Friday, November 12, 2021

Wakurugenzi, Fedha Za Wadau Ziingizwe Kwenye Mipango Ya Halmashauri-Waziri Ummy

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu

Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu amewataka Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha Fedha za Wadau wa Afya zinaingizwa kwenye mipango na bajeti za Halmashauri.

Waziri Ummy ameyasema hayo wakati wa kufunga mradi wa USAID Boresha Afya Kanda ya Kaskazini.

“Natoa maelekezo kwa Wakurugenzi wote nchini wahakikishe fedha zote zinazochangia jitihada za Serikali katika miradi ya afya kutoka kwa wadau wa maendeleo wanaofanya utekelezaji wa shughuli za miradi katika mkoa na halmashauri zijulikane na zionekane katika mipango ya mwaka ya halmashauri.

Na utekelezaji wake ufanyike kwa muda ulipangwa ili kutoa huduma zenye ubora unaotakiwa.

Pia niwahakikishie wadau kuwa tutaendelea kuwapa ushirikiano wa kutosha kwa sababu nia yetu ni moja nayo ni kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za Afya.

Aliongeza kuwa Serikali inatambua umuhimu wa Wadau wa maendeleo wa Afya katika kuchangia juhudi za serikali katika kuimarisha utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.

Na kwa kutambua hilo, serikali imetengeneza mazingira rafiki ya uwepo na ushiriki wa sekta binafsi katika utoaji wa huduma kwa kutengeneza mfumo wa ushikishwaji ikiwemo uwepo wa sera ya ubia, sheria ya asasi zisizokuwa za kiserikali na miongozo ambayo inarahisisha ushirikiano wetu” Mhe Ummy.

No comments :

Post a Comment