Sunday, April 11, 2021

WIZARA KUJENGA VITUO 40 VYA MAFUNZO YA UFUGAJI SAMAKI, UHOLANZI YAVUTIWA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akisalimiana na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Mhe. Jeroen Verheu, mara baada ya balozi huyo kufika katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo jijini Dar es salaam, kwa ajili ya mazungumzo na Waziri Ndaki ambapo wamekubaliana kuongeza ushirikiano baina ya nchi hizo mbili katika sekta za mifugo na uvuvi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiwa kwenye mazungumzo na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Mhe. Jeroen Verheu katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo jijini Dar es salaam, ambapo balozi huyo amemhakikishia Waziri Ndaki nchi yake inaunga mkono mkakati wa wizara kujenga vituo vya mafunzo ya ufugaji samaki kila wilaya. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akimsindikiza Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Mhe. Jeroen Verheu mara baada ya kuwa na mazungumzo naye katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo jijini Dar es salaam, ambapo katika sekta ya mifugo wamekubaliana kuhakikisha asilimia 98 ya wazalishaji maziwa nchini wasio rasmi wanakuwa rasmi katika kukuza maendeleo ya nchi 

 Na. Edward Kondela


Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Mhe. Jeroen Verheu amesema nchi yake iko tayari kusaidia

ujenzi wa vituo vya mafunzo ya ufugaji samaki nchini ili kuunga mkono mkakati wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha inafikisha huduma za mafunzo hayo kila wilaya.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza jana (10.04.2021), mara baada ya kufanya mazungumzo na balozi huyo katika ofisi ndogo za wizara zilizopo jijini Dar es Salaam, amesema Mhe. Balozi Verheu ameridhishwa na mkakati wa wizara ambapo katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22 imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo arobaini vya mafunzo ya ufugaji samaki.

“Sisi kama wizara tumeanza na mkakati huo na tumetenga fedha kwa ajili ya vituo arobaini katika bajeti ijayo na kwamba wamesema wako tayari kusaidia kwa kuweka vituo vingine zaidi, tunataka kuweka vituo vya mafunzo kila wilaya kwa ajili ya wafugaji wa samaki wapate mahali pa kujifunza badala ya kwenda kwenye vituo ambavyo viko mbali.” Amesema Mhe. Ndaki

Kuhusu uchumi wa bluu Waziri Ndaki amesema balozi huyo amemhakikishia wanaweza kuisaidia Tanzania kupitia mpango wao maalum ujulikanao “Global Development Program” ambao unalenga kusaidia nchi zinazoendelea kwenye masuala ya uchumi wa bluu na kuiomba wizara iangalie maeneo ambayo inaweza kunufaika kupitia mpango huo.

Aidha, Mhe. Balozi Verheu ameisifia Zanzibar kwa hatua ilizofikia kuhusu uchumi wa bluu, huku Waziri Ndaki akimhakikishia pia Tanzania Bara imeweka malengo ya kutengeneza uchumi unaotokana na Bahari ya Hindi, maziwa na mabwawa.

Pia, katika Sekta ya Mifugo Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Mhe. Jeroen Verheu ameonesha nia yake kubwa namna nchi yake iko tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa pande zote mbili.

Waziri Ndaki amefafanua kuwa Uholanzi iko tayari kusaidia maeneo ya malisho ya mifugo pamoja na ushirikiano wa kitaalamu kwa kutoa utaalamu kwa watanzania nao kupata utaalamu kutoka kwa watanzania juu ya sekta ya mifugo.

“Nchi ya Uholanzi wameendelea sana katika tasnia ya maziwa na wamesema wako tayari kushirikiana na Tanzania katika kukuza soko la maziwa na wazalishaji wa maziwa ambapo hawako rasmi takriban asilimia 98, tunaweza kuwafanya hao wazalishaji wakawa rasmi na maziwa yao yakasaidia nchi kimaendeleo.” Amefafanua Mhe. Ndaki

Katika mazungumzo hayo Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Mhe. Jeroen Verheu wamekubaliana kuongeza wigo zaidi wa ushirikiano katika sekta za mifugo na uvuvi.


No comments :

Post a Comment