Muonekano wa moja ya mashine ya K-Walk Through Booth zilizotolewa na Shirika la Koica iliopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Kisauni. Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar Abdalla Salim Ally akitoa shukrani kwa Koica kwa kukabidhiwa mashine tatu za kuchukulia sampuli za maradhi ya Korona. Afisa Afya wa Kituo cha Bandari ya Malindi Samia Jamal Said akitoa maelezo ya matumizi ya mashine ya kuchukulia sampuli ya maradhi ya Korona wakati wa makabidhiano wa mashine Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume KisauniBaadhi ya Wafanyakazi wa afya wa Uwanja wa Ndege na Kituo cha Bandari ya Malindi wakifuatilia makabidhiano ya moja ya mashine ya kuchukulia sampuli kwa wasafiri wanaoingia Zanzibar.Picha na Makame Mshenga.
Na Ramadhani Ali – Maelezo
Shirika la Kimataifa la Korea, Koica limetoa msaada wa mashine tatu za kuchukulia sampuli za
maradhi ya Corona (K-Walk Through Booth) ambazo zimewekwa katika vituo vikuu vya kuingilia wageni Zanzibar.Mkurugenzi Mkaazi wa Ofisi ya Koica Tanzania Kyucheol Eo amemkabidhi Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. Abdalla Salim Ally moja ya mashine hizo katika sherehe zilizofanyika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Kisauni.
Amesema Koica itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha Mipango yake ya Maendeleo ikiwemo dira ya 2050 na Mpango Mkakati wa Maendeleo.
Ameongeza kuwa Sekta ya Afya na Elimu ni kipaumbele cha Koica hivyo msaada wa vifaa hivyo K-Walk Through Booth ni moja ya juhudi wanazochukua za kuimarisha afya za wananchi wa Zanzibar.
Dk. Abdalla amelishukuru Shirika la Koica kwa misaada inayotoa hasa kwenye sekta ya Afya ambayo imesaidia sana katika mapambano dhidi ya maradhi ya kuambukiza.
Amesema Koica walikua wa mwanzo kuisaidia Zanzibar wakati wa kukabiliana na Kipindupindu miaka michache iliyopita na hadi sasa maradhi hayo yameweza kudhibitiwa kwa kiasi kikubwa.
Amewashauri wafanyakazi watakaosimamia mashine hizo kuwa na uangilizi nzuri na kuzitunza ili zidumu kwa kipindi kirefu.
Akielezea ufanisi wa mashine za K-Walk Through Booth, Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Dk. Fadhil Abdalla amesema zitarahisisha kuchukuwa sampuli za wasafiri kwa muda mfupi na kuondosha usumbufu na msongamano uliokuwepo.
Alisema baada kuchukua Sampuli zitakazobainika kuwa na mashaka zitapelekwa maabara kwa uchunguzi zaidi.
Mashine za K-Walk Through zimewekwa Uwanja wa Ndege wa Kimatiafa wa Abeidi Amani Karume Kisauni, Bandari Kuu ya Malindi na Uwamja wa ndege wa Kisiwani Pemba.
No comments :
Post a Comment