoma.
====== ======= ======== ========
TAARIFA YA WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI MHE. PROF. MAKAME MNYAA MBARAWA (MB), WAKATI WA MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI TAREHE 12/11/2021 KUELEKEA MAADHIMISHO YA MIAKA 60 YA UHURU WA TANZANIA BARA.
Ndugu Wanahabari,
Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, ambaye kwa rehema zake nyingi ametujalia afya njema na kutuwezesha kukutana hapa leo hii. Aidha, nipende kuchukua fursa hii tena kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa rehema zake na kwa kuijalia nchi yetu tunu za amani, mshikamano, umoja katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru waTanzania Bara.
Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ni moja ya Wizara muhimu katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye jukumu la kusimamia masuala ya miundombinu na huduma za usafiri na usafirishaji ambazo ni kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
Katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara (1961 - 2021) tumepata mafanikio makubwa katika Sekta za Ujenzi na Uchukuzi. Aidha, kumekuwa na mabadiliko mbalimbali ya kisera yaliyoendana na utungwaji wa sheria kadhaa zilizowezesha sekta hizi mbili kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Ndugu Wanahabari,
Nikianza na Sekta ya Ujenzi, Nikianza na Sekta ya Ujenzi, Sekta hii ambayo inasimamia ujenzi, matengenezo na ukarabati wa barabara, madaraja, vivuko, viwanja vya ndege, nyumba na majengo ya Serikali imekwenda sambamba na ongezeko la Bajeti kutoka Shilingi bilioni 2.1 mwaka 1962/63 hadi kufikia zaidi ya Shilingi trilioni 1.5 mwaka 2021/22.
Sekta hii kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), inasimamia mtandao wa barabara zenye urefu wa takribani kilometa 36,361.88 ambapo kilometa 12,215.51 ni barabara kuu na kilometa 24,146.37 ni barabara za mikoa. Aidha, kati ya barabara hizo, barabara kuu za lami ni kilometa 9,058.2, na za mikoa ni kilometa 2,128.22.
Mtandao wa Barabara nchini umekuwa ukiboreshwa na kuongezeka kwa kuweka mkazo katika ujenzi na ukarabati wa Barabara Kuu, Barabara za Mikoa, Barabara za Wilaya na madaraja kwa lengo la kuleta uhakika na nafuu ya usafiri na usafirishaji nchini. Aidha, kipaumbele kimetolewa katika kutunza, kutengeneza na kukarabati Barabara kupitia mipango na miradi mbalimbali iliyoandaliwa na Wizara ambapo mpaka sasa wastani wa asilimia 88 ya barabara kuu na za mikoa zipo katika hali nzuri.
Ndugu Wanahabari,
Mafanikio yaliyojitokeza katika mtandao wa barabara tangu kupata uhuru mwaka 1961 ni kuongezeka kwa mtandao wa barabara za lami kutoka kilometa 1,360 (1961) hadi kufikia kilometa 11,186 (Septemba 2021) na hivyo kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji katika maeneo mbalimbali nchini.
Mfano ni kwa wakazi wa kanda ya ziwa ambao walikuwa wanatumia zaidi ya saa 30 kusafiri kwa kutumia usafiri wa mabasi kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na wakati mwingine kulazimika kupitia nchi jirani kama vile Kenya (Nairobi), ambapo kwa sasa wasafiri wanatumia chini ya saa 15 kwa safari hiyo.
Katika kipindi hiki, Serikali inaendelea na ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara zenye urefu wa kilometa 1,593 ambazo zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Baadhi ya miradi inayotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa barabara za Mzunguko wa Nje Dodoma (Dodoma Outer Ring Road) kilometa 112.3, Tabora – Koga – Mpanda kilometa 365.98 na Kabingo – Kibondo Town – Kasulu – Manyovu kilometa 286.5; Pangani – Tanga (km 50) pamoja na Barabara ya zege ya Lusitu – Mawengi (km 50) .
Ndugu Wanahabari,
Mnamo mwaka 2001 Serikali iliamua kuanzisha miradi maalum ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami na madaraja kwa kutumia fedha zake yenyewe hali ambayo iliongeza kasi ya ujenzi wa barabara za lami na madaraja nchini. Mathalani baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na sehemu ya barabara ya kuunganisha Dar es Salaam na Mikoa ya kusini ya jumla ya kilometa 223 inayohusisha sehemu ya Somanga – Matandu (km 33), Nangurukuru – Mbwemkuru (km 95) na Mbwemkuru – Mingoyo (km 95); sehemu ya barabara ya kuunganisha Dar es Salaam, Mikoa ya Kati na Kanda ya Ziwa ya jumla ya kilometa 455 inayohusisha sehemu ya Geita – Buzirayombo – Kyamyorwa (km 120), Geita – Usagara (km 90), Dodoma – Manyoni (km 127), na Manyoni – Singida (km 118) na katika Mkoa wa Tanga, barabara ya Korogwe – Handeni – Mkata (km 119) ilijengwa.
Aidha, barabara zingine zilizojengwa na kukamilika ni Nzega – Tabora – Urambo – Kaliua – Kazilambwa (km 294.8); Isaka – Ushirombo – Lusahunga (km 242) pamoja na Uyovu – Bwanga – Biharamulo (km 112); Mwigumbi – Maswa – Bariadi – Lamadi (km 171.80); Sumbawanga – Kanazi – Kizi – Kibaoni (km 151.60) pamoja na Sumbawanga – Matai – Kasanga Port (km 112); Mbeya – Lwanjilo – Chunya – Makongolosi (km 111); Tabora – Nyahua – Chaya – Manyoni sehemu za Tabora – Nyahua (km 85) na Manyoni hadi Chaya (km 89.4). Vilevile, ujenzi umekamilika kwa Barabara ya Korogwe – Same – Mkumbara (km 172).
Kwa upande wa madaraja yaliyokamilika kujengwa kwa kutumia fedha za ndani ni pamoja na Daraja la Nyerere – Dar es Salaam (mita 680); Magufuli katika mto Kilombero - Morogoro (mita 384), Lukuledi II - Lindi (mita 30), Momba - Songwe (mita 84), Mara – Mara (mita 94), Sibiti - Singida (mita 82), Magara – Manyara (mita 84) na Daraja la Ruhuhu (linaunganisha Mikoa ya Ruvuma na Njombe (mita 98.7).
Ndugu Wanahabari,
Ukuaji wa miji na kuongezeka kwa idadi ya watu kumesababisha kuwepo kwa msongamano wa magari katika barabara hususan katika miji na majiji makubwa. Serikali katika kutatua changamoto hiyo imeanza utekelezaji wa miradi ya kupunguza msongamano katika majiji ya Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma, Mbeya, Arusha na Tanga pamoja na miji ya Iringa na Babati ambapo jumla ya kilometa 102.4 za barabara zilipangwa kujengwa kwa kiwango cha lami. Barabara hizo zimekamilika na nyingine mpya zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Miradi ya Barabara na Madaraja yenye lengo la kupunguza msongamano kwenye majiji ambayo imekamilika ni pamoja na ujenzi wa barabara ya Usagara - Kisesa (km 17), upanuzi wa barabara ya Mwaloni Furahisha – Pasiansi – Uwanja wa Ndege mkoani Mwanza (km 5.32), upanuzi wa Barabara ya Sakina – Tengeru (km 14.1) na ujenzi wa barabara ya mchepuo ya Arusha (Arusha Bypass), mkoani Arusha (km 42.4). Vilevile, ujenzi wa Daraja la Juu la Mfugale (Mfugale Flyover), kwenye Makutano ya TAZARA na Daraja la Juu la Kijazi (Kijazi Interchange), kwenye makutano ya Ubungo mkoani Dar es Salaam.
Miradi mingine iliyokamilika ni upanuzi wa barabara ya Kimara – Kibaha (km 19.2), kuwa njia nane, Upanuzi wa Barabara ya Morocco – Mwenge (km 4.3) na Miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) Awamu ya I. Aidha, Kwa sasa ujenzi wa Awamu ya II ya BRT pamoja na Daraja la Gerezani unaendelea.
Pia, katika Jiji la Mbeya Serikali inaendelea na juhudi mbalimbali za kupunguza msongamano ambapo tayari Upembuzi yakinifu na Usanifu wa Kina wa barabara ya Igawa – Uyole – Songwe – Tunduma (km 217) na barabara ya mchepuo katika Jiji la Mbeya (Uyole – Songwe Bypass) yenye urefu wa kilometa 49 umekamilika. Kwa upande wa Jiji la Dodoma tayari ujenzi wa barabara za mzunguko wa Nje (Dodoma Outer Ring Roads) zenye urefu wa kilometa 112.3 unaendelea.
Ndugu Wanahabari,
Sera ya Serikali ni kuunganisha Makao Makuu ya mikoa yote nchini, ambapo hadi sasa mikoa yote imeungwa kwa barabara za lami isipokuwa mikoa michache ambayo hata hivyo Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya barabara ya kuunganisha mikoa hiyo. Miradi inayoendelea kutekelezwa kwa sasa ni pamoja na:
v Ujenzi kwa kiwango cha lami sehemu ya Tabora – Usesula – Komanga – Kasinde – Mpanda (km 365.98) inayounganisha mikoa ya Katavi na Tabora.
v Ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Njombe – Ndulamo – Makete (km 107.4), inayounganisha mikoa ya Njombe na Mbeya.
v Ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Makutano – Natta (sehemu ya Makutano – Sanzate (km 50) na sehemu ya Wasso (Loliondo) – Sale Jct (km 49) kwa ajili ya kuunganisha mikoa ya Mara na Arusha.
v Serikali ina mpango wa kuanza ujenzi wa sehemu ya Mkiwa – Itigi – Noranga (km 56.9), kwa ajili ya kuunganisha mikoa ya Singida – Mbeya.
v Ujenzi wa barabara sehemu ya Vikonge – Ruhafe (km 25) ipo katika hatua ya mwisho ya kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami, Barabara hiyo inaunganisha mikoa ya Katavi na Kigoma.
v Ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Kibaoni – Sitalike (km 71.0), sehemu ya Kibaoni – Mlele inayounganisha mikoa ya Katavi na Rukwa.
Ndugu Wanahabari,
Pamoja na kuunganisha makao makuu ya Mikoa, Serikali pia imeunganisha nchi yetu na nchi jirani za Msumbiji, Kenya, Uganda, Rwanda na Zambia kupitia mtandao wa barabara.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Barabara za Mpemba – Isongole (km 50.3) (Tanzania/Malawi), Kabingo – Kasulu – Manyovu (km 260) (Tanzania/Burundi), na Bagamoyo – Tanga – Horohoro/Lungalunga (km 240) (Tanzania/Kenya).
Vilevile, miradi ya barabara ambayo inaunganisha nchi yetu na nchi jirani ambayo usanifu umekamilika ni pamoja na Omugakorongo – Kigarama – Murongo (km 105) (Tanzania/Uganda). Aidha, barabara ya Bugene – Kasulo/Benako (km 124) sehemu ya Bugene – Chato/Buligi (km 60) ipo katika hatua za kumpata Mkandarasi kwa ajili ya kuunganisha Tanzania na Burundi.
Ndugu Wanahabari,
Katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru, Serikali pia imejenga madaraja makubwa na madogo nchini. Madaraja makubwa yaliyokamilika ni pamoja na Daraja la Kirumi (Mara), Daraja la Mto Kagera (Kagera), Daraja la Rusumo (Kagera), Daraja la Mkapa (Pwani), Daraja la Umoja (Mtwara), Daraja la Kikwete (Kigoma), Daraja la Sibiti (Singida), Daraja la Mara (Mara), Daraja la Mlalakuwa (Dar es Salaam), Daraja la Momba (Rukwa), Lukuledi II (Lindi), Ruhuhu (Ruvuma/Njombe), Magufuli (Morogoro), Magara (Manyara), Nyerere (Dar es Salaam), Kavuu (Katavi), Ruvu Chini (Pwani) na mengine mengi.
Madaraja makubwa yanayoendelea kujengwa ni pamoja na Daraja la Tanzanite (Dar es Salaam), Msingi (Singida), Daraja Jipya la Wami (Pwani), Kitengule (Kagera), Gerezani (Dar es Salaam) na Kigongo – Busisi (Mwanza). Aidha, madaraja mengine 7 yapo kwenye hatua ya usanifu ya ujenzi. Madaraja hayo ni Sukuma (Mwanza), Simiyu (Mwanza), Mkenda (Ruvuma), Mtera (Dodoma/Iringa), Godegode (Dodoma), Malagarasi Chini (Kigoma) na Ugalla (Tabora) yako kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji.
Ndugu Wanahabari,
Kumekuwa na mafanikio makubwa katika kuongeza idadi ya wataalamu katika taaluma ya kihandisi nchini ambapo usajili wao umekuwa ukiongezeka mwaka hadi ya mwaka. Kwa mfano, mwaka 1961 wakati nchi yetu inapata uhuru wahandisi wazawa walikuwa wawili (2), tu ambapo kwa sasa wahandisi waliosajiliwa wamefikia 32,145.
Aidha, Bodi ya Usajili wa Wahandisi inaendelea kusimamia utekelezaji wa mafunzo ya kujiendeleza kitaaluma kwa Wahandisi Wataalam na Wahandisi Washauri unaojulikana kama Continuing Professional Development (CPD) pamoja na kusimamia utekelezaji wa mpango wa mafunzo kwa vitendo kwa Wahandisi Wahitimu (Structured Engineers Apprenticeship Programme - SEAP) 3,000 ambao wapo katika miradi yote mikubwa inayoendelea kutekelezwa hapa nchini.
Ndugu Wanahabari,
Serikali inaendelea kuwajengea uwezo na kusajili makandarasi wazawa kupitia Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), ambapo hadi sasa makandarasi 12,382 wamesajiliwa kati ya hao makandarasi wazawa ni 11,916 na wa nje ni 466.
Serikali imekuwa ikitenga miradi mbalimbali ili kuwajengea uwezo makandarasi wazawa. Miradi hiyo ni pamoja na: -
v Ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Kaliua – Urambo (km 28), iliyojengwa kwa ubia na Makandarasi M/s Salum Motor Transport Co. Ltd, M/s Annam Road Works Co Ltd na M/s Jossam Company Ltd;
v Ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Rudewa – Kilosa (km 24), unaotekelezwa na kampuni ya Umoja Kilosa JV ambayo ni ubia wa Makandarasi M/s Kings Builders Ltd, M/s Comfix & Engineering Ltd, Emirate Builders Co. Ltd, Halem Construction Company Ltd, Audacia Investment Ltd na Pioneer Builders Ltd;
v Miradi mingine ni ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Bulamba – Kisorya (km 51), na ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Nyakanazi – Kibondo (km 50), unaotekelezwa na Kampuni ya M/s Nyanza Road Works.
v Upanuzi wa barabara ya Kimara – Kibaha (km 19.2), kutoka njia mbili hadi nane pamoja na ujenzi wa madaraja ya Kibamba, Kiluvya na Mpiji unaotekelezwa na Kampuni ya M/s Estim Company Ltd na
v Ujenzi wa Kiwanja Kipya cha Ndege cha Geita unaotekelezwa na Kampuni ya M/s Mayanga Contractors Company Ltd.
Ndugu Wanahabari,
Serikali kupitia Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) imeendelea kuimarisha Mfuko wa Kusaidia Makandarasi wa ndani (Contractors Assistance Fund - CAF), ili kuwawezesha kupata dhamana katika mabenki bila rehani ya kitu chochote.
Mpango huu unatoa dhamana kwa ajili ya zabuni (Bid Security) na malipo ya awali (Advance Payment Guarantees) kwa Makandarasi wadogo na wa kati (Madaraja ya 4 – 7 kawaida na 2-3 maalum). Aidha, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi 2020 Makandarasi 1,168 wamenufaika na huduma za mfuko huo.
Ndugu Wanahabari,
Kwa upande wa Vivuko, wakati Tanzania Bara inapata Uhuru wake mwaka 1961 hapakuwepo na vivuko vya kisasa isipokuwa vivuko 5 vya kuvutwa kwa Kamba. Kwa kuzingatia umuhimu wa vivuko kama kiungo muhimu kwenye usafirishaji, Serikali iliendelea kununua na kujenga vivuko vya kutumia Engine vinavyofikia 33 katika maeneo 22 hapa nchini na Boti 10 zinazotoa huduma katika maeneo mbalimbali wakati wa dharura.
Vivuko vinavyotoa huduma kwa sasa ni:-
ü Dar es Salaam - MV Magogoni, Kigamboni na MV Kazi
ü Mwanza - MV Mwanza, MV Sabasaba, MV Sengerema, MV Misungwi, MV Ukara, MV Ukara II, MV Temesa, MV Ilemela, MV Kome II na MV Tegemeo
ü Geita - MV Chato na MV Chato II
ü Tanga - MV Pangani, MV Pangani II na MV Bweni
ü Kigoma - MV Ilagala na MV Malagarasi
ü Kagera - MV Kyanyabasa na MV Ruvuvu
ü Mtwara - MV Kilambo, MV Tangazo, MV Mafanikio na MV Kuchele
ü Pwani - MV Mkongo na MV Kilindoni
ü Mara - MV Musoma na MV Mara
ü Lindi - MV Kitunda (Lindi) na MV Lindi.
ü Ruvuma - MV Ruhuhu
Ndugu Wanahabari,
Kwa upande wa Nyumba na Majengo ya Serikali, Katika kipindi cha miaka 60, Serikali imejenga na kukarabati majengo ya Ofisi kwa ajili ya matumizi ya baadhi ya Wizara, Makao Makuu ya Mikoa na Wilaya, Nyumba za Majaji, Viongozi na watumishi wa Serikali katika maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara.
Aidha, Serikali imefanya ukarabati mkubwa wa Ikulu ya Dar es Salaam na Dodoma pamoja na Jengo la Mahakama ya Biashara Kivukoni (Dar es Salaam).
Ndugu Wanahabari,
Serikali pia inaendelea kuimarisha usafiri wa anga ambapo Viwanja vya Ndege vyenye lengo la kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji vimeendelea kujengwa na kukarabatiwa katika mikoa mbalimbali nchini. Hadi sasa Serikali ina jumla ya Viwanja vya Ndege 58 vilivyo chini ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na kimoja (01) kilicho chini ya KADCO.
Miradi iliyotekelezwa/inayoendelea kutekelezwa ni pamoja na
· Jengo la tatu la kisasa la abiria (TB – III) katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere limejengwa;
· Uboreshaji wa Viwanja vya Ndege vya Mwanza (Phase I), Tabora (Phase II), Kigoma (Phase I), Bukoba (Phase I), Dodoma, Mpanda na Mafia ambavyo vimekalimika kwa kiwango cha lami;
· Ukarabati wa Viwanja vya Ndege vya Mtwara, Iringa, Songwe, Geita, Songea na Musoma upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji;
· Mkataba wa Ujenzi wa Mradi mpya wa Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Msalato Awamu ya Kwanza (package 1) unaohusisha ujenzi wa miundombinu ya Kiwanja (Airport Infrastructure); ambao utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu (3). umesainiwa tarehe 13 Septemba, 2021 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 165,627,031,495.52. Kwa sasa Mkandarasi ameanza utekelezaji wa mkataba huo; na
· Maandalizi ya ukarabati na upanuzi wa viwanja vya ndege vya Moshi, Sumbawanga, Tabora (Awamu ya 3) Kigoma (Awamu ya pili), Shinyanga, Mwanza (Jengo jipya la abiria) na Arusha yanaendelea.
Serikali pia inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa viwanja vya ndege vya Lindi, Lake Manyara, Tanga na Simiyu.
Aidha, katika mpango wa miaka mitano ijayo kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022-2025/2026 Serikali imepanga kutekeleza ujenzi na ukarabati wa Viwanja vingine vya Ndege kadri ya upatikanaji wa fedha baada ya miradi inayoendelea kukamilika.
Ndugu Wanahabari,
Ili kuweza kuzilinda barabara zetu Serikali imefunga mizani 64 ya kupima uzito wa magari kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Jumuiya Afrika Mashariki ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018 katika maeneo mbalimbali ya kimkakati ya barabara kuu. Lengo la kufunga mizani hizo ni kuzuia uharibifu wa miundombinu ya barabara na madaraja unaotokana na uzidishaji uzito wa magari na hivyo kufanya miundombinu hiyo kudumu kwa kipindi kilichokusudiwa wakati wa usanifu wake.
Vilevile Serikali imefunga mizani ya kisasa yenye uwezo wa kupima gari likiwa kwenye mwendo (Weigh in Motion) katika mizani 13 hapa nchini ikiwa ni pamoja na Mizani za Nala – Dodoma, Njuki – Singida- Dakawa – Morogoro, Mikese (South) – Morogoro, Vigwaza – Pwani, Mpemba - Songwe na Wenda – Iringa kwa ajili ya kutatua changamoto ya foleni katika mizani. Katika mwaka huu wa fedha 2021/22, Wizara inatarajia kufunga mizani ya aina hiyo katika vituo vya Mikumi – Morogoro, Kimokouwa – Arusha na Rubana – Mara.
Aidha, Serikali inaendelea na uboreshaji wa mifumo ya usimamizi wa vituo vya mizani ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na kupunguza mianya ya rushwa katika vituo vya mizani kwa kufunga mfumo wa kamera za kisasa za CCTV ambapo hadi sasa jumla ya mizani 13 zimefungwa mfumo huo. Mfano wa mizani hizo ni Mpemba (Songwe), Mikumi (Morogoro), Vigwaza (Pwani), Himo (Kilimanjaro), Njuki (Singida), Mutukula (Kagera), Usagara (Mwanza), Mikese (Morogoro), Nala (Dodoma), Mingoyo (Lindi) na Makuyuni (Arusha). Katika mwaka huu wa fedha 2021/2022, Wizara inatarajia kufunga mfumo wa aina hiyo kwenye mizani 42.
Ndugu Wanahabari,
Mbali na mafanikio niliyoyaeleza, Sekta hii inakabiliwa na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yake. Changamoto hizo ni pamoja na:-
Uvamizi wa maeneo ya hifadhi ya barabara (Road Reserve) unaofanywa na wananchi kwa ajili ya shughuli za kijamii katika maeneo ya hifadhi ya barabara na hivyo kusababisha usumbufu na uchelewaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Wizara (Ujenzi), inaendelea na mpango wa kuelimisha umma kwa njia ya vyombo vya habari, vipeperushi, mikutano na semina ili waweze kufahamu vyema kuhusu Sheria ya Barabara Na. 13 ya mwaka 2007. Aidha, Wizara (Ujenzi), inashirikiana na wadau wengine kuhakikisha kuwa eneo la hifadhi ya barabara halichukuliwi kwa matumizi mengine.
Ndugu Wanahabari,
Changamoto nyingine ni uwezo mdogo wa mtaji kwa makandarasi wazawa hivyo kushindwa kushiriki katika fursa za miradi ya maendeleo kutokana na masharti ya upatikanaji wa dhamana za zabuni. Dhamana za ushiriki wa kazi, na mitaji ya kuwawezesha kufanya kazi kutoka mabenki kuwa ngumu na kutozingatia mahitaji halisi ya shughuli za kihandisi. Aidha, kushindwa kupata mitaji kunawafanya makandarasi kushindwa kukua na kupata fursa ambazo zitawawezesha kukua na kumudu miradi mikubwa.
Katika hili, Serikali inaendelea kuwashirikisha kikamilifu makandarasi wazawa katika miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara na madaraja kwa lengo la kuwajengea uwezo. Vilevile, Serikali kupitia Bodi ya Usajili ya Makandarasi (CRB), imeanzisha mfuko wa kusaidia makandarasi wazawa (wadogo na wa kati) ili kupewa dhamana za zabuni na malipo ya awali kwa makandarasi hao bila ya kuweka rehani kitu chochote.
Ndugu Wanahabari,
Changamoto nyingine ni Uzidishaji wa Uzito wa Magari unaofanya na Wasafirishaji na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara na madaraja.
Wizara (Ujenzi), inaendelea kusimamia utendaji kazi katika mizani za kudhibiti uzito wa magari barabarani. Jitihada nyingine ni ujenzi wa vituo vya pamoja vya ukaguzi (One Stop Inspection Stations – OSIS), ambavyo vinajengwa katika ukanda wa kati na Ukanda wa Dar es Salaam (TANZAM). Ujenzi wa vituo hivyo utasaidia kupunguza msongamano wa magari katika vituo vya mizani hasa magari yanayosaforosha mizigo nje ya nchi (Transit Vehicles).
Ndugu Wanahabari,
Sekta ya Uchukuzi: Miundombinu ya uchukuzi pamoja na huduma zake ni kichocheo kikubwa katika kukuza uchumi wa nchi yeyote. Tanzania hatupo nyuma katika kutekeleza sera ya uendelezaji wa miundombinu ya uchukuzi hususan miundombinu ya reli, bandari na viwanja vya ndege. Aidha, tumeendelea kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji kwa njia ya barabara, reli, maji, anga pamoja na huduma za hali ya hewa.
Tukianza na usafiri wa reli; usafiri wa reli ni nguzo muhimu ya kuwezesha na kuchochea ukuaji wa uchumi na biashara. Hii inatokana na ukweli kwamba usafiri wa reli ni wa gharama nafuu ikilinganishwa na usafiri wa Anga na Barabara hususan katika usafirishaji wa mizigo mikubwa kwa umbali mrefu kuanzia kilometa 400 na zaidi. Kutokana na umuhimu huo, mwaka 1961, wakati Tanzania Bara inapata uhuru ilikuwa na mtandao wa reli wenye urefu wa km 2,068 unaojumuisha reli ya Dar es Salaam –Tabora (km 840); Tabora – Kigoma (km 411); Tabora – Mwanza (km 379); na Tanga – Moshi – Arusha (km 438). Mtandao huo ni wa reli nyembamba yenye upana wa mita moja (Meter Gauge Railway - MGR) na kihistoria ulijengwa katika kipindi ambacho Tanganyika ilikuwa chini ya utawala wa Wajerumani na sehemu ya mtandao huo ilijengwa wakati Tanganyika ikiwa chini ya utawala wa Waingereza.
Baada ya Uhuru wa Tanzania Bara mwaka 1961, Serikali iliongeza mtandao wa reli ya kati kwa kujenga reli mpya ya jumla ya km 639 ili kufikia masoko mbalimbali ya ndani na nje ya nchi. Ongezeko hili la mtandao wa reli limewezesha reli ya Kati kuwa na mtandao wenye urefu wa jumla ya km 2,707. Reli zilizoongezeka ni pamoja na Ruvu Junction – Mruazi Junction (km 188); Kilosa – Kidatu branch line (km 108); Kaliua – Mpanda branch line (km 210); Manyoni – Singida branch line (km 115); na Kahe –Taveta (Mpakani na Kenya) branch line (km 18).
Ndugu Wanahabari,
Pamoja na uwepo wa mtandao wa reli ya Kati (Metre Gauge Railway - MGR), hivi sasa Serikali inaendelea na mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa yenye upana wa mita 1.435 (Standard Gauge Railway - SGR). Awamu ya kwanza ya mradi huo ni ya ujenzi wa Reli ya kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza (km. 1,219), ambayo imegawanyika katika vipande vitano (5). Kipande cha kwanza ni cha Dar es Salaam – Morogoro (km. 300); Kipande cha pili ni Morogoro – Makutopora (km. 422), kipande cha tatu ni Makutopora – Tabora (km. 376.5), kipande cha nne ni Tabora – Isaka (km. 162.5), na kipande cha tano ni Isaka – Mwanza (km. 341). Reli hii imesanifiwa kuwa na mwendokasi wa kilomita 160 kwa saa kwa treni ya abiria na kilomita 120 kwa saa kwa treni ya mizigo. Lengo la mradi huu ni kutoa huduma ya usafirishaji wa abiria na mizigo ya ndani na nje ya nchi kwa wingi na kwa muda mfupi ili kukuza uchumi wa nchi kwa kuziunganisha bandari zetu na nchi jirani ambazo hazipakani na bahari (land locked countries).
Ujenzi wa vipande vya Dar es Salaam – Morogoro (km 300), Morogoro – Makutopora (km 422) na Mwanza – Isaka (km 422), unaendelea. Hadi Septemba, 2021, Ujenzi wa reli kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro umekamilika kwa asilimia 93.73 na kazi ya majaribio ya uendeshaji wa treni inatarajia kuanza mwishoni mwa Disemba, 2021, Ujenzi wa reli kipande cha Morogoro hadi Makutupora (km 422), umekamilika kwa asilimia 72.43 na kwa mujibu wa mkataba kazi ya ujenzi kwa kipande hicho inatarajiwa kukamilika Februari, 2022, na ujenzi wa reli kipande cha Mwanza – Isaka umekamilika kwa asilimia 3.33 na kwa mujibu wa mkataba kazi ya ujenzi huo inatarajiwa kukamilika Aprili, 2024.
Ndugu Wanahabari,
Treni ya awamu ya kwanza inayoanzia Dar es Salaam hadi Morogoro itaanza kutoa huduma rasmi baada ya ujenzi wa reli na majaribio ya matumizi yake kukamilika. Ili kuwezesha kutoa huduma za usafiri huo, Mkataba wa ununuzi wa Vichwa viwili (2) vya Treni za umeme pamoja na Mabehewa 30 umesainiwa na vifaa hivyo vitawasili nchini Novemba, 2021 na majaribio ya kwanza ya Reli ya SGR yamepangwa kufanyika Disemba, 2021. Mkataba kwa ajili ya ununuzi wa vichwa vya treni za umeme 17, seti 10 za treni za umeme za abiria (EMU) umesainiwa tarehe 14 Julai, 2021 na vinatarajiwa kuwasili baada ya miezi 34, na Mkataba kwa ajili ya ununuzi wa mabehewa 59 ya abiria ulisainiwa tarehe 23 Septemba, 2020. Malipo ya awali yameshafanyika na hadi Juni, 2021 kazi ya matengenezo imefikia asilimia 45. Mkataba huu ni wa miaka miwili utakamilika tarehe 22 Septemba, 2022. Taratibu za ununuzi wa mabehewa 1,430 ya mizigo zinaendelea.
Ndugu Wanahabari,
Serikali kupitia TRC ipo kwenye maandalizi ya kuanza Ujenzi wa reli ya SGR awamu ya pili kwa kipande cha Tabora - Kigoma (Km 411); Kaliua-Mpanda-Karema (Km 321), Keza - Ruvubu (km 36); Isaka - Rusumo (km 371), na Uvinza-Musongati (Km 240). Upembuzi yakinifu na Usanifu wa awali wa vipande hivi umekamilika na hatua inayoendelea ni kuandaa makabrasha ya zabuni.
Ndugu Wanahabari,
Serikali inatambua umuhimu wa usafiri wa anga katika kuchangia ukuaji wa sekta nyingine hususan utalii wa aina zote; kilimo cha mboga mboga, matunda, nyama na samaki na kuinua uchumi wa nchi na ustawi wa wananchi. Tanzania ina Kampuni ya Ndege inayojulikana kama Kampuni ya Ndege Tanzania (Air Tanzania Company Limited - ATCL). Uwepo wa Kampuni hii nchini ambayo pia ndiyo inatumika kuitangaza Tanzania (Flag Ship Company), umeendelea kuimarishwa ili kuifanya Tanzania kuwa kiungo (Hub) cha usafiri wa anga katika Afrika Mashariki na Kati.
Ndugu Wanahabari,
Baada ya Tanzania kupata uhuru, kulikuwa na Shirika moja la ndege katika Jumuiya ya Afrika Mashariki hadi Machi 10, 1977 lilipoanzishwa Shirika la Ndege Tanzania (ATC), baada ya kuvunjika kwa lililokuwa Shirika la Ndege la Afrika Mashariki. Shirika la Ndege Tanzania lilianza kutoa huduma za usafiri wa anga kwa kutumia ndege tatu, moja aina ya DC-9 na mbili aina ya Foker Friendships F27.
Baadaye Serikali ilinunua ndege nyingine aina ya Boeing B737-200 Combi (mbili), Foker Friendships (mbili), na Twin Otters (nne). Kutokana na kudorora kwa uendeshaji wa Shirika hilo ikiwa ni pamoja na kuiingizia Serikali hasara, mwaka 2002, Shirika hilo lilibinafsishwa na kuundwa Kampuni ya Ndege Tanzania (Air Tanzania Company Ltd (ATCL). Hadi kufikia mwaka 2002, ATC ilikuwa na ndege moja aina ya B737-200 na nyingine ya kukodi ya B737-300.
Ndugu Wanahabari,
Nia ya Serikali kubinafsisha Shirika la Ndege ilikuwa ni kulifanya shirika hilo kuwa imara na kutoa huduma bora za ndani na nje ya nchi. Hata hivyo, baada ubinafsishaji na uundwaji mpya wa Kampuni ya Ndege Tanzania bado kampuni hiyo ilishindwa kukua na kujiendesha kwa hasara. Hali hii ilileta mzigo wa madeni kwa ATCL na Serikali iliamua kuvunja ubia kati ATCL na Shirika la Ndege la Afrika Kusini (South Africa Airways – SAA) mwaka 2006, kwa kununua hisa asilimia 49 zilizokuwa zinamilikiwa na SAA. Wakati ubia huu unavunjika, ATCL ilikuwa na ndege moja tu aina Dash Q 300.
Ndugu Wanahabari,
Kutokana na umuhimu wa Kampuni ya Ndege, mwaka 2016, Serikali iliamua kufufua ATCL kwa kununua ndege mpya na kuboresha menejimenti na muundo wa Kampuni hiyo. Hadi kipindi hiki tunachoadhimisha miaka 60 tangu kupata uhuru, ATCL ina jumla ya ndege 12 za kisasa zinazotoa huduma ndani na nje ya nchi.
Ndege hizo ni aina ya Bombardier Dash 8 Q 400 tano (5), Air bus A220-300 nne (4), Boeing 787-8 Dreamliner mbili (2), na Dash 8 Q300 moja (1). Aidha, Agosti, 2021, Serikali imesaini na kulipa malipo ya awali ya ununuzi wa wa ndege mpya tano (5) aina ya Boeing 787-8 moja (1) Boeing 737-9 Max mbili (2), Ndege ya Mizigo (Freighter) Boeing 767-300 moja (1), na Bomabrdier Dash 8 Q400 moja (1). Kuwasili kwa ndege hizo kutaifanya ATCL kuwa na ndege 17 hadi kufika mwaka 2023, ambazo zitaimairisha mtandao wake wa safari za ndege kwa soko la ndani, kikanda na kimataifa
Ndugu Wanahabari,
Licha ya kuwepo kwa janga la UVIKO – 19, ATCL imeendelea kutoa huduma ya usafiri wa anga ndani ya nchi katika vituo kumi na tatu (13), ambavyo ni Arusha, Bukoba, Dar es Salaam, Dodoma, Geita, Kigoma, Kilimanjaro, Mbeya, Mpanda, Mwanza, Songea, Tabora na Zanzibar. Kwa vituo vya kikanda, ATCL imeendelea kutoa huduma katika vituo vitano (5) vya Entebbe, Uganda; Hahaya, Comoro, Harare, Zimbabwe, Lusaka, Zambia, na Mumbai, India.
Aidha, ATCL ilisimamisha kwa muda utoaji wa huduma ya usafiri wa abiria katika kituo cha Bujumbura, Burundi na Guangzhou, China kutokana na athari za mlipuko wa UVIKO -19 na pia katika kituo cha Johannesburg, Afrika ya Kusini kutokana na masuala ya kisheria. Hata hivyo, Huduma za usafirishaji wa mizigo kwa kituo cha Guangzhou, China zinaendelea kutolewa hadi sasa.
Ndugu Wanahabari,
Baada ya Tanzania Bara kupata uhuru wake mwaka 1961, huduma za usalama wa usafiri wa anga zilikuwa chini ya Kurugenzi ya Usafiri wa Anga ya Afrika Mashariki yenye makao makuu nchini Kenya ambapo nchi za Tanzania, Kenya na Uganda zilikuwa na Ofisi ndogo. Majukumu ya Kurugenzi hii yalikuwa kutoa huduma za uongozaji ndege, huduma za mawasiliano, utoaji leseni, usajili wa ndege, utafutaji na uokoaji wa ndege zinazopotea na kupata ajali, utoaji leseni kwa mashirikia ya ndege, uchunguzi wa ajali za ndege na utoaji wa taarifa za anga. Baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977, Tanzania ilianzisha Kurugenzi ya Usafiri wa Anga Tanzania ambayo ilipewa majukumu yote ambayo Kurugenzi ya Usafiri wa Anga Afrika Mashariki ilikuwa ikiyafanya na kuwekwa chini ya Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi.
Ndugu Wanahabari,
Kutokana na mageuzi ya ki-mfumo na ki-uendeshaji, Kurugenzi hiyo ilibadilika na kuwa Wakala wa Serikali mwaka 1997 na hatimaye Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), mwaka 2003. Lengo la mabadiliko hayo likiwa ni kuipa madaraka ya kufanya maamuzi ya shughuli za udhibiti na ki-uchumi kwa haraka na ufanisi. Katika kuhakikisha kwamba usalama katika anga la Tanzania unakuwa mkubwa na wa kutosha, mwaka 1998 Serikali ilinunua Rada ya kuongozea ndege za kiraia ambayo ilifungwa katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).
Ndugu Wanahabari,
Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania imeendelea kuimarisha usalama wa usafiri wa anga ikiwa ni pamoja na kutoa huduma za uongozaji ndege zilizo salama kwa ndege zinazopita katika anga la Tanzania na ndege zinazotumia viwanja vya ndege nchini.
Aidha, ili kuendelea kuongeza imani kwa mashirika ya ndege ya kimataifa kutumia anga la Tanzania katika safari za ndege zao, mwaka 2019, Serikali kupitia TCAA ilinunua mitambo minne (4), ya rada zenye teknolojia ya kisasa za kuongozea ndege za kiraia. Rada hizo zimefungwa katika mikoa ya Dar es salaam, Kilimanjaro, Mwanza na Mbeya.
Hivi sasa ndege yoyote ya kiraia inayopita katika anga lote la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaoneka kupitia Rada hizo. Kufungwa kwa rada hizi mpya kulisababisha rada iliyokuwepo awali kusitishwa kutoa huduma. Pamoja na uwepo wa Rada hizo, Serikali imeendelea na mipango yake ya kuimarisha mawasiliano ya huduma za uongozi ndege kwa kuendelea kubadilisha mifumo ya zamani na kuweka mifumo mipya ya mawasiliano yenye teknolojia ya kisasa ili anga la Tanzania liendelee kuwa salama na la kuvutia uwekezaji.
Ndugu Wanahabari,
Baada ya kupata uhuru mwaka 1961 hadi 1967, huduma za hali ya hewa nchini zilikuwa zinatolewa na Idara ya Hali ya Hewa ya Afrika Mashariki iliyokuwa na Ofisi zake Kabete, Kenya. Mwaka 1977, baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, huduma za hali ya hewa nchini zilihamishwa na kuwa chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kama Idara Kuu ya Hali ya Hewa (Directorate of Meteorology - DoM).
Aidha, wakati tunapata uhuru, tulikuwa tunamiliki vituo viwili vya rada za hali ya hewa zilizokuwa Dar es Salaam na KIA, lakini kutokana na mabadiliko ya Teknolojia, Rada hizo zilipitwa na wakati na hivyo hazitumiki tena. Wakati huu ambao tunaadhimisha miaka 60 ya Uhuru, Tanzania tunazo Rada za kisasa za hali hewa zipatazo tatu (3) zilizofungwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Mtwara.
Hadi sasa wastani wa asilimia 85 ya malipo yamefanyika kwa ajili ya ununuzi wa rada nne (4), zitakazofungwa katika Mikoa ya Kigoma, Mbeya, Dodoma na Kilimanjaro. Kazi ya utengenezaji wa rada hizo inaendelea na itakamilika Machi, 2022. Ujenzi wa miundombinu ya majengo na njia ya umeme kwa vituo vya rada hizo unaendelea. Kufungwa kwa rada hizo kutaiwezesha Tanzania kuwa na Rada saba (7), za hali ya hewa na hivyo kukidhi matakwa ya Shirika la kimataifa la Hali ya Hewa (World Meteorological Organization - WMO).
Ndugu Wanahabari,
Katika kipindi cha miaka 60 iliyopita, huduma za usafiri katika maziwa Makuu ya Tanganyika, Victoria na Nyasa zimeendelea kutolewa na Kitengo cha Usafiri Majini kilichokuwa chini ya lilikuwa Shirika la Reli Tanzania (TRC) na baadaye kuanzia mwaka 1999 ziliendelea kutolewa na Kampuni ya Huduma za Meli (Marine Service Company Limited - MSCL). Kampuni hii imeendelea kuwa kiungo muhimu kwa kufanya biashara na Nchi zinazotegemea huduma za meli kupitia maziwa hayo kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na kijamii kama Uganda, Kenya, Sudan Kusini, Rwanda, Burundi, DR-Congo, Zambia na Malawi.
Ndugu Wanahabari,
Mara tu baada ya Uhuru, Serikali iliendelea kutoa huduma ya usafiri wa majini katika maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa kwa kutumia meli tatu (3) za M.V. Victoria na M.V. Clarias katika Ziwa Victoria; na M.V. Liemba katika Ziwa Tanganyika. Aidha, Serikali ilinunua meli mpya saba (7), zilizotumika kama ifuatavyo: M.V. Butiama, M.T. Ukerewe na M.V. Serengeti katika Ziwa Victoria; M.T. Sangara na M.V. Mwongozo katika Ziwa Tanganyika; na M.V. Songea na M.V. Iringa katika Ziwa Nyasa.
Meli hizo pamoja na meli nyingine zilizokuwepo kabla ya uhuru zimekuwa zikisafirisha abiria na mizigo katika maziwa hayo matatu na hivyo kusaidia kukuza biashara na kuboresha maisha ya jamii. Hadi mwaka 2015, Kampuni hii ilikuwa inamiliki meli 14 ambazo kati ya hizo Meli 9 zipo katika Ziwa Victoria, Meli 3 na Boti 1 katika Ziwa Tanganyika na Meli 2 katika Ziwa Nyasa. Meli nyingi kati ya hizi zimekuwepo tangu Uhuru wa nchi hii na hivyo zimechakaa na nyingine kusimamishwa kutoa huduma kutokana na usalama wake kwa maisha ya watu na mali zao. Hadi Januari, 2017, MSCL ilikuwa na meli tatu (3) za MV.Umoja, MV Liemba na MV Songea zilizokuwa zinatoa huduma.
Ndugu Wanahabari,
Kutokana na kudorora kwa Kampuni hii katika utoaji wa huduma pamoja na umuhimu wake kwa wananchi wanaoishi katika maeneo ya maziwa makuu na uchumi wa nchi kwa ujumla, Serikali iliamua kufufua huduma za usafiri kwa njia ya maji kwa abiria na mizigo katika maziwa hayo. Hivyo, mwaka 2018, Serikali ilianza kutenga fedha kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa miradi mikubwa minne katika Ziwa Victoria, kama awamu ya kwanza ya mpango wa kufufua huduma za usafiri katika maziwa makuu kupitia MSCL. Awamu hii ilihusisha ujenzi wa Meli mpya ya MV Mwanza “Hapa Kazi Tu”, yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Victoria, Mkataba wa ujenzi ulisainiwa Septemba, 2018 na unatarajiwa kukamilika Novemba, 2022. Ujenzi wa meli hii umekamilika kwa asilimia 81.
Mradi wa pili ni ujenzi wa Chelezo ambayo inatumika kama kitanda cha meli kabla haijashushwa katika maji wakati ikiundwa. Ujenzi wa chelezo hii katika Ziwa Victoria ulikamilika Machi, 2020 na upo kwenye kipindi cha uangalizi. Miradi mingine ilikuwa ni ukarabati wa Meli za MV Victoria na MV Butiama ambao umekamilika Aprili, 2020 na Meli hizo zinaendelea kutoa huduma katika Ziwa Victoria.
Ndugu Wanahabari,
Awamu ya pili ya uboreshaji wa huduma za usafiri kwenye maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa inahusika miradi sita (6). Miradi hiyo ni:
- Ujenzi wa meli mpya yenye uwezo wa kubeba tani 3,000 za mabehewa ya mizigo katika Ziwa Victoria. Mkataba wa mradi huu ulisainiwa tarehe 15 Juni, 2021 na unatarajiwa kukamilika Septemba, 2023. Kwa sasa mkandarasi anaendelea na maandalizi (mobilization).
- Ukarabati mkubwa wa meli MV. Umoja inayobeba mabehewa katika Ziwa Victoria. Mkataba wa mradi huu ulisainiwa tarehe 15 Juni, 2021 na unatarajiwa kukamilika Septemba, 2023. Kwa sasa mkandarasi anaendelea na maandalizi (mobilization).
- Ukarabati wa meli ya kubeba shehena ya mafuta ya MT. Sangara katika Ziwa Tanganyika. Mkataba wa mradi huu ulisainiwa tarehe 15 Juni, 2021 na unatarajiwa kukamilika Septemba, 2022. Mkandarasi anaendelea na maandalizi (mobilization), tayari kwa ajili ya kuanza utekelezaji utakaofanyika katika Chelezo kilichopo bandari ya Kigoma.
- Ujenzi wa meli mpya ya kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Tanganyika. Mkataba wa mradi huu ulisainiwa tarehe 15 Juni, 2021 na unatarajiwa kukamilika Machi, 2024. Kwa sasa, Mkandarasi anaendelea na maandalizi (mobilization), tayari kwa ajili ya kuanza utekelezaji utakaofanyika katika eneo la Chuo cha Uvuvi (FETA), Kibirizi, Mkoani Kigoma.
- Ujenzi wa meli mpya ya kubeba shehena ya mizigo kiasi cha tani 2,800 katika Ziwa Tanganyika. Mkataba wa mradi huu ulisainiwa tarehe 15 Juni, 2021 na unatarajiwa kukamilika Machi, 2024. Kwa sasa mkandarasi anaendelea na maandalizi (mobilization), tayari kwa ajili ya kuanza utekelezaji wake utakaofanyika katika eneo la Chuo cha Uvuvi (FETA), Kibirizi Mkioani Kigoma.
- Ujenzi wa meli mpya ya kubeba shehena ya mizigo kiasi cha tani 2,700 katika Bahari Hindi. Mkataba wa mradi huu ulisainiwa tarehe 15 Juni, 2021 na unatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2024.
Serikali inaendelea na taratibu za kuanza Mradi wa Ukarabati mkubwa wa meli ya kubeba shehena ya mizigo (mafuta) ya MT. Nyangumi iliyopo Ziwa Victoria na Ukarabati wa meli ya uokozi na kuvuta matishari ya MT. Ukerewe.
Ndugu Wanahabari,
Bandari ni kiungo muhimu katika uchukuzi kati ya nchi kavu na majini na zaidi ya asilimia 85 ya biashara yote duniani inasafirishwa kupitia huduma za bandari. Tanzania ina ukanda wa bahari wenye urefu wa kilomita 960 na bandari kuu tatu ambazo ni Dar es Salaam, Tanga na Mtwara. Pia ina maziwa makuu matatu ambayo yana bandari kuu za Mwanza, Bukoba, Musoma na Kemondo katika Ziwa Victoria; Kigoma na Kasanga katika Ziwa Tanganyika; na Itungi na Mbambabay katika Ziwa Nyasa. Bandari zote hizo zinasimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).
Aidha, bandari za Tanzania ni tegemeo katika kuhudumia shehena ya Tanzania na nchi za jirani za Burundi, Rwanda, Congo na Uganda ambazo zinatumia reli ya kati (TRC); na Zambia, DR Congo na Malawi zinazotumia reli ya TAZARA. Usafiri wa barabara pia hutumika katika kusafirisha bidhaa za nchi hizi kutoka na kuingia bandarini.
Ndugu Wanahabari,
Wakati Tanzania Bara, inapata uhuru wake mwaka 1961, nchi tatu za Afrika Mashariki zilikuwa kwenye mkataba wa ushirikiano katika kumiliki vyombo vikuu vya usafirishaji njia ya reli, huduma ya barabara, huduma za meli na bandari, huduma za anga, na karakana kuu zilizokuwa katika miji ya Dar es Salaam na Nairobi. Kufuatia mvutano kati ya Tanzania na Kenya, uliosababisha kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977, mali na madeni ya Jumuiya viligawanywa baina ya nchi hizo tatu na kila nchi ilikuwa huru na yenye mamlaka ya kuhifadhi mali zake. Hivyo, tarehe 11 Februari, 1977, Tanzania ilianzisha Mamlaka ya Bandari Tanzania (Tanzania Harbours Authority).
Ndugu Wanahabari,
Wakati wa mgawanyo wa bandari za Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977, Tanzania ilikabidhiwa Bandari mbili (2) za Dar es Salaam na Tanga kwa ajili ya kuziendesha. Kutokana na mabadiliko mbalimbali ya kimuundo, kisheria na kiutendaji, hivi sasa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), inasimamia jumla ya Bandari rasmi 89 zinazotambuliwa na Sheria ya Bandari Sura ya 166 kama ifuatavyo:-
(a) Bandari 12 ziko katika mwambao wa Bahari ya Hindi ambazo ni Bandari ya Dar es Salaam ambayo ni lango kuu (1), bandari kuu mbili (2) za Tanga na Mtwara, bandari tano (5) ndogo za Kilwa, Lindi, Mafia, Pangani, Bagamoyo na Bandari ndogondogo nne (4);
(b) Bandari 24 zipo katika Ziwa Victoria ikiwa ni pamoja na Bandari kuu sita (6) za Mwanza Kusini, Mwanza Kaskazini, Bukoba, Kemondo Bay, Nansio na Musoma pamoja na Bandari nyingine ndogondogo 18
(c) Bandari 19 zipo katika Ziwa Tanganyika ikiwa ni pamoja na Bandari mbili (2) kuu za Kigoma na Kasanga pamoja na Bandari nyingine ndogondogo 17.
(d) Bandari 11 zipo katika katika Ziwa Nyasa ikiwa ni pamoja na Bandari kuu mbili (2) za Itungi na MbambaBay pamoja na Bandari nyingine ndogondogo tisa (9).
Aidha, zipo Bandari nyingine 23 zinazohudumiwa na TPA lakini hazijaainishwa kwenye Sheria Namba 17 ya Mwaka 2004 (The Ports Act No. 17). Kati ya bandari hizo, Bandari sita (6) zipo katika mwambao wa Bahari ya Hindi, Bandari saba (7) katika Ziwa Victoria, Bandari sita (6) katika ziwa Tanganyika na Bandari nne (4) za Ziwa Nyasa. Taratibu za kutambua Bandari hizi kisheria zinaendelea.
Hata hivyo, TPA imeendelea kutambua na kurasimisha bandari zisizo rasmi ambapo hadi Juni 2021, jumla ya Bandari 693 zisizohudumiwa na TPA zilikuwa zimetambuliwa. Kati ya hizo, Bandari 239 ziko katika mwambao wa bahari ya Hindi, Bandari 329 katika Ziwa Victoria, Bandari 108 katika Ziwa Tanganyika na Bandari 17 katika Ziwa Nyasa. Taratibu za kuidhinisha Bandari hizo kwa mujibu wa sheria zinaendelea kutekelezwa.
Ndugu Wanahabari,
Kumekuwa na ongezeko la Shehena kupitia bandari za Mamlaka tangu wakati wa Uhuru mwaka 1961 hadi mwaka 2021. Shehena imeongezeka toka tani Milioni moja laki moja na elfu themanini na tano (1,185,000) mwaka 1961 hadi kufikia tani Million kumi na saba laki saba na kumi na sita elfu mia nne na ishirini na tisa ( 17,716,429) zilizohudimiwa katika mwaka 2020/2021. Bandari ya Dar es salaam ndiyo kubwa kuliko bandari zote zilizo Tanzania. Katika mwaka 1961, lango la bandari hii lilikuwa na uwezo wa kuingiza meli zenye urefu wa mita 145 – 175 na kulikuwa na kina cha maji cha mita 7. Mwaka 1998 ilichimbwa kufikia kina cha mita 10.5 na upana wa mita 140 ili kuruhusu meli kuingia saa 24. Hivi sasa bandari hii ina kina cha mita 14.5 na lango linaruhusu meli zenye ukubwa usiozidi mita 234.
Ndugu Wanahabari,
Katika mwaka 1961, Bandari ya Tanga ilikuwa na kina kifupi kilichosababisha meli kufunga nje ya bandari (outer anchorage), na hivyo mizigo kupakiwa na kupakuliwa kwa kutumia pantoni. Hivi sasa kazi ya uboreshaji wa Bandari ya Tanga awamu ya pili unaendelea ili kuongeza kina cha gati za Bandari hiyo na hivyo kuondokana na gharama kubwa za kuhudumia meli nangani.
Bandari ya Mtwara ilianza mwaka 1954, ambapo gati mbili zilijengwa pamoja na reli ya Nachingwea. Reli ya Nachingwea iliondolewa mwaka 1963 na hivyo kuathiri shughuli za bandari. Kutokana na uchakavu wa bandari hii, Serikali inaendelea kuboresha bandari hii kwa kujenga gati nne za kisasa ambapo ujenzi wa gati moja (multipurpose terminal) lenye urefu wa mita 300 katika Bandari ya Mtwara ulioanza Machi, 2017 ulikamilika Oktoba, 2020.
Ndugu Wanahabari,
Wakati tunapata uhuru, katika Ziwa Victoria kulikuwa kuna Bandari za Mwanza, Bukoba, Nansio na Musoma; Ziwa Tanganyika ilikuwa Bandari ya Kigoma; na Ziwa Nyasa ilikuwa ni Bandari ya Kyela. Kutokana na mahitaji ya kuboresha miundombinu ya bandari iliyopo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa bandari mpya ili kuhimili ongezeko la shehena, hivi sasa kuna ongezeko kubwa la bandari katika Maziwa Makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.
Hadi Juni, 2021, magati mapya yaliyojengwa katika Ziwa Victoria ni pamoja gati la Lushamba; gati la Ntama; gati la majahazi Mwigobero; gati la Nyamirembe; gati la Magarini; na ukarabati wa Bandari ya Mwanza, Kemondo na Bukoba. Katika Ziwa Tanganyika ni pamoja na gati la Kagunga; gati la Kalya (Sibwesa), na gati la Kabwe (Nkasi). Katika Ziwa Nyasa ni pamoja na bandari ya Kiwira.
HITIMISHO:
Taarifa hii inaonesha kwa ufupi historia ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi yenye hatua mbalimbali za ukuaji wa sekta kwa mantiki ya Miundombinu na huduma za Ujenzi na Uchukuzi kwa kipindi cha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Takwimu zilizopo hapo juu zimeonesha tulikotoka tangu Uhuru wa Tanzania Bara Desemba, 1961 na tulipo sasa na tuendako katika maendeleo ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
Hatuna budi kujivunia historia yetu ya maendeleo chanya yaliyofanywa na Serikali za awamu ya kwanza chini ya Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere hadi awamu hii ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA NA KAZI IENDELEE……
No comments :
Post a Comment