Wednesday, May 5, 2021

MAHAKAMA YAWAACHIA HURU VIONGOZI NA WAFUASI 27 WA CHADEMA


 MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewaachia huru viongozi na wafuasi 27 wa Chadema waliokuwa wanadaiwa kufanya mkusanyiko na kuvunja geti la gereza la Segerea chini ya kifungu cha 225(5) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai (CPA.)

Kesi hiyo imefutwa leo Mei 5, 2021 na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya upande wa mashtaka kushindwa kupeleka mashahidi mahakamani.

Mapema leo asubuhi kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa lakini upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi  Mkunde Mshanga akisaidiana na wakili wa serikali Ester Martin kudai mahakamani  hapo kuwa kuwa kwa leo hawana shaidi hivyo wameiomba mahakama kuipangia kesi hiyo tarehe nyingine ya kusikilizwa.

Upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Peter Kibatala na Edson Kilatu walipinga kuahirishwa kwa kesi hiyo na kuiomba mahakama kuifuta kwa kuwa upande wa mashtaka wameshindwa kuleta mashahidi kwa muda mrefu. 

Kesi hii imeshakuwa na maahirisho kwa muda mrefu hivyo ninawaachia huru washtakiwa wote chini ya kifungu cha 225(5)" amesema Hakimu Shaidi.

Kifungo hicho kinawapa mamlaka jeshi la polisi kuwakamata tena washtakiwa pale wanapokamilisha ushahidi.

Washtakiwa hao ni, Wabunge Halima Mdee(41) Mbunge Ester Bulaya(40)  na Jesca Kishoa( 36).

Boniface Jakobo, Patrick Assenga, Henry Kilewo,Yohana Kaunya,Kedmony Mhembo, Mshewa Karua, Khadija Mwago, Pendo Raphael maarufu kama Mwasomola na mkazi wa Bonyokwa, Cesilia Michael, Happy Abdalla; Stephen Kitomali  na Paul Makali, Edgar Adelinj na Reginald Masawe

Washtakiwa  wanakabiliwa na mashtaka saba yakiwemo ya  kutoa lugha ya kuudhi kuharibu Mali; kufanya mkusanyiko usio kuwa wa halali na kutokutii amri halali iliyowekwa na Jeshi la Magereza na shambulio.

Inadaiwa, Machi 13, 2020 , eneo la gereza la Segerea, lililopo wilaya ya Ilala, kwa makusudi washtakiwa walikaidi amri halali ya kuondoka eneo la gereza kwa amani ili eneo hilo libaki wazi, amri hiyo iliyotolewa na askari mwenye namba B 3648, Sajenti John ambaye ni mlinzi wa Geti la gereza hilo.

Katika shtaka pili ambalo ni la kufanya mkusanyiko,  washtakiwa wanadaiwa kukusanyika  isivyo halali kwenye geti la Gereza la Segerea na kusababisha hofu iliyokuwa inapelekea uvunjifu wa amani na utulivu.

Pia washtakiwa hao wanadaiwa kuharibu geti kuu la kuingilia na kutokea katika gereza la Segerea mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanznia huku Mdee, Bulaya na Jacob wakidaiwa kutoa lugha ya matusi kwa askari Magereza mwenye namba B 3648, Sajent John.

 Aidha mshtakiwa Jacob pia anadaiwa kumshambulia askari Magereza  Sajente John kwa kumvuta shati na kumchania, wakati akiwa katika utekeleza wa majukumu yake ya ulinzi kwenye geti kuu la gereza la Segerea.

No comments :

Post a Comment