Wednesday, May 26, 2021

MAKATIBU WAKUU MAENDELEO YA JAMII NA KATIBA NA SHERIA WAHAKIKISHA MFUMO WA HAKI KWA MAKOSA YA UKATILI UNAIMARIKA

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii na Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome wakiangalia mchoro wa jengo la Mahakama ya Mkoa wa Songwe iwapo umezingatia mahitaji muhimu ikiwemo ofisi za Maafisa Ustawi wa Jamii, walipofanya ziara ya pamoja yenye lengo la kuangalia namna uendeshaji wa kesi za jinai hasa ukatili zinavyofanyika.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu(kushoto) na Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Profesa Sifuni Mchome (katikati)  wakisalimiana na watendaji wa Mahakama ya Wilaya ya Momba walipowasili Ofisi ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya hiyo kwa ziara ya pamoja yenye lengo la kuangalia namna uendeshaji wa kesi za jinai hasa ukatili zinavyofanyika.
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Momba akiwasilisha taarifa ya uendeshaji wa kesi za jinai katika Mahakama hiyo kwa Makatibu Wakuu wa Afya na Katiba na Sheria wakiwa kwenye ziara yenye lengo la kuangalia namna uendeshaji wa kesi za jinai hasa ukatili zinavyofanyika.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Tunduma Regina Bieda akimkaribisha Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu kuzungumza na wajumbe wa Kamati ya MTAKUWWA ya Halmashauri hiyo katika ziara ya pamoja na Katibu Mkuu wa Katiba na Sheria yenye lengo la kuangalia namna uendeshaji wa kesi za jinai hasa ukatili zinavyofanyika.

Na Mwandishi wetu, Momba

KATIBU Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu na Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Profesa Sifuni Mchome wamewataka watendaji wote wanaohusika na upatikanaji wa haki za

makosa ya jinai kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ili kuhakikisha haki inapatikana hasa kwa waathirika wa ukatili.

Wameyasema hayo wakati wa ziara yao ya pamoja Wilayani Momba, Mkoa wa Songwe yenye lengo la kuona namna sekta mbalimbali zinavyoshirikiana katika utoaji wa haki hususani kwa watoto waliokinzana na sheria.

Akizungumza na watendaji wa Mahakama, Magereza pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Mpango wa Taifa wa kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) ya Halmashauri ya Mji Tunduma kwa nyakati tofauti, Dkt. Jingu amesema watoto wanaokinzana na sheria wana haki ya kupatiwa huduma muhimu wanazostahili.

"Watoto wanatakiwa watendewe tofauti kwa sababu wao ni tofauti, tuendelee kufanya kazi, kumekuwa na changamoto sana hasa kwenye eneo la ushahidi, wanajamii wanatakiwa kuona umuhimu wa kushirikiana na vyombo vyetu ili haki iweze kutendeka ili iwe ni fundisho kwa wengine wanaofanya vitendo kama hivyo" alisema Dkt. Jingu.

Jingu pia amesema Jamii ina nafasi kubwa ya kumaliza changamoto mbalimbali hasa migogoro kwa kutumia mifumo yao hivyo kuna umuhimu wa kuimarisha mifumo ya kijamii ambayo itasaidia kupunguza misongamano katika vyombo vingine vya utoaji wa haki.

Dkt. Jingu amesema pia Wazee ni kundi muhimu katika mchakato wa utoaji haki kwenye jamii hivyo wana nafasi kubwa ya kumaliza migogoro iwapo wakitumika vizuri.

Katika hatua nyingine, Dkt. Jingu amezitaka Kamati za MTAKUWWA kuhakikisha wanafanya kazi ya kubadili fikra potofu katika jamii ikiwemo za baadhi ya wazazi kuona ni mzigo kusomesha watoto wao.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Mchome amezitaka Mahakama kufanya jitihada za kutumia adhabu mbadala ikiwemo njia za kijamii ili kupunguza idadi ya mahabusu magerezani.

"Kwa sasa hivi takwimu zinaonesha kwamba hali ya mahabusu ni zaidi ya wafungwa ambapo wengi wao ni wale wenye makosa makubwa" alisema Prof. Mchome.

Kwa upande wake Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Momba Timothy Lyon amesema katika Wilaya hiyo kesi za watoto ni chache na wana utaratibu maalumu wa kuzishughulikia ili kulinda haki za watoto japokuwa kuna changamoto ya ukosefu wa mahabusu ya watoto na shule ya maadilisho.

Nao baadhi ya wajumbe wa Kamati ya MTAKUWWA Halmashauri ya Mji Tunduma wameishukuru Serikali hasa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo  Regina Bieda kwa kuwawezesha kutekeleza majukumu yao hivyo jamii  imeelimika na watoto wanaweza kutoa taarifa za matukio ya ukatili kwa wakati.

Makatibu Wakuu hao wametembelea pia na kujionea ujenzi wa Jengo la Mahakama ya Mkazi Songwe pamoja na kuzungumza na wafungwa wa Gereza la Songwe linalohudumia Wilaya za Mbozi na Momba.

 

No comments :

Post a Comment