Saturday, January 30, 2021

TAKUKURU YAWASAIDIA WANYONGE KWENYE MIKOPO UMIZA


Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari mjini Babati.

*********************************************

Na Mwandishi wetu, Manyara

 

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoani Manyara, kwa kipindi cha

miezi mitatu imefanikiwa kuwarejeshea waathirika wa mikopo umiza mali zao ikiwemo nyumba tano, magari matatu na pikipiki mbili.

 

Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu ameyasema hayo mjini Babati wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya kazi za robo ya mwaka zilizofanyika kuanzia mwezi Oktoba hadi Desemba mwaka jana.

 

Makungu amesema mali hizo waliporwa baada ya kuingia mikataba ya kuchukua fedha kutoka kwa wakopeshaji ambao ilibainika wanakopesha kinyume na taratibu za sheria ya biashara ya fedha na kutoza riba kubwa.

 

“Pamoja na wanyonge hao TAKUKURU pia ilifanikiwa kusaidia urejeshaji wa mali nyingine zisizohusiana na mikopo umiza ambazo ni kiwanja chenye ukubwa wa mita 930 cha CCM ambacho kiliporwa tangu mwaka 2015 huko wilayani Kiteto,” amesema.

 

Amesema pia, walisaidia urejeshwaji wa shilingi milioni 35.9 kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilayaya Simanjiro Yefred Myenzi kutoka kwa wazabuni wakorofi.

 

“Mbali ya hizo pia katika kipindi hicho TAKUKURU ilifanikiwa kuokoa fedha nyingine kiasi cha shilingi milioni 22.2 fedha ambazo zilirejeshwa kutoka mikononi mwa watu wasiokuwa waaminifu waliokopeshwa kupitia vyama vya msingi ikiwa ni mikopo ya pembejeo za kilimo,” amesema Makungu.

 

Amesema pia katika kipindi hicho cha miezi mitatu, walifanikiwa kurejesha shamba lenye ukubwa wa ekari 70 kwa bibi Hando mwenye umri wa zaidi ya miaka 70 huko wilayani Kiteto. 

 

No comments :

Post a Comment