Wednesday, May 5, 2021

NHC KUMALIZA CHANGAMOTO ZA MAKAZI DODOMA, YAENDESHA MRADI WA NYUMBA 400 KWA WAKATI MMOJA

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba NHC akizungumza na wandishi wa habari wakati wa ukaguzi wa mradi wa nyumba 300 zinazojengwa eneo la Iyumbu jijini Dodoma na nyumba 100 zinazojengwa Chamwino.
Mafundi wakiendelea na ujenzi wa nyumba 100 zinazojengwa eneo la Chamwino mkoani Dodoma.
Ujenzi wa nyumba 300 zinazojengwa kwa ajili ya kuuzwa katika eneo la Iyumbu jijini Dodoma ambao umefikia asilimia 40.
 


Charles James, Michuzi TV

KATIKA kuhakikisha inamaliza changamoto ya makazi iliyopo katika

Makao Makuu ya Nchi na Serikali mjini Dodoma, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linaendelea na ujenzi wake wa nyumba 1,000 zilizopo sehemu mbalimbali za Mji huo.

Kwa sasa NHC inaendelea na mradi wake wa nyumba 400 ambapo nyumba 300 zinajengwa katika eneo la Iyumbu jijini Dodoma huku nyumba 100 zinazojengwa kwa mtindo wa Ghorofa zikitekelezwa wilayani Chamwino.

Akizungumza na wandishi leo wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa nyumba hizo, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Dk Maulid Banyani amesema nyumba hizo 300 zinazojengwa Iyumbu ni kwa ajili ya kuuzwa huku 100 zinazojengwa kwa mtindo wa ghorofa wilayani Chamwino zitapangishwa kwa wananchi na taasisi mbalimbali.

Dk. Banyani amesema mradi huu unajengwa kwa msaada wa Serikali ambayo iliikopesha Shirika hilo mkopo nafuu wa Sh Bilioni 20 huku wao wakitoa Sh Bilioni 1.4 na kufanya jumla ya gharama ya mradi huo kuwa Sh Bilioni 21.4.

" Tunashukuru kwa mkopo huu ambao tumepewa na serikali yetu ambao ni nafuu, mpaka sasa mradi wa nyumba za Chamwino umefikia asilimia 35 na unaelekea asilimia 40 na mradi wa Iyumbu wa nyumba 300 ukiwa umefikia asilimia 40, miradi yote hii ipo ndani ya wakati na tunaamini kufikia mwezi Juni tutaanza mchakato wetu wa mauzo.

Awamu hii nyumba zetu tumezingatia ubora wa ujenzi, ukubwa wa nyumba na eneo pamoja na uzuri wa majengo,  vitu hivyo vimechangia kwa kiasi kikubwa mwamko wa wateja kuwa mkubwa na tunaamini tukitangaza rasmi mauzo tutapata wateja wengi sana," Amesema Dk Banyani.

Amesema katika nyumba 300 za Iyumbu ambazo zitauzwa bei yake itakua Sh Milioni 50-99 kulingana na ukubwa wa nyumba na eneo huku pia kukiwa na maeneo ya kupumzikia, maeneo ya Biashara, viwanja vya michezo na Shule ya awali.

" Ununuaji wa nyumba hizi unamlenga kila mtanzania yeyote, kama mtu ataamua kulipa papo kwa papo ni sawa kama ataamua kukopa pia tutamuuzia kwa makubaliano na benki ambayo amekubaliana nayo, niwasihi watanzania wa Dodoma kuchangamkia nyumba hizi zinazojengwa na Shirika lao.

Malengo yetu siyo kuishia Iyumbu na Chamwino tu, tutafikia maeneo tofauti ndani ya Mkoa huu, na pia tumejipanga kuyafikia maeneo yote ya Nchi yetu, Mkoa kwa Mkoa hadi ngazi za Wilaya, kiu yetu ni kujenga nyumba bora za Kisasa kwa ajili ya Watanzania, " Amesema Dk Banyani.

 

No comments :

Post a Comment