Sunday, May 30, 2021

SERIKALI KUUNDA TIMU MAALUM ITAKAYOFUATILIA MALALAMIKO YA WAFUNGWA NA MAHABUSU


Gereza la Mpanda Mkoani Katavi lenye jumla ya wafungwa na mahabusu 333. Robo tatu ya Mahabusu  katika gereza hilo ni wanaotuhumiwa kwa kesi za mauaji kutokana na wingi wa mahabusu wanaotuhumiwa kwa kesi za mauaji,Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome  amelezea kusudio la Serikali la kuunda Timu Maalamu  itakayo fuatilia   kwa nini kuna hali hiyo na    malalamiko mengine  ya wafungwa na mahabusu yakiwamo ya kubambikiziwa kesi

 Na Mwandishi Maalum,Mpanda –Katavi

Idadi ya  kubwa ya   mahabusu wanaotuhumiwa  kwa  kesi za mauaji   waliopo  katika

Gereza  Mahabusu Mpanda, Mkoani Katavi, imewashangaza   Makatibu Wakuu   wa  Wizara ya Katiba na Sheria, Utumishi na Utawala Bora na Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, ambapo  sasa wanakusudia        kuunda  Timu   Maalamu itakayofuatilia  pamoja na mambo mengine  kwa nini Mkoa huo una watuhumiwa wengi kiasi hicho.

 Makatibu wakuu hao waliupata mshangao huo   mwishoni mwa wiki wakati   walipotembelea Gereza Mahabusu la Mpanda  ambako  walipata fursa ya kuzungumza na  wafungwa na mahabusu wa gereza hilo.

Makatibu Wakuu  Sifuni Mchome, Laurian Ndumbalo, na John Jingu wapo katika ziara ya kikazi ya kawaida ya kutembelea  Mikoa ya  Songwe, Rukwa na Katavi ambapo wamejionea hali halisi ya mnyororo wa  utoaji HakiJinai,changamoto zinazowakabili watumishi wa serikali na changamoto za maendeleo na ustawi wa jamii.

“Hebu  wenye kesi za  wizi nyosheni mikono, wenye kesi za ubakaji nyosheni mikono, wenye kesi za mauaji nyosheni mikono ” akaamuru Katibu Mkuu Mchome.

Katika wafungwa na mahabusu walionyosha  mikono yao kulingana na makosa yao, robo tatu ya  mahabusu  hao walikuwa ni watuhumiwa  wa kesi za mauaji.

Alipowauliza tena kwa nini  kuna idadi kubwa ya mahabusu wenye kesi za mauaji.  Walijibu kwamba wengi wao wamembikiziwa kesi hizo, au walikamatwa katika zoazoa ya polisi na kubambikiziwa kesi hizo.

Kwa mujibu wa  taarifa ya  Mkuu wa  Gereza hilo  SP Moses Mbesela ,  mahabusu wa kiume wenye kesi za mauaji na  waliokuwa wanasubiria kikao  walikuwa sabini na moja ( 71) na ambao kesi zao upelelezi unaendelea walikuwa themanini (80). Kwa upande wa Wanawake wenye kesi za mauaji na ambao wanasubiri kikao walikuwa  sita (6) na wale  ambao  upelelezi unaendelea walikuwa  watatu (3). 

Kutokana na kauli hiyo, ndipo Katibu Mkuu Sifuni Mchome aliposema “ Cha msingi  kuna matatizo hapa, tutaunda Timu Maalumu  kuja hapa ili kuweza kuchambua kesi mbalimbali, kuna kesi nyingi za mauaji hapa”.

Akasema Timu hiyo pia itashughulikio malalamiko katika eneo la utawala bora na ustawi wajamii na akawashukuru  wafungwa  na mahababusu hao kwa michango ya hoja zao na kwa  mifano michache ya kesi walizoziwasilisha kwao na kwamba watapata mahali pa kuanzia.

Kasema  masuala  mengine yatakayofuatiliwa ni  pamoja na  malalamiko ya kubambikiziwa kesi, uchukuaji wa  mali za watuhumiwa  na kwamba Timu hiyo itakapoundwa itafanya kazi yake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Mchome, Timu hiyo maalumu itakuwa  na wajumbe kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Wizara ya Mambo ya Ndani.

Kwa upande wake Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais   Menejimenti ya Utumishi  wa Umma na Utawala Bora  Laurian Ndumbalo atafuatilia na  katika ngazi za juu  baadhi ya malalamiko ya wafungwa  na mahabusu, pamoja  maombi  yaliyowasilishwa na Mkuu wa Magereza Mkoa wa Katavi kuhusu  upungufu mkubwa wa  Maafisa na Askari  magereza katika Mkoa huo.

Naye Katibu Mkuu, Maendeleo ya Jamaii, Jinsia, Wazee na Watoto, John Kingu yeye alisema, siyo jambo la kawaida kwa magereza moja kuwa na idadi kubwa kiasi hicho naye akaunga mkono kwamba kuna  kila sababu ya kuunda Timu hiyo na kuangalia shida ipo wapi kwa sababu suala hilo linahusu ustawi wa jamii.

Makatibu Wakuu hao  watatu wamemaliza ziara yao ya kikazi ya kawaida  katika mikoa ya  Songwe, Rukwa na Katavi ambapo na Jumatatu watamalizia ziara yao Mkoani Tabora.

No comments :

Post a Comment