Thursday, April 15, 2021

TCCIA YAPONGEZA UWEKEZAJI WA DUKA LA KISASA LA KIMATAIFA LA UUZAJI SAMANI


Mkurugenzi wa Duka la OPPEIN Doroth Kihimbi  Katikati akiwa pamoja na wadau mbalimbali sambamba na Makamu wa Rais wa Shirikisho la wafanyabiashara na wenye viwanda nchini (TCCIA) Octavian Mshiu mwenye suti kulia, wakati wa ufunguzi wa duka hilo

MAKAMU wa Rais wa Shirikisho la wafanyabiashara na wenye viwanda nchini (TCCIA) Octavian Mshiu amepongeza uwekezaji wa duka la kisasa la

kimataifa la uuzaji wa samani za majumbani la ‘OPPEIN’ uliofanywa na mtanzania Doroth Kihimbi na kusisitiza kuwa hatua hiyo inatokana na mazingira wezeshi inayofanywa na Serikali kwa malengo ya kukuza uchumi wake.

Alitoa kauli hiyo Dar es Salaam juzi wakati wa ufunguzi wa duka hilo lililopo eneo la Mwenge ambalo ni miongoni mwa maduka machache ya aina hiyo ulimwenguni yanayojishughulisha na uuzaji wa  samani hizo huku akiipongeza Serikali kwa jitihada mbalimbali za kuwainua wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi sambamba na kutoa fursa nyingi za wao kujiendeleza.

Mbali na hapa nchini duka hilo lipo pia katika nchi za Uingereza, Marekani, Uswiswi, Ujerumani, Israel, Japani, Australia na Hispania, huku Mshiu akisisitiza kuwa  uwepo wake hapa nchini unatoa fursa nzuri za kibiashara huku akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufungua njia zaidi kwa wafanyabiashara na wawekezaji kufanya biashara nchini.

Mshiu alisema kutokana na sera nzuri za uwekezaji nchini, watanzania wengi wamejitokeza na kuanzisha biashara mbalimbali ambazo mbali na kuliingiza nchi mapato yatokanayo na kodi pia zimewasaidia watanzania wengi kupata ajira zinazowapa fursa ya kuendesha maisha yao ya kila siku.

“Tunampongeza mtanzania mwenzetu kwa kuthubutu kufanya uwekezaji huu hapa nchini, maduka haya yapo sehemu chache ulimwenguni, hivyo kwa kuamua kulianzisha hapa nchini pamoja na mambo mengine kutasaidia kuitangaza nchi yetu kimataifa” alisema Mshiu ambaye pia ni mjumbe wa Taasisi ya sekta binafsi.

Kwa upande wake mgeni rasmi katika ufunguzi wa duka hilo, Mchungaji wa Kanisa la ‘Enlighten Christian Gathering Church’(ECG) Patrick Manda, mbali na kumpongeza mwanzilishi wa duka hilo hapa nchini, alisema Tanzania inazidi kuneemeka kutokana na uwepo wa mazingira yanayomvutia kila mtu kuwekeza.

Huku akimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa agizo lake la kuondoa vikwazo  mbalimbali vya kodi kwa wafanyabishara, alisema  kitendo cha mwekezaji wa duka hilo ambaye ni mwanamke kinapaswa kuwa mfano kwa wanawake wengine kufuata nyendo zake kutokana na umuhimu wao katika kukuza uchumi wa Taifa.

Kwa upande wake mwekezaji wa duka hilo Doroth Kihimbi aliwaomba watanzania kumuunga mkono huku akisisitiza kuwa malengo yake ni kuona anatekeleza kwa vitendo msisitizo  unaotolewa na Serikali ukiwataka watanzania kuwekeza.

 

No comments :

Post a Comment