Sunday, April 11, 2021

Bolt yapokea uwekezaji wa Euro 20 milioni kutoka IFC


BOLT yapokea uwekezaji wa Euro 20 millioni kutoka IFC kuongeza upatikanaji wa huduma za usafiri katika nchi zinazoendelea

 Kampuni inayoongoza ya usafiri kwa njia ya mtandao, Bolt imepokea uwekezaji wa €20 millioni (Euro) kutoka kwa Shirika la Kimataifa la Fedha (IFC) utakaosaidia kuongeza upatikanaji wa huduma

za usafiri katika masoko yanayokua, ikiwemo Tanzania.

 Uwekezaji huo ambao unajumuisha huduma za ushauri kutoka IFC – mshirika wa Benki Ya Dunia, itasaidia Bolt kupanua huduma za usafiri zinazochangia ukuaji wa biashara ndogo ndogo, kukuza fursa za ajira na kuboresha upatikanaji wa huduma za usafiri katika masoko ya Afrika na Ulaya Mashariki.

  “Tuna matarajio makubwa ya kushirikiana na IFC kuchangia ujasiriamali, kuwezesha wanawake na kuongeza upatikanaji wa huduma nafuu za usafiri barani Afrika na Ulaya Mashariki. Uwekezaji huu ukijumuishwa na ule tuliopata mwaka jana kutoka Benki ya Uwekezaji Ulaya inatufanya tuwe na washirika wengi wakubwa wanaoamini umuhimu wa Bolt katika masoko mapya,” Markus Villig, Mkurugenzi Mkuu na Mwanzilishi wa Bolt alisema.

 Stephanie von Friedeburg, ambaye ni Makamu Mkuu wa Rais wa IFC anayesimamia masuala ya utendaji alisema “Teknologia inaweza na inafaa kufungua fursa mpya za maendeleo endelevu na kuwawezesha wanawake. Uwekezaji wetu katika kampuni ya Bolt unalenga kuwezesha teknologia kuleta mageuzi chanya katika sekta ya usafiri kwa njia ambazo ni rafiki kwa mazingira, kutoa fursa zaidi za ajira kwa wanawake na kuleta usafiri salama na wa gharama nafuu katika masoko yanayochipuka.”

 Bolt kwa sasa inapatikana katika nchi 7 barani Afrika huku ikitoa fursa za kipato wa madereva 400,000 katika miji 70 barani.

 “Tunaongeza kipato miongoni mwa jamii kwa kuwapa madereva wanaotumia mfumo wetu fursa za kujipatia malipo. Huduma zetu zinaleta mageuzi ya usafiri wa haraka na nafuu kwa mamilioni ya watu wanaoishi mjini,” Mkurugenzi wa Bolt Tanzania, Remmy Eseka alisema.

 Nchini Tanzania, Bolt inatoa huduma za usafiri wa magari, pikipiki (bodaboda) na pikipiki za miguu mitatu almaarufu bajajii katika miji ya Dar es Salaam, Dodoma, Arusha na Mwanza.

 

No comments :

Post a Comment