Thursday, March 11, 2021

MBEYA YAPONGEZWA KWA UJENZI WA JENGO JIPYA LA HOSPITALI YA WAZAZI META


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.Dorothy Gwajima akikagua ujenzi wa jengo la wazazi linalojengwa Kwenye hospitali ya Meta  jijini Mbeya.
Muonekano wa upande mmoja wa jengo Hilo ambalo litakua na vyumba 223 vikiwemo vyumba vitatu vya upasuaji na huduma za dharura.
Waziri wa Afya Dkt.Gwajima na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Albert Chalamila wakikagua upande mwingine wa jengo Hilo ambalo litagharimu shilingi bilioni 9.
Waziri wa Afya Dkt. Gwajima akipanda ngazi kukagua ujenzi unaoendelea Kwenye hospitali ya rufaa ya Mkoa Mbeya.
Waziri wa Afya Dkt.Dorothy Gwajima na Mkuu wa Mkoa Mbeya Mhe. Albert Chalamila  wakijadiliana wakati wa ukaguzi wa mradi wa ujezi wa jengo la wazazi lililopo hospitali ya Meta  na kifurahishwa na matumizi ya pesa za ujenzi huo(Picha na Catherine Sungura.)


Na.Catherine Sungura, Mbeya

UONGOZI  wa Mkoa wa Mbeya umepongezwa kwa usimamizi mzuri na hatua

kubwa iliyofikiwa kwenye mradi wa ujenzi wa jengo jipya la huduma ya wazazi katika hospitali ya wazazi ya Meta. Aidha, hatua iliyofikiwa ni 88% kwa miezi 20 tu kati ya 24 iliyokadiriwa kutumika huku hatua hiyo ikiwa imetumia bilioni 6.4 kati ya bilioni 9  zilizotarajiwa ili kukamilisha mradi huo.  

Pongezi hiyo zimetolewa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima mara baada ya kutembelea mradi huo ambao unajengwa kwa utaratibu wa ‘force account’.

Dkt. Gwajima alisema ameridhishwa na ujenzi huo kwani ni wa viwango na umaliziaji wake ni mzuri na kasi ya ujenzi wake ni nzuri. Hii inaonesha timu ya mkoa imejipanga vizuri kwenye usimamizi.

“Nimefurahishwa sana na ujenzi huu kwa mkoa wa Mbeya haya ni mapinduzi makubwa katika kuendelea huduma za afya ya uzazi na mtoto, nilikwishakupita hapa miaka ya nyuma hali ilikua tete kwenye jengo la zamani. Mkoa mmefanya  kazi kubwa na nzuri, jengo linavutia"

Mkoa mmetengeneza Kamati makini ya kununua vifaa katika kusimamia dhana ya force account, kwakweli nimefurahi.” Aliongeza.

Alisema hospitali hiyo ikikamilika itakuwa na vyumba 223 kwa ajili ya huduma, vyumba vya upasuaji vitatu, vyumba maalumu (VIP ),wodi ya kujifungua pamoja na wodi ya wagonjwa mahututi (ICU)." Kwahiyo mama mjamzito akiingia humo ndani kila kitu kitaishia humo hata kama atatakiwa kuwa kwenye uangalizi maalumu".

Hata hivyo Dkt. Gwajima alisema yapo mapinduzi na maboresho makubwa ya ujenzi  yaliyofanywa na Serikali nchi nzima katika dhana ya kuendeleza afya ya mama na mtoto kwenye halmashauri kuanzia kwenye zahanati mpaka hospitali za wilaya na mkoa ambapo vituo hivyo  vina uwezo wa kufanya upasuaji.

“ Hata kwenye jamii kuna wahudumu  wa afya ya jamii wanaofuatilia masuala ya afya ya watoto na wazazi na kutoa ushauri.  Serikali kwa kushirikiana na wananchi imejenga  zahanati 1198 katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2015, vituo vya afya  487 vyenye uwezo wa kufanya upasuaji na vituo vingi vimeanza kutoa huduma hiyo na vile ambavyo bado tunaenda kuviwezesha vianze kutoa huduma hiyo mara moja kwani Serikali imedhamiria kumuokoa mtoto na mwanamke ili waachane na changamoto za kupoteza maisha ya watoto wakiwa tumboni au mwanamke anapojifungua ”. alisisistiza

Naye Mkuu wa mkoa wa Mbeya Mhe. Albert Chalamila alisema kukamilika kwa jengo hili litasaidia sana kufuta vifo vya mama na mtoto Kwenye mkoa wake kwani jengo hilo litakua na vifaa na vifaa tiba na kuongeza kuwa hadi sasa malalamiko ya akina mama kuhusiana na uzazi yamepungua licha ya ufinyu wa jengo lililopo.

Mhe. Chalamila alisema takwimu zinaonyesha akina mama wanaofika kujifungua kwenye hospitali hiyo kwa mwezi ni akina mama zaidi ya mia sita na hospitali hiyo imeweza kushusha vifo vitokana vyo na uzazi  hivyo anaishukuru Serikali kwa kuwaletea mradi huo ambao unaenda kuwaokoa akina mama na Watoto wa Mkoa wake.

Katika ziara yake mkoani hapa Dkt. Gwajima alitembelea pia hospitali ya rufaa ya mkoa Mbeya na kujionea hali ya ujenzi wa jengo la upasuaji lenye vyumba sita vya upasuaji na jengo la dharura  na ameahidi wizara itafanya mpango wa ujenzi wa jengo la uzazi kwenye hospitali hiyo ya mkoa ili kuweza kuwapunguzia mzigo hospitali ya wazazi ya meta ambayo ipo chini ya hospitali ya rufaa ya kanda Mbeya.

 

No comments :

Post a Comment