Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB – Filbert Mponzi (pili kushoto) na Mkurugenzi na Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Bernard Konga wakionyesha mikataba baada ya kutiliana saini ya mpango wa Bima ya Afya ‘Ushirika Afya’ kwa wakulima wa vyama vya Ushirika kwa uhakika wa huduma za matibabu wakati wote na popote wakati wa hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam. Katikati ni Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Udhibiti na Usimamizi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika – Collins Nyakunga. Kushoto ni Mwanasheria Mkuu wa NMB – Lilian Komwihangiro na kulia ni Mwanasheria wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya – Benjamin Mwalugaja.
Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB – Filbert Mponzi (kushoto) na Mkurugenzi na Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Bernard Konga wakipongezana baada ya kutiliana saini ya mpango wa Bima ya Afya kwa wakulima wa vyama vya Ushirika kwa uhakika wa huduma za matibaubu wakati wote na popote wakati wa hafla iliyofanyika.jijini Dar es Salaam. Katikati ni Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Udhibiti na Usimamizi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika – Collins Nyakunga.
………………………………………………………………………………….
Benki ya NMB na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) wameingia makubaliano rasmi ya kuwawezesha wakulima walioko ndani ya vyama vya ushirika nchini kunufaika na huduma za matibabu kupitia mpango wa bima ya afya kwa wakulima unaojulikana kama Ushirika Afya.
Katika makubaliano haya, Benki ya NMB itamlipia mkulima gharama za bima ya afya kwa wakati na mkulima huyu atarejesha mkopo huo bila riba wakati wa msimu wa mavuno na baada ya mauzo ya mazao husika.
Akizungumza katika uzinduzi wa mpango huo, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, alisema lengo lao ni kuwafikia wakulima zaidi 300,000 ndani ya kipindi cha miaka mitatu. Alisema wanufaika wa mpango huu ni pamoja na wateja na wasiyo wateja wa benki hiyo, lakini mwanzoni walengwa ni wakulima wa pamba, korosho, kahawa, katani na mahindi kote nchini.
Mponzi alisema makubaliano hayo ni mojawapo ya nia ya NMB kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha Watanzania wengi wanakuwa na bima ya afya. Hata hivyo, kwa kutambua tamaduni mbalimbali za Kitanzania, malipo ya huduma hiyo yatazingatia ukubwa wa familia kama ifuatavyo:Mkulima mwenyewe TZS 76,800 kwa mwaka; Bima ya mtoto TZS 50,400 kwa kila mtoto kwa mwaka; Familia ya mkulima, mwenza wake na watoto wawili TZS 254,400 kwa mwaka; na Familia ya mkulima, mwenza wake na watoto wanne TZS 355,200 kwa mwaka.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga, alisema kuwa, ushirikiano huu na Benki ya NMB utamwezesha mkulima na familia yake kupata huduma zote za matibabu katika mtandao mpana wa vituo zaidi ya 9,000 Tanzania Bara na Zanzibar kuanzia ngazi ya Zahanati hadi Hospitali ya Rufaa ya Taifa.
Mgeni rasmi katika tukio hilo, Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Udhibiti na Usimamizi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika – Bw. Collins Nyakunga, alizipongeza Benki ya NMB na NHIF kwa jitihada za kuhakikisha wakulima wanapata bima ya afya na hawatatumia tena pesa taslimu kujitibia. Aliwaasa wakulima kote chini kuchangamkia fursa hii kwani ni nafuu.
No comments :
Post a Comment