Monday, June 7, 2021

HESLB YAINGIA MAKUBALIANO YA KIMKAKATI NA RITA KUONGEZA UFANISI UTOAJI WA MIKOPO ELIMU YA JUU. HESLB YAINGIA MAKUBALIANO YA KIMKAKATI NA RITA KUONGEZA UFANISI UTOAJI WA MIKOPO ELIMU YA JUU.

Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) Bw. Abdul – Razaq Badru akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala na Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) Bi. Emmy Hudson akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam baada ya kusaini makubaliano ya kimkakati ya kufanya kazi pamoja na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.

Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) Bw. Abdul – Razaq Badru kushoto akimkabidhi mkataba Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala na Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) Bi. Emmy Hudson baada ya kusaini makubaliano ya kimkakati ya kufanya kazi pamoja leo jijini Dar es Salaam

……………………………………………………………………………………………………

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.

Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) wameingia makubaliano ya kimkakati kwa kutia saini kwa ajili ya kufanya kazi pamoja ikiwemo

kuhakiki vyeti vya kuzaliwa na vifo kwa waombaji mikopo ya elimu ya juu na kubadilishana taarifa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul – Razaq Badru, amesema kuwa lengo la makubaliano yao ni kuhakikisha wanafanya kazi kwa ufanisi ikiwemo kuepuka wanafunzi kuleta taarifa zilizoghushiwa.

Bw. Badru amesema kuwa makubaliano hayo yana tija kwa pande zote mbili HESLS na RITA kwani wamekuwa wakishirikiana hata bila hati inayosainiwa.

“Tutabadilishana uzoefu wa kiutendaji kati ya watumishi ili kuhakikisha kila jambo linafanyika kwa ufanisi mkubwa” amesema Bw. Badru.

Hata hivyo mebainisha kuwa Juni 25 mwaka huu wanatarajia kutoa mwongozo wa utoaji wa mikopo kwa mwaka wa masomo 2021/2022.

Ameeleza kuwa mwongozo huo utapatikana kwa lugha ya kiswahili na kiingereza katika tovuti ya HESLB – www.heslb.go.tz, na kuwataka wanafunzi kusoma kwa makini na ukizingatia kabla ya kuanza kuomba pale dirisha au mfumo utakapofunguliwa kwa miezi miwili kuanzia mwezi Julai 1 mwaka huu.

Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa wapo katika maandalizi ya kwenda mikoa mbalimbali na kambi za Jeshi la kujenga Taifa (JKT) kwa ajili ya kutoa elimu kwa wanafunzi wanatarajia kuomba mkopo wa elimu ya juu.

Hata hivyo Bw. Badru amefafanua kuwa tayari bunge limeidhinisha bajeti ya Shillingi bilioni 500 kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2021/2022 inayotarajia kuwanufaisha wanafunzi takribani 160,000.

Amesema kuwa katika utoaji wa mikopo jumla wanafunzi 149, 472 wamepangiwa mikopo yenye thamani ya Shillingi bilioni 464 kati ya hizo tayari serikali imeshatoa asilimia 85 ya bajeti yote.

Bw. Badru amesema katika ukusanyaji wa mikopo mpaka sasa wamekusanya Shillingi bilioni 168 ambapo ni sawa na asilimia 88.4 , huku akieleza kuwa lengo ni kukusanya bilioni 190 katika mwaka wa fedha 2020/ 2021.

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala na Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) Bi. Emmy Hudson, ameomba wanafunzi wote kutuma maombi yao kwa wakati, huku taarifa zao zikiwa katika mfumo wa PDF.

Bi. Hudson amesema kuwa wanafunzi wengi wamekuwa na utamaduni kwa uchelewa kutuma maombi, hivyo amewataka kuhakikisha kila kitu kinafanyika kwa wakati ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.

“Tutaendelea kufanya kazi kwa kushiriki na ufanisi ili kila kitu kiende sawa katika kuhakikisha taarifa zinakuwa sahihi kwa waombaji wa mikopo ya elimu ya juu” amesema Bi. Hudson.

 

No comments :

Post a Comment