Thursday, November 18, 2021

Wahamiaji Haramu Wahukumiwa Jela Miaka Miwili Au Faini Sh. 500,000

Na Amiri Kilagalila, Njombe
MAHAKAMA ya wilaya ya Makete mkoani Njombe,imewahukumu kulipa faini shilingi 500,000/= kila mmoja au kutumikia kifungo cha miaka miwili gerezani wahamiaji haramu wapatao 18 waliokamatwa hivi karibuni katika kijiji cha Iwawa kwa kosa la kuingia nchini bila ya kuwa na paspoti au kibali kinyume na sheria.

Katika kesi hiyo namba 71 ya mwaka 2021 ni ya Jamhuri dhidi ya Gurano Adane Babiso na wenzake 17 ambapo wote ni raia wa nchi ya Ethiopia, wamepandishwa tena kizimbani Novemba 17, 2021 katika mahakama ya Wilaya ya Makete

Washtakiwa hao 18 wanashitakiwa kwa kosa la kuwa nchini yaani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila kuwa na paspoti au kibali kinyume na kifungu namba 45(1)i na kifungu kidogo cha (2) cha sheria ya uhamiaji sura ya 54 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2016

Washtakiwa wote kwa pamoja wamesomewa shitaka linalowakabili mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo Ivan Msaki na Mwendesha mashitaka wa serikali Inspekta wa Jeshi la Polisi Benstad Mwoshe.

Mara baada ya kusomewa shitaka hilo, washtakiwa wote wamekiri kutenda kosa hilo hivyo mahakama hiyo kuwatia hatiani kwa kosa la kuwepo hapa nchini bila paspoti au kibali

Kabla ya kutoa hukumu hiyo mwendesha mashtaka wa serikali Bw. Mwoshe ameieleza mahakama hiyo kuwa hana rekodi za nyuma za washtakiwa hao hivyo kuiomba mahakama itoe adhabu kwa washtakiwa kwa kuwa kosa walilolitenda ni kinyume na sheria za nchi

Hakimu Mkazi Mfawidhi Ivan Msaki alipotoa nafasi kwa washtakiwa hao kujitetea kabla ya hukumu kutolewa, wamesema wameondoka nchini mwao kutokana na hali ngumu ya maisha iliyopo huko na kulazimika kwenda kutafuta maisha nje ya nchi hivyo wanaomba mahakama iwaonee huruma

Hakimu Msaki amesema amezingatia utetezi wa washtakiwa hao waliousema na ikizingatiwa kosa hilo ni la mara ya kwanza kwao hivyo mahakama hiyo imewahukumu kulipa faini ya shilingi 500,000/- kila mmoja au kutumikia kifungo cha miaka miwili gerezani

Hata hivyo washtakiwa hao wote wameshindwa kulipa faini hiyo hivyo wamepelekwa gerezani

Mnamo Novemba 10, 2021 jeshi la polisi kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji na Wananchi waliwakamata wahamiaji haramu hao katika eneo la Kisajanilo Kijiji cha Iwawa wilayani hapo wakiwa njiani kuelekea nchini Malawi jambo ambalo ni kinyume na sheria za Tanzania.

No comments :

Post a Comment