Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba akifungua warsha ya siku moja iliyoandaliwa na RITA kwa viongozi wa dini na kimila hii leo Jijini Dar es salaam kuhusu Usajili wa miunganisho ya wadhamini pamoja na kushughulikia Migogoro ya ndoa, talaka na mambo ya mirathi.
Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu Bi. Emmy Hudson akitoa maelezo ya awali wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku moja iliyoandaliwa na RITA kwa viongozi wa dini na kimila hii leo Jijini Dar es salaam kuhusu Usajili wa miunganisho ya wadhamini pamoja na kushughulikia Migogoro ya ndoa, talaka na mambo ya mirathi.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba hii leo Jijini Dar es salaam alipokuwa akifungua warsha ya siku moja kwa viongozi wa dini na wakimila iliyoandaliwa na Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kuhusu usajili wa miunganisho ya Wadhamini, ndoa na talaka na namna ya kushughulikia migogoro ya mirathi ambayo inaonakana kuongezeka kila siku katika jamii inayotuzunguka.
“Nawaomba viongozi wote wa dini na mila kutoa mapendekezo na michango mbalimbali itakayosaidia kupatikana kwa sheria jumuishi itakayotoa haki na fursa kwa makundi yote katika jamii ili kuondoa migogoro ya ndoa na mirathi’’.Alisema Mhe. Dkt. Nchemba.
Kwa upande wake Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu wa RITA Bi Emmy Hudson amesema kuwa viongozi wa dini na kimira wamekuwa nguzo muhimu katika utoaji wa elimu kuhusu umuhimu wa kusajili ndoa na talaka pamoja na kutoa muelekeo wa kushughulikia migogoro ya ndoa na mambo ya mirathi katika jamii hivyo kuwakutanisha kwa pamoja kutawezesha kupata maoni ya jinsi gani migogoro hiyo itamalizwa kwa kufuata mafundisho ya dini au miongozo ya kimila bila ya kuathiri au kukinzana na sheria za nchi.
Bi Hudson ameongeza kuwa Serikali inatambua umuhimu wa viongozi wa dini na wakimila katika utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu mambo ya ndoa, talaka na mirathi hivyo kupitia warsha hiyo itasaidia kufikisha ujumbe kwa waumini na makundi mbalimbali ili kujenga utamaduni wa kuandika wosia mapema pamoja na kuvumiliana ikitokea kutokuelewana ili taratibu za kisheria ziweze kufuatwa na kutoa haki kwa kila mmoja.
‘’Tumekuwa tukishirikiana nanyi katika mambo mbalimbali hivyo tunawaomba tuendelee kushikamana kuhakikisha hakuna migogoro tena itakayotokea inayohusu mirathi bila ya kumalizwa kwa kutoa haki kwa walengwa.’’ Alisema Bi Hudson.
Naye Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania ( BAKWATA) Sheikh. Nuhu Jabir Mruma amesema viongozi wa dini ya kiislam wamekuwa wakishirikiana kwa karibu na madhehebu mbalimbali katika kuisaidia Serikali wakati ikitekeleza majukumu yake na hata utungwaji wa sera na sheria mbalimbali na hivyo kwa warsha hiyo itasaidia kutoa mapendekezo yao kuhusu mapendekezo ya sheria jumuishi itakayotoa haki kwa makundi yote bila ya migongano ya kimaslahi katika dini husika.
Kwa upande wake Mchungaji Elisante Mshama wa Kanisa la Wasabato Tanznaia Jimbo la Kusini Mashariki ameiomba Serikali kushirikiana kwa karibu na viongozi wa dini kabla na hata wakati wa kutoa hukumu za kusudio la kuvunjika kwa ndoa ili kusaidia kuwapatia elimu wanandoa hao kurejesha imani na kuendelea kuishi kwa kwa kuvumiliana na kumuamini Mungu badala ya kuamua kufikiria njia pekee ya kumaliza migogoro ya ndoa ni kuachana.
RITA imekuwa ikiwakutanisha wadau mbalimbali wa kitaifa na Kimataifa kama sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake ya kuyafikia makundi yote katika jamii.
No comments :
Post a Comment