Na Mwandishi Maalum, Songwe
MAHABUSU na Wafungwa waliopo katika Gereza la Mbozi Mkoani Songwe, wameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kutunga sheria ya ukomo wa
upelelezi ili pamoja na mambo mengine kuhakikisha utoaji wa hakijinai unakwenda kwa wakati lakini pia kupunguza na kuondoa msongamano wa mahabusu na wafungwa katika magereza mbalimbali nchini.Wametoa ombi hilo leo ( Jumanne) mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Profesa Sifuni Mchome aliyeambatana na Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. John Jingu walipotembelea Gereza hilo kujifunza, kutambua kero na changamoto wanazokabiliana nazo watendaji wa Magereza, Wafungwa na Mahabusu.
Katika risala yako iliyosomwa na mmoja wa mahabusu hao Jumanne Athuman Ali, wamesema, kumekuwapo na ucheleweshaji mkubwa wa utoaji wa haki kwa watuhumiwa kutokana kuchelewa kwa upelelezi wa kesi ambao unachukua zaidi ya miaka mitano na kuendelea kwa baadhi ya kesi hasa zile za mauaji na uhujumu uchumi.
“Mheshimiwa Makatibu Wakuu, sisi ( mahabusu na wafungwa) tumefurahishwa sana na ujio wenu, na wewe Katibu Mkuu wa Sheria ndiyo mwenyewe, tunakuomba basi, uangalie uwezekano wa kutungwa kwa sheria ya ukomo wa upelelezi ili haki iweze kutendeka mapema, na mtuhumiwa ajue hatima yake kama anafungwa au anaachiwa huru wengi wetu humu tumeshakaa muda mrefu inauma na inasikitisha sana, na sisi tuna familia zetu, tunashughuli zetu, tusaidie katika hili”.
Pamoja na kuomba kutungwa kwa sheria ya ukomo wa kipindi cha upelelezi, mahabusu na wafungwa hao pia wamewaeleza Makatibu Wakuu hao, kwamba, ucheleweshaji wa upelelezi wa kesi umepelekea kuwa na mlundikano mkubwa wa mahabusu na wafungwa katika gereza hilo ambalo uwezo wake ni kuhifadhi wafungwa 100 lakini hadi wakati huo kulikuwa na wafungwa na mahabusu wapatao wapatao 448.
“Waheshimiwa, hatuna shida ya chakula wala matibabu katika Gereza hili, shida yetu kubwa ni msongamano tunalazimika kulala watu 160 katika chumba kimoja chumba kile kidogo Mhe. Watu 160 fikiria tunalalaje mle , na hali hii inachangiwa na ucheleweshwaji wa upelelezi wa kesi zetu tunaomba sana kwa ujio wenu mtusaidie kuitatua changamoto hii.”
Pamoja na changamoto ya mlundikano, changamoto nyigine walizozieleza ni pamoja na ubambikizwaji wa kesi ambao wameeleza hufanywa zaidi na Polisi,masharti magumu ya dhamana, na uhaba mkubwa wa maji katika Gereza hilo jambo ambalo wamesema ni hatari kwa afya zao.
Wakielezea zaidi juu ya changamoto kubwa ya ukosefu wa maji , hawakusita kumshukuru na kutoa shukrani za pekee kwa Mkuu wa Gereza hilo ACP Bosco Lupala kwa namna ambavyo amekuwa akilishughulikia tatizo hilo kwa kadri ya uwezo wake hata hivyo wakasema Mkuu huyo wa Gereza naye amefikia ukomo wake wa kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo.
“Mkuu wetu wa Gereza hili kwa kweli anajitahidi sana kutusaidia katika kukabiliana na uhaba mkubwa wa maji na kwa kweli tunampongeza sana sana lakini na yeye anafikia mahali ana kwama. Tunaomba basi kupitia ujio wenu muangalie namna ya kutusaidia katika suala hili la maji ili nasi tupate angalau maji ya kuoga hata kama ni kwa kugawana kidogo kidogo” wakasema wafungwa na mahabusu hao .
Awali Mkuu wa Gereza hilo ACP Bosco Lupala katika taarifa yake fupi kwa Makatibu Wakuu hao alielezea pamoja na mambo mengine changamoto hiyo ya upatikanaji wa maji hasa wakati wa kiangazi.
Katibu Mkuu Profesa Sifuni Mchome pamoja na kusikiliza na kupokea risala ya mahabusu na wafungwa hao, pia alitoa fursa kwa baadhi ya wafungwa na mahabusu waliokuwa na shida kubwa kujieleza mbale yake.
Akijibu na kutolea ufafanuzi baadhi ya changamoto zilizowasilishwa na mahabusu hao na wafungwa wa Gereza la Mbozi ambalo pia linahifadhi mahusubu kutoka Mahakama za Ileje na Momba, Katibu Mkuu Mchome amesema, Serikali imekuwa ikifanya na inaendelea kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali ili kupitia marekebisho hayo hali ya utoaji haki jinai iweze kutekelezwa kwa tija inayotakiwa.
Akawaeleza mahabusu na wafungwa hao kwamba, Serikali inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba, haki za watuhumiwa zinalindwa kwa kile alichosema ingawa ni mahabusu au wafungwa bado wao ni sehemu ya Jamii.
Kuhusu changamoto ya kubambikiwa kesi, Katibu Mkuu amesema Serikali inaitambua changamoto hiyo na hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa ili kuidhibiti hali hiyo ambayo alisema haileti taswira nzuri
Kuhusu shida kubwa ya maji katika Gereza hilo, Profesa Mchome ameahidi kulishughulikia baada ya kuelezwa pia na Mkuu wa Gereza hilo kwamba, ufatifi uliofanywa unaonyesha kwamba eneo lilipo gereza hilo kuna maji ya kutosha kuweza kuchimba kisima.
Pamoja na kuzungumza na mahabusu na wafungwa wanaume, Makatibu hao pia waliwatembelea wafungwa wanawake ambao wapo katika gereza hilo na kusikiliza shida zao.
Wafungwa na mahabusu wanawake wapatao 18 huku wawili kati yao wakiwa na watoto wadogo walipopewa nafasi ya kuelezea shida zao, baadhi yao walisema wapo pale kwa kesi za kumbambikiwa na kuomba wasaidiwe kwa kuwa wameshakaa muda mrefu gerezani humu na wamewaacha watoto wao ambao wengine ni wadogo na wanahitaji malezi ya mama zao.
Mfungwa mwingine yeye alitaka kufahamu kwa nini nakala ya hukumu yake hajaipata mpaka sasa.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria amemtaka Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoani Songwe kwa kushirikiana na wadau wengine kuangalia namna watakavyoweza kushughulikia kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu baadhi ya mashauri ambayo yanaweza kumalizwa bila kufika Mahakamani.
Aidha ametaka kufuatilia na kwa mujibu wa sheria kesi zote ambazo watuhumiwa wake wapo mahabusu na kuangalia kama kunauwezekano hasa kwa makosa yale madogo madogo kama kupigana yanaweza kumalizwa kwa njia ya adhabu mbadala.
Katibu Mkuu Mchome, amesema katika mambo ambayo anayasisitiza anapokutana na wadau wanaohusika na utoaji wa haki ni kuangalia namna bora zaidi ya kumaliza baadhi ya mashauri nje ya vyombo vya sheria kwa njia ya majadiliano na kwa kutoa adhabu mbadala ili wale wanaotakiwa kwenda Magerezani basi wawe ni kweli wale wanaostahili kwenda huko.
Akiwa Mkoani Songwe katika siku ya pili ya Ziara ya Kikazi ya Kawaida ya Makatibu Wakuu hao, wamepata fursa ya kuitembelea Mahakama ya Wilaya ya Momba ambayo inatekeleza shughuli zake katika majengo ya Mahakama ya Mwanzo. Ambapo alipata fursa ya kubadilishana mawazo na watendaji wa Mahakama hiyo.
Vile vile Katibu Mkuu Mchome alipata fursa ya kutembelea mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi . Ujenzi wa Mahakama hiyo unaogharimu shilingi milioni 768,270,116 unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti 2021.
Makatibu Wakuu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wapo katika ziara ya pamoja ya kuitembelea Mikoa Mipya na ile ya Pembezoni ambayo ni Songwe, Rukwa na Katavi.
No comments :
Post a Comment