Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amepiga marufuku
halmashauri, Taasisi na Watu binafsi kuchukua maeneo ya wananchi bila
kulipa fidia.
Akizungumza hivi
karibuni mkoani Singida wakati wa ziara yake ya kikazi katika mkoa huo,
Lukuvi alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya halmashauri na Taasisi
kuchukua maeneo ya wananchi bila ya kuwalipa fidia kwa maelezo maeneo
hayo kuhitajika kwa ajili ya shughuli za kimaendeleo.
Kwa mujibu wa
Lukuvi, sheria inakataza kuchukua maeneo ya wananchi bila kulipa fidia
na Mhe. Rais John Pombe Magufuli alishakataza watu, taasisi au
halmashsuri kunyang’anya maeneo ya wananchi bila kulipa fidia.
Waziri Lukuvi alifikia kutoa
maamuzi hayo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa Bibi Maria Samweli
mkazi wa Singida ambaye alimpa malalamiko yake ya kutolipwa fidia kwa
zaidi ya miaka 12 kwa ajili ya kupisha mradi wa upimaji na ugawaji
viwanja.
” Mtu yeyote
atakayeendeleza maumivu kwa wananchi kwa kuendeleza kero ya kuchukua
maeneo bila kulipa fidia kazi yake itakuwa kubwa, kwanza msisitizo
ulishawekwa na Mhe Rais Magufuli aliyepiga marufuku watu, taasisi au
halmashauri kupora maeneo ya wananchi bila kulipa fidia” alisema Lukuvi.
Alisema, upo
utaratibu wa kuchukua maeneo ya wananchi kwa manufaa ya umma na
utaratibu huo lazima mwananchi alipwe fidia kwa kupewa haki yake na
kusisitiza kuwa ardhi pekee inayoweza kuchukuliwa bila kulipa fidia ni
ile aliyomilikishwa mtu kwa hati na mmiliki huyo akashindwa kuendeleza
kwa wakati ambapo hati hiyo ikifutwa mmiliki wake hawezi kulipwa fidia.
Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliongeza kwa kuwa, halmashauri yoyote
ikitamani ardhi inayomilikiwa kihalali na hata kama halijaendelezwa
lazima mmiliki wake alipwe fidia na kusisitiza kwamba, tangu mwaka 1999
ardhi isiyofanyiwa kitu chochote ina thamani yake na kilichoendelezwa
juu yake nacho kina thamani yake.
No comments :
Post a Comment