Othman Masoud ateuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, kuchukua nafasi ya Maalim Seif Sharif Hamad aliyefariki tarehe 17 Februari mwaka huu.
Uteuzi wa Masoud umefanywa na Rais wa Zanzibar, Dkt Hussein Mwinyi baada ya mashauriano na
chama cha ACT-Wazalendo. Masoud amewahi kuhudumu katika nafasi za ngazi za juu katika serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwemo mwanasheria Mkuu wa serikali.''...Baada ya kushauriana na Chama cha ACT-Wazalendo, Rais wa Zanzibar na Mweyekiti wa Baraza la Mapinduzi , Dkt Hussein Ali Mwinyi amemteua Mheshimiwa Othman Masoud Othman Sharif kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar'', imeeleza sehemu ya taarifa kutoka Ikulu ya Zanzibar kuhusu uteuzi huo.
Masoud anatarajiwa kuapishwa rasmi kushika wadhifa huo kesho tarehe 2 Machi.
Othman Masoud aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) chini ya Dkt. Ali Mohammed Shein. Wadhifa huo ulifikia tamati Oktoba 2014 baada ya kuenguliwa.
Sura yake si maarufu katika siasa za upinzani lakini tangu afukuzwe ndani ya SMZ, amekuwa maarufu kwa misimamo yake ya kutetea maslahi ya Zanzibar katika Muungano.
Wakati wa pilikapilika za uchaguzi mkuu alikuwa mjumbe katika kamati ya ilani ya chama cha ACT Wazalendo kwa upande wa Zanzibar.
No comments :
Post a Comment