WAZIRI wa Viwanda na Biashara Mhe. Geoffrey Mwambe (Mb) amekutana na
kufanya kikao na Menejimenti, wakuu wa idara, Vitengo na wakuu wa taasisi zilizochini ya Wizara hiyo kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja na kujadili utekelezaji wa bajeti hiyo katika kufikia malengo yaliyowekwa na kila taasisi kueleza malengo yake na vipaumbele vyake.Akifungua kikao hicho cha siku mbili Waziri Mhe. Geoffrey Mwambe (Mb) amezitaka kila taasisi kuhakikisha zinafanya kazi kwa weredi na ubunifu mkubwa na katika bajeti yake kila taasisi ilenge katika miradi ya maendeleo na ipewa kipaumbele katika mipango ya utekelezaji wa bajeti yake.
“Nataka kila taasisi ihakikishe katika bajeti yake inalenga miradi ya maendeleo itakayosaidia kukua kwa taasisi, pia kila taasisi ipunguze kwa kiasi kikubwa matumizi yasiyo ya lazima tunataka bajeti ilete tija” amesema Mhe. Mwambe.
Aidha amezitaka taasisi katika bajeti yake zilenge vipaumbele vichache ambavyo vitatekelezeka na sio kuweka vipaumbele vingi na bajeti ikawa haitoshi na fedha kutawanywa katika sehemu mbalimbali na mwisho wa siku hakuna matokeo katika utekelezaji wake.
Amezitaka taasisi kufanya kazi kiubunifu ambapo amebainisha kuwa Tanzania ni nchi ambayo imejaliwa kuwa na fursa nyingi lakini bado hazijaleta tija kwa jamii na kuwa ni wajibu wa taasisi kuwa wabunifu nini kifanyike fulsa hizi ziwafikie walengwa hasa katika teknolojia.
“Ukiangalia katika kilimo hasa vijijini miaka nenda rudi tunatumia majembe ya mkono hiyo tija itapatikana sangapi na taasisi za utafiti zipo tu, kabla ya kuondoka katika hiki kiti nataka nizindue jembe lililobuniwa na CAMARTEC linaloleta mapinduzi” amesema.
Ameongeza kuwa “Hatuna kiwanda cha kutengeneza nguo lakini malighafi zipo na kila siku yanasafirishwa marobota mengi na mwisho wa siku tunauziwa nguo, wakati uwezo tunao wa kuwa na viwanda hapa nchini nataka hili lifanyiwe kazi haraka sababu nguvu kazi tunayo” amesema.
Ameitaka Mamlaka ya maendeleo ya biashara nchini TANTRADE kuja na mikakati ya kuhakikisha wanaweka mazingira mazuri ya biashara hasa kwa wajasiliamali katika halmashauri zote ili kuwaendeleza wafanyabiashara hao kukua kutoka hapo walipo na kuwa na biashara kubwa.
Pia ameitaka TANTRADE kuwa na mikataba ya mazao ya kibiashara kama korosho badala ya kusubiri minada ambayo sio uhakika huku akitaka kuja na teknolojia inayofaa ili kuhakikisha korosho zote zinabanguliwa na sio kuuza korosho ghafi kuongeza thamani ya zao hilo.
Aidha amekitaka chuo cha elimu ya biashara CBE kubadili mtazamo wake na kuanza kutoa elimu itakayomuwezesha mwanafunzi anapomaliza chuo kwenda kuanzisha biashara na sio mtazamo wake wa sasa wa kuzalisha wasimamizi wa biashara huku akitaka kishirikiane na vyuo vingine katika kuboresha kada hiyo.
Kwa upande mwingine ameitaka tume ya ushindani kufanyakazi kwa ubunifu na si kufanyakazi kwa mazoea ili kuhakikisha inafanyakazi na wawekezaji vizuri na sio kuwa kero kwa wawekezaji hapa nchini na hasa katika kushughulikia mapungufu ya wawekezaji hapa nchini.
“Tume ya ushindani msiwasumbue wenye viwanda kuna njia nyingi badala ya kufunga biashara yake na huyo mwenye kiwanda kuona namna ya kumaliza mapungufu hayo sio kumfungia kiwanda chake” amesema.
Naibu wa Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb) amewataka watumishi katika wizara hiyo kufanya kazi kwa nidhamu na uadilifu mkubwa na kila kiongozi katika nafasi yake ajitathmini katika utendaji wake wa kazi kama anafaa kuwa katika nafasi aliyopo.
Aidha amekemea vitendo vya uchepushaji wa fedha za miradi ambapo taasisi nyingi zimekuwa zikitumia fedha kutekeleza miradi ambayo haikukusudiwa tangu awali huku akizitaka taasisi zinazotekeleza miradi inayofanana kushirikiana na sio kila taasisi inatekeleza kivyake wakati mradi ni mmoja.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe amesema kikao hicho ni cha siku mbili kwa ajili ya kujadili vipaumbele vya kila taasisi na bajeti yake namna ya kutekeleza ili kuleta tija katika malengo ya kuanzisha taasisi hizo zilizochini ya Wizara ya Viwanda na biashara.
No comments :
Post a Comment