Waziri wa Madini, Doto Biteko amewakaribisha wadau wa madini nchini kutembelea banda la Wizara ya Madini katika Maadhimisho yanayoendelea katika Ofisi za Wizara ya Madini jijini Dodoma.
Akiwa kwenye banda la Wizara, Waziri Biteko amewapongeza wadau wa madini wanaokuja kupata elimu juu ya shughuli za Sekta ya Madini.
Aidha, Waziri Biteko amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imerahisisha mazingira ya sekta binafsi zinazojishughulisha na uchimbaji madini ili kuziwezesha kuzalisha zaidi na kulipa kodi.
Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma Waziri Biteko amesema, Wizara anayoisimamia ina Mkataba wa Huduma kwa Mteja ambao unawawezesha wateja wake wakiwemo watumishi na wadau wa madini kujua huduma wanayostahili kuipata.
“Kama mnavyojua uchimbaji madini kote nchini kwa asilimia 90 unategemea sekta binafsi, kwa hiyo tumekuwa wepesi sana kuihudumia sekta binafsi ili iweze kuzalisha zaidi na kutuwezesha kupata kodi,” amesema Waziri Biteko.
Pia, Waziri Biteko amesema kuwa, Wizara ya Madini inaendelea kusikiliza wateja wake ili kufahamu changamoto wanazokabiliana nazo pamoja na ushauri, na kwamba imekuwa ikikutana na wadau mbalimbali wa madini wakiwemo wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa ili kuhakikisha wanazimaliza changamoto zao.
“Wizara ya Madini imebadilika sana, mfumo wa utoaji huduma umekuwa mwepesi sana, sisi tunayemuangalia ni mteja, mteja wetu akihudumiwa vizuri hakika hata uzalishaji wake utaongezeka,” amesema Waziri Biteko.
Katika Maadhimisho hayo, baadhi ya Watumishi kutoka Wizara ya Madini na Taasisi zilizo chini yake wametembea na kutoa maoni, changamoto na kero mbalimbali zinazo wakabiri katika kutimiza majukumu Yao.
Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma huadhimishwa kila tarehe 16 mpaka 23 Juni kila mwaka
No comments :
Post a Comment