Serikali ya Tanzania, Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF) waungana na Mabalozi wa
nchi za Nordic (Sweden, Denmark, Finland na Norway) kwenye kongamano la siku moja kujadili mwelekeo wa Tanzania katika mageuzi ya kidigitali katika zama za Mapinduzi ya Nne ya Viwanda (Fourth Industrial Revolution).Kongamano hilo lililofanyika katika Hoteli ya Ramada, jijini Dar es Salaam lilihudhuriwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia (Uwekezaji) Profesa Godius Kahyarara, Dr. Jim Yonazi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari likiwa na kauli mbiu “Tanzania’s Path towards Prosperity: Balancing the State, Market and Community” likishirikisha wadau kutoka serikalini, taasisi za huduma, viongozi wa dini, sekta binafsi, wafanyabiashara na wadau wa uchumi.
Akichangia katika kongamano hilo, Mheshimiwa Dkt. Ndugulile alisema, Serikali ipo kwenye mkakati wa kuhakikisha inakwenda sambamba na mabadiliko ya kidigitali duniani.
Aliongeza kwamba kwa sasa Serikali kufanya maboresho ya mifumo ya utoaji huduma za kiserikali kwa jamii kwa kuihusisha jamii yenyewe kwenye kujiletea maendeleo ya kiuchumi kwa kutumia mitandao katika kufanikisha shughuli zao za kiuchumi na kijamii katika nyakati hizi za mapinduzi ya kidigitali.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia uwekezaji Profesa Godius Kahyarara amesema kuwa serikali inatumia kwa kiasi kikubwa teknolojia ya TEHAMA (ICT) katika kuhamasisha uwekezaji nchini.
“TEHAMA imekuwa msaidizi mkubwa wa kuongeza uwekezaji nchini ambapo tumekuwa tukitumia teknolojia hii kuweza kutangaza maeneo yetu ya uwekezaji na hivyo tumeweza kupata wawekezaji wengi kupitia ICT,” alisema.
Akitoa neno la utangulizi katika Kongamano hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF Dkt. Tausi Kida alisema, tangu kuanzishwa kwake 1993 Taasisi yake imetoa mchango mkubwa katika uandaaji wa sera na mikakati mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania.
Sambamba na hilo, Mkurugenzi wa ESRF alifafanua pia kwamba Taasisi yake imekuwa ikiendesha tafiti na kuendeleza programu mbalimbali zenye kuchochea matumizi ya kidigitali katika mchakato mzima wa kuwaleta wananchi maendeleo. Baadhi ya shughuli hizo ni pamoja na kutengeneza mfumo wa kuwasaidia wakulima, wafugaji na wavuvi kupata taarifa na shughuli za ugani kwa kupitia simu za mkononi.
Pia ilianzisha Maktaba Mtandao (TzOnline) ambayo umesheheni machapisho mbalimbali yahusuyo maendeleo katika Tanzania. Mtandao huu unasaidia sana watumiaji kupata machapisho na taarifa mbalimbali kirahisi kwa kupitia mtandao bila kulazimika kufika Maktaba
Naye Mheshimiwa Balozi wa Sweden Anders Sjöberg kwa niaba ya mabalozi wengine wa nchi za Nordic aliwakaribisha washiriki wote ambao waliohudhuria katika kongamano hili ambalo ni sehemu ya wiki ya Nordic nchini Tanzania.
“Shukrani za pekee ziwaendee Dkt. Tausi Kida Mkurugenzi Mtendaji ESRF na ESRF kwa ujumla kwa ushirikiano wetu wa pamoja katika kuandaa kongamano hili” alisema Balozi wa Sweden.
“Kama Mabalozi wa Nordic wakati mwingine tunakumbushwa kwamba sisi pamoja na Tanzania tuna matarajio na malengo sawa. Wote tunataka jamii zenye usawa kiuchumi, kijamii na mazingira endelevu. Na sisi kama Mabalozi wa Nordic tunafurahi kuona Tanzania ina nia ya kufanya madadiliko katika maeneo haya,” Mheshimiwa Balozi Anders Sjöberg aliongeza.
Wadau mbalimbali walioshiriki katika kongamano hili wameshauri kuwa Tanzania lazima iende sambamba na mabadiliko ya Mapinduzi ya Nne ya Viwanda Duniani ambapo matumizi ya Teknolojia hususani mitandao lazima yapewe kipaumbele katika kukuza uchumi wa nchi.
Kongamano hilo hufanyika kila mwaka ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya Nordic kusherehekea uhusiano wa maendeleo ya muda mrefu kati ya Tanzania na nchi za Nordic. Maadhimisho hayo huambana na shughuli mbalimbali kwa wiki zima.
No comments :
Post a Comment