Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU), Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo,akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 16,2021 ofisini kwake Dodoma wakati akitoa taarifa mbalimbali za matukio yaliyojiri.
………………………………………………………………..
Na Alex Sonna, DODOMA
RAIA wa Kenya Alexander Mwikali(42), amefikishwa katika Mahakama ya Mkoa wa Dodoma kwa tuhuma ya kutoa rushwa ya Sh.200,000 kwa Mganga Mkuu wa Serikali Prof.Abel Makubi ili
ampatie cheti cha uthibitisho wa kutokuwa na ugonjwa wa Corona.Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma leo Januari 16,2021, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU), Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo, amesema Raia huyo anaishi Nkuhungu Jijini Dodoma na anafanya kazi kama Mtaalam wa nyama wa Kampuni ya Alkafil.
Kibwengo amesema Raia huyo alinaswa baada ya kuandaliwa mtego ofisini kwa Mganga Mkuu huyo alipokuwa akitoa rushwa ya Sh.200,000 kinyume na kifungu namba 15(1)(b) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na rushwa namna 11 ya mwaka 2007 ili apate cheti hicho.
“Mtuhumiwa huyo alifikishwa Mahakama ya Mkoa wa Dodoma na kufunguliwa shtaka husika ambalo alikiri na kutozwa faini ya Sh.500,000 na fedha aliyotoa kama hongo ikitaifishwa,”amesema.
Katika hatua nyingine, TAKUKURU inawashikilia wanafunzi 13 wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini(IRDP) Dodoma kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa na udnganyifu wakati wa kufanya mtihani wa marudio wa somo la Applied Statistics II kwa mwaka wa tatu uliofanyika Novemba mwaka jana.
Pia, Taasisi hiyo imetaja sekta vinara kwa kuongoza kulalamikiwa kwa vitendo vya rushwa ambapo serikali za mitaa inaongoza kwa asilimia 23 ikifuatiwa na mikopo umiza kwa asilimia 20.
Kibwengo ametaja taasisi zingine ni sekta ya ardhi asilimia 14 huku vyama vya siasa au uchaguzi, polisi afya zikilalamikiwa zote kila mmoja kwa asilimia sita.
Sambamba na hilo, Taasisi hiyo imebaini baadhi ya kampuni za ujenzi wa miundombinu ya barabara na maji kukwepa kodi ya ushuru wa huduma hali inayozikosesha Halmashauri mapato stahiki.
“Kwa mfano tumebaini kwamba Sh.Milioni 500 hazikulipwa na kampuni hizo kati ya mwaka 2017 hadi 2020, TAKUKURU kwa kushirikiana na TANROADS(Wakala wa Barabara) na DUWASA(Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Dodoma) imeanza kufuatilia ili fedha hizo zilipwe,”amesema.
Kadhalika, TAKUKURU inamsaka Mmiliki wa Kampuni ya ukopeshaji fedha ya Mjini Kondoa, Abubakary Kinyuma, baada ya kubainika kushikilia kadi za benki zaidi ya 400 za watumishi mbalimbali hasa wanaokaribia kustaafu.
Kibwengo, amesema taasisi hiyo inachunguza kampuni hiyo iitwayo Geneva Credit Shop baada ya kupokea malalamiko ya wananchi 30 ambao wanadaiwa kupatiwa mikopo umiza na kampuni hiyo.
Wakati huo huo, Taasisi hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, jumatatu inatarajia kumfikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Dodoma, Mhasibu Msaidizi wa mapato wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Dodoma(DUWASA), Severo Mutegeki(42) kwa tuhuma za kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya Sh.Milioni 428.
No comments :
Post a Comment