Adeladius Makwega, Mbagala
Mwaka 2006 Mathayo Davidi Mathayo ambaye alikuwa ni Waziri katika Serikali ya awamu ya nne alifika Semtema Iringa katika zoezi la ukaguzi wa shule ambazo zilikuwa za kata kwa nia ya kuzikagua ili kuwapokea wanafunzi waliokuwa wakianza kidato cha kwanza.
Kwa maelezo ya mheshimiwa huyu alisema kuwa mawaziri wote waliagizwa katika kikao cha Baraza la Mawaziri kuzunguka nchi nzima alafu taarifa hiyo ilitakiwa na mheshimiwa rais. Kila Waziri na Naibu wake waligawiwa mikoa ambayo walizunguka nchi nzima ili kupatikana picha ya pamoja ya hali za shule za kata kabla ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2007.
Kwani kwa wakati huo kulikuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi waliomaliza darasa saba baada ya mpango wa MEMKWA kufanikiwa sana. Kwa wale wasiokumbuka hilo nawakumbusha wakati ule kulikuwa na ujenzi mkubwa wa madarasa, vyoo na nyumba za walimu za shule za msingi na baadaye shule za sekondari za umma nchi nzima.
Kwa hiyo Waziri Mathayo David Mathayo alipofika hapo alipokelewa na wananchi wa eneo hili la Semtema akiwamo Diwani wa Kata ya Kihesa wa wakati huo na Mwenyekiti wa Mtaa wa Semtema kwa wakati huo akifahamika kama Bibi Zainabu Kufakunoga na viongozi wa CCM wa kata hiyo..
Kwa kuwa mheshimiwa Mathayo Davidi Mathayo alikuwa kiongozi wa kitaifa aliongozana na viongozi wa Wilaya ya Iringa Mjini ili kukagua madarasa ambayo yalikuwa yamejengwa kwa nguvu za wananchi, wadau na serikali. Siku hiyo alikuta madarasa matatu yakiwa yameezekwa kwa bati.
Baada ya kuikagua shule hiii mheshimiwa huyu alikuwa na kamera maalumu akirekodi hali ya shule ilivyo. Kwa mtazamo mwingine ilionekana kana kwamba palikuwa na maagizo ya kupata picha halisi ya shule hizo kutoka kwa Baraza la Mawaziri.
Msafara huo wa mheshimiwa waziri uliambatana na timu ya wanahabari Mkoani Iringa Akiwamo Francis Gondwin, Frank Leonard, Dominiki Sichalel, mzee mmoja alikuwa mwandishi wa magazeti ya kiingereza ya East Africa, Daily Nation ya Kenya Malangalila na Marehemu Daud Mwangosi.
Shule ya Sekondari Semtema wakati wa ujenzi, kwa sehemu kubwa iliwashrikisha wadau mbalimbali wakiwamo Chuo Kikuuu cha Tumaini Iringa. Chuo hiki kilishiriki kikamilifu kwa sababu kilikuwa na kozi ya Shahada ya Ualimu wa Hisabati kwa hiyo kukamiliki kwake ingesaidia walimu tarajali kufanya mazoezi jirani na chuo hiki na kuwapunguzia gharama.
Kwa hiyo mwenyekiti wa mtaa wa Semtema Bi Zainabu Kufakunoga aliwaalika wadau wake nambari moja ambao ni Chuo hiki Kikuu. Chuo Kikuu hiki kiliwaagiza wanachuo wake wa Shahada ya Sanaa ya Habari kushiriki kikamilifu na kuripoti tukio hilo.
Kwa hiyo hadhara iliyokuwepo katika tukio hilo ilikuwa ni mchanganyiko wa wasomi wengi wa chuo kikuu na wananchi wa kawaida na nadhani mheshimiwa Waziri Mathayo hakulifahamu hilo.
Kwa hiyo mheshimiwa huyu alipomaliza kuigakua shule ambayo ilikuwa imezungukwa na vichaka vikubwa vya miti na majani akaombwa kuongea na wananchi.
“Jamani hapa tunawapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwakani na natambua idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na shule hii kwa hakika wataanza masomo mara moja.”
Kauli hiyo ilileta mashaka kwa wananchi kwa kuguna mmmmm…waliokuwepo pembeni wakiwa wamekaa kando ya kivuri cha mti ulikuwa ukiwapa nafuu ya jua kali la mchana huo.
Utata huo uliibua maswali mengi kutoka kwa wanachuo cha Tumaini waliokuwa wanasoma Shahada ya Sanaa ya Habari wakitaka kujua kwa muda uliokuwepo ni jambo gani linaweza kufanyika kuokoa jahazi la kuweza kuwapokea wanafunzi hao wa kidato cha kwanza? Au mheshimiwa alikuwa akianua jamvi juani tu. Kwani wasomi hao wakitolea mfano ukusanyaji wa fedha ulikuwa mgumu kutoka kwa wananchi ambapo hadi waziri anafika hakukuwa na choo, ubao wa kufundishia na wala ofisi ya walimu.
Swali hilo lilibua kelele kwa wananchi wakimuunga mkono muuliza swali lakini halikuwa gumu kujibiwa na Waziri Mathayo Davidi bali ulikuwepo ugumu wa kuiaminisha jamii ya wakaazi wa Semtema juu ya kukamilika kwa shule hiyo haraka na kuwapokea wanafunzi hao wa kidato cha kwanza, wakati hata mwalimu mmoja hakuwepo.
Swali hilo lilimuibua marehemu Daudi Mwangosi kumfuata yule mwanafunzi wa chuo kikuu cha Tumaini Iringa aliyeuliza swali akisema kuwa umeuliza swali zuri ambalo lilibeba ukweli wa hali halisi ilivyo lakini swali hilo limeibua taharuki hata sababu ya kuja hapa kwa waziri imemezwa badala ya kuwatia moyo wananchi imewakatisha tamaa.
Mazungumzo yalikuwa makubwa huku waziri akiwa ndani ya gari yake na viongozi wa wilaya tayari kwenda Iringa Mjini. Huku waandishi wengine wakiwa kimya pengine kimoyomoyo wakisema kuwa leo tumepata stori nzuri baada ya kupata mrejesho wa wananchi juu ya kauli ya waziri bila ya kuwahoji.
Kweli jioni ya siku hiyo na asubuhi baada ya tukio hilo habari kubwa ilikuwa ni juu ya swali lile la mwanachuo kutilia shaka mpango wa MESS kutokana na MEMKWA kuongeza idadi kubwa na wanaofaulu kidato cha kwanza.
Nachotaka kusema kwa siku leo ni kuwa tazama namna mwanafunzi wa Shahada ya Sanaa ya Habari alivyouliza swali ambalo lilijenga habari ya siku hiyo lakini pia tazama namna Daud Mwangosi alivyokuwa akisisitiza mahusiano mazuri baina ya serikali na wanahabari wilayani Iringa.
Tukio hilo kutokana na kuripotiwa na vyombo vya habari vingi kweli serikali ilitoa pesa kwa haraka na shule hii ilijengwa usiku na mchana kwa kujenga vyoo, ofisi ya walimu na mbao za kufundishia na waliwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa wakati na naambia kuwa kuwa hadi sasa ni shule kubwa ya sekondari ikiwa na nyumba za walimu.
Ukilitazama tukio hilo Daudi Mwangosi hakuwa na elimu kubwa ya habari lakini alitambua na kuheshimu ushirikiano wa wanahabari na serikali lakini msomi huyu wa chuo kikuu alitambua umuhimu wa viongozi kuwa wakweli na swali lake likawa chachu ya kuchapirisha ujenzi wa sekondari hii.
Naweka kalamu yangu chini nikisema kwa pamoja tutashinda na tukiwatenga baadhi ya wenzetu kwa mizengwe ya sheria tutashindwa.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
No comments :
Post a Comment