Wednesday, February 10, 2021

DC GONDWE AMSHUKIA MKANDARASI MWENDOKASI MBAGALA

Mkuu wa Wilaya ya Temeke Godwin Gondwe mwenye shati nyeupe aliyeinama akionyesha nyufa katika barabara ya mwendokasi inayoanzia Gerezani hadi Mbagala Rangitatu alipotembelea kukagua na kubaini kujengwa chini ya kiwango.

Mkuu wa Wilaya ya Temeke Godwin Gondwe mwenye shati nyeupe akionyesha nyufa katika barabara ya mwendokasi inayoanzia Gerezani hadi Mbagala Rangitatu alipotembelea kukagua na kubaini kujengwa chini ya kiwango.(Picha na Mpiga Picha Maalum)

…………………………………………………………………………………….

Na.Mwandishi Maalum

Mkuu wa Wilaya ya Temeke Godwin Gondwe amekasirishwa na kitendo cha mkandarasi

anayejenga  Barabara ya Mabasi Yaendayo Haraka kuanzia Gerezani hadi Mbagala Kampuni ya Sino Hydro kutoka China kwa kujenga barabara hiyo chini ya kiwango na kwa kusuasua.

Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa barabara hiyo jana , Mkuu huyo wa Wilaya amesema mkandarasi Sino Hydro ameonyesha mapungufu makubwa katika utendaji wake wa kazi kwani barabara hiyo ina nyufa nyingi sana wakati hata haijakamilika na kuanza kutumika.

“Nimesikitishwa sana na mkandarasi huyu kwa jinsi anavyofanya kazi zake, nadiriki kusema kazi zake ziko chini ya kiwango na za hovyo kabisa haiwezekani badabara haijaanza kutumika imepasuka namna hii, hili sio sawa hata kidogo” Alisema Mkuu wa Wilaya.

Amesema Rais Magufuli anatekeleza miradi ya kimkakati kwaajili ya watanzania lakini watu wasio watanzania wanakuja kuiharibu na hawachukuliwi hatua stahiki.

“Naagiza msimamizi wa mradi huu ambaye ni Wakala wa Barabara Tanzania TANROADS kuhakikisha mapungufu yote yaliyojitokeza yanarekebishwa mara moja ikishindikana taratibu za kisheria zifuatwe ili aondolewe, haiwezekani Mh. Rais ahujumiwe na mimi nikiwa hapa kama Mkuu wa Wilaya hilo halipo na wala sitakubali” Alisisitiza.

Katika Ziara hiyo iliyoanzia katika aneo la makutano ya Reli na Bandari Jijini Dar es Salaam Kamati ya ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Temeke ikiongozwa na Mkuu huyo wa Wilaya ilitembelea na kukagua ujenzi wa barabara hiyo ya Mabasi Yaendayo Haraka pamoja na vituo vya Mabasi hayo na kushuhudia mapungufu mengi katika mradi huo.

“Sisi na wenzetu wa China ni ndugu na uhusiano wetu ni wa kihistoria na wa miaka mingi tangu enzi za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, haiwezekani kampuni hii ije iharibu mahusiano yetu na China , nitahakikisha namfikishia Waziri husika suala hili na pia nitamtaarifu Balozi wao ambaye ni rafiki yetu mkubwa na anafanya kazi nzuri sana” Alisema.

Amesema mkandarasi huyo amekua na kiburi na anaendelea kuihujumu nchi kwani anadiriki kubadilisha matokeo ya uchunguzi wa kimaabara unaoonyesha kuwa kazi zake ziko chini ya kiwango, na anafukuza watanzania wanatoa taarifa za kuhujumiwa kwa mradi.

“Nimepata taarifa kuwa sampuli za udongo zilizochukuliwa na wataalam hapa katika eneo la Mgulani zilikataa na walitakiwa warudie ujenzi wa tabaka la chini la hii barabara lakini wao walikwenda kubadilisha matokeo na wakawatishia wataalam wetu na wengine wakawafukuza kazi hii si sawa hata kidogo katika utawala huu wa JPM” alisisitiza.

Kwa upande  wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Mhandisi Ronald Lwakatare alisema barabara ya Mabasi Yaendayo Haraka katika Barabara ya Kilwa ni muhi mu sana kwa maisha ya wakazi wa Mbagala na maeneo ya Jirani hivyo ni lazima ijengwe katika kiwango cha kimataifa ili idumu kwa miaka mingi zaidi.

“Mh. Rais ameweka fedha nyingi katika mradi huu, hii yote ni kwaajili ya mapenzi yake kwa watanzania hasa watanzania wanyonge ili waondokane na adha ya msongamano wa magari nivyema msimamizi wa mradi akahakikisha anawasimamia wakandarasi kila hatua ili kuona kama kazi inayofanyika inakidhi viwango vya kimataifa” Alisema Mhandisi Lwakatare.

Alisema zaidi ya Shilingi Bilioni 217 zinatumika katika mradi huo hivyo ni vyema kasi ya utekelezaji wa mradi iongezeke ili hatimaye wakazi wa Mbagala waanze kufurahia usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka ambayo kwa mujibu wa mpango wa Wakala njia hiyo inatakiwa kuwa na mabasi zaidi ya 400.

 

No comments :

Post a Comment