Saturday, January 30, 2021

MAKAMO WA PILI WA RAIS AZINDUA CHAMA CHA MADAKTARI BINGWA WA SARATANI TANZANIA

Rais wa Chama cha Madaktari bingwa wa Saratani Tanzania Dkt. Jerry Ndumbalo akieleza historia ya Chama hicho kabla ya kuzinduliwa rasmi na Makamu wa Pili wa Rais katika Hotel ya Verde Mtoni, nje kidogo ya Mjini Zanzibar.

Kaimu Waziri wa Afya ambae pia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Simai Muhammed Said, akimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdallah kuzungumza na kuzindua Chama cha Madaktari wa Saratani Tanzania.

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdallah akizungumza na wanachama wa Chama cha Madaktari bingwa wa Saratani katika Hoteli ya Verde Mtoni, nje kidogo ya Mji wa Zanzibar

Baadhi ya Madaktari bingwa na wageni walikwa wakifuatilia hotuba ya uzinduzi wa Chama cha Madaktari bingwa wa Saratani Tanzania hafla iliyofanyika Hoteli ya Verde Mtoni, nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdalla akizindua Chama cha Madaktari bingwa wa Saratani Tanzania katika Hoteli ya Verde Mtoni. (wa kwanza kulia) Rais wa Chama hicho Dkt. Jerry Ndumbalo na (kushoto) ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais Dkt.Khalid Salum na Kaimu Waziri wa Afya Simai Muhammed Said

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdallah katika picha ya pamoja na baadhi ya madaktari bingwa wa Saratakani.

Picha na Makame Mshenga.

***************************************************

Na Ramadhani Ali Maelezo                                     30.01.2021

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdalla amesema Serikali zote

mbili za Tanzaina zinathamini mchango mkubwa unaotolewa na wataalamu wa afya na zitaendelea kuboresha mazingira ili waweze kutoa huduma bora zaidi na kupunguza vifo vitokanavyo na maradhi mbali mbali

Makamu wa Pili wa Rais ameeleza hayo wakati wa uzinduzi wa Chama cha Madaktari bingwa wa maradhi ya Saratani Tanzania uliofanyika katika Hoteli ya Verde iliyopo Mtoni, nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Amesema kuanzishwa kwa Chama cha Madaktari bingwa wa Saratani nchini ni kitu cha kujivunia kwani inaelekea lengo ni kwenda mbali zaidi katika mapambano ya maradhi hayo ambayo yamekuwa yakiongeza kwa kasi.

Amewahakikishi wanachama wa Chama hicho kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zitaendelea kushirikiana na Chama hicho kuhakikisha huduma za matibabu ya maradhi ya Saratani zinaimarishwa.

Mh. Hemed alikumbusha kwamba virusi vya maradhi ya Saratani kama vilivyo vya maradhi mengine vimekuwa vikibadilika, hivyo kuwepo kwa taasisi ambazo wanachama wake watafaidika na ujuzi unaoendana na mabadiliko yanayotokea katika uwanja wa tiba ni jambo zuri.

Amewashauri madaktari bingwa wa maradhi ya Saratani ambao bado hawajajiunga na Chama hicho wajiunge kutokana na faida nyingi zinazopatikana kutoka taasisi nyengine za kitaaluma.

Amesema Saratani ni moja ya magonjwa hatari yasiyoambukiza na inakadiriwa watu takriba milioni 7.9 hufariki kila mwaka duniani ikiwa ni sawa na asilimia 21 ya vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyoambukiza na zaidi ya theluthi mbili ya wagonjwa hao wanagunduliwa katika nchi zinazoendelea.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliweka wazi kuwa kwa Tanzania Saratani inashika nafasi ya tano kwa wanaume na pili kwa wanawake kusababisha maradha na vifo.

Aliitaja Saratani ya shingo ya kizazi kuwa inaongoza ikifuatiwa na Saratani ya matiti, ngozi na Umio kwa wanawake na upande wa wanaume ni Saratani ya ngozi, umio kichwa na tenzi dume ndio zinaongoza.

Rais wa Chama cha Madaktari bingwa wa maradhi ya Saratani Tanzania Dkt. Jerry Ndumbalo amesema lengo la Chama chao ni kuisaidia Serikali katika kuimarisha matibabu na kufanya kampeni ya kuchunguza Saratani katika mikoa mbali mbali ya Tanzania ili kuweza kuigundua katika hatua za awali na kuwapatia matibabu.

Amesema tatizo kubwa la kuongezeka kwa maradhi hayo inatokana na wagonjwa wengi kwenda Hospitali wakiwa katika hali mbaya ambayo huwa vigumu kutibika.

Dkt. Ndmbalo aliipongea Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuongeza idadi ya Hospitali zinazotoa matibabu ya Saratani badala ya Hospitali ya Ocean Road pekee,  na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuanzisha kitengo cha kutibu wagonjwa wa maradhi hayo katika Hospitali kuu ya Mnazimmoja.

 

No comments :

Post a Comment