Tuesday, January 5, 2021

WAZIRI DKT. CHAMURIHO AIAGIZA TEMESA KUTUNZA MV CHATO II

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho (watatu kulia) akiwa na viongozi wengine akikata utepe kuashiria kukipokea rasmi kivuko cha Mv Chato II HAPA KAZI TU leo, wilayani Chato, mkoani Geita
Baadhi ya Wananchi wa kijiji cha Kalema, wilayani Chato Mkoani Geita waliojitokeza kukipokea kivuko Kipya cha MV Chato II, HAPA KAZI TU leo tarehe 5 Januari, 2021.

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, ameuwagiza uongozi wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) mkoa wa Geita, kuhakikisha unasimamia kwa karibu uendeshaji wa kivuko cha Mv Chato II, hapa kazi tu, ili wananchi wa mkoa huo waweze kufaidi matunda ya Serikali kwa maendeleo yao binafsi na nchi nzima kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa kupokea kivuko hicho wilayani Chato mkoani Geita, Waziri Chamuriho, amsema kuwa kivuko hicho ambacho kimepokelewa leo kitatumika kwa muda na pindi uongozi husika utakapojiridhisha na ufanisi wake, utakuja tena kukizindua rasmi.

" Kama mnavyoona leo hii tumekipokea kivuko hiki ambacho tutakiangalia ufanisi wake kwa muda, tukiridhika tutakuja kukizindua, hivyo wananchi wa hapa tunaomba mkitunze kwa ajili ya maendeleo yenu na nchi kwa ujumla", amesema Waziri Chamuriho.

Chamuriho, amesisitiza kuwa katika kuhakikisha usalama wa vivuko vyote nchini, Serikali itaendelea kuboresha usimamizi wa uendeshaji wa vyombo vya majini ili kuepusha matukio ya ajali yanayoweza kutokea.

Aidha, Chamuriho ameuelekeza Wakala wa Meli nchini (TASAC), kuendelea kutoa mafunzo kwa wamiliki na waendesha vyombo vya usafiri majini ikiwemo TEMESA ili kuwaongezea ufahamu juu ya umuhimu wa kuzingatia taratibu na kanuni zinazosimamia uendeshaji wa vitu hivyo.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chato, ambaye pia ni Waziri wa Nishati. Dkt Medard Kalemani,ameipongeza wizara kwa kuleta kivuko hicho katika eneo hilo la Kalema, wilayani Chato na amemuhakikishia Waziri huyo kuwa yeye na wananchi wake, wanaahidi kutunza muindombinu ya kivuko hicho.

" Niliahidi wananchi kuwaletea kivuko wakati wa Kampeni na leo hata miezi mitatu haijafika tayari tumepokea kivuko, naamini kuja kwa kivuko tutapata fursa yakuwa na biashara ya uhakika usiku na mchana", amesema Waziri Kalemani

Naye, Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Mhandisi Japhet Maselle, amesema kuwa kivuko hicho kilianza kujengwa rasmi mwezi Mei, 2019 na mkandarasi mzawa kampuni ya Songoro Marine Transport.

Ameongeza kuwa kivuko hicho kina uwezo wa kubeba Tani 100 ambapo sawa na magari madogo 10 pamoja na abiria 200 na kimefungwa injini mbili mpya na tayari kimeshafanyiwa ukaguzi na kusajiliwa na TASAC.

Awali akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Kalema, wilayani Chato, Mkuu wa Wilaya ya Chato amesema kuwa uwepo wa kivuko hicho ni fursa wilayani hapo kutokana na Wananchi kuwa watakitumia katika kusafirisha bidhaa zao kutoka eneo moja kwenda jingine.

Kivuko hiki ambacho ni moja ya vivuko vinne vilivyonunuliwa kanda ya ziwa, kimenunuliwa na Serikali kwa gharama ya shilingi billion 3.1 ambazo zote zikiwa zimetolewa na Serikali na kinatarajiwa kutoa huduma ya usafirishaji katika eneo la Chato, Nkome, Muharamba, Senga, Kikumbaitale na Izumacheli.

 

No comments :

Post a Comment