Saturday, January 16, 2021

WAZIRI MWAMBE AIAGIZA EPZA KUJIKITA NA UJENZI WA MAENEO MAPYA YA VIWANDA


Waziri wa Viwanda na Biashara Geoffrey Mwambe ameiagiza Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) kujikita katika ujenzi wa maeneo mapya ya viwanda kulingana na biashara iliyopo katika mkoa husika ikianza na Mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani kwa ajili ya kuwawezesha wajasiliamali wadodo kuchakata korosho ikifuatiwa na maeneo mengine yayozalisha pamba kwa wingi pamoja na uchenjuaji madini

Waziri Mwambe ameyasema hayo alipokuwa akiongea na menejimenti na wafanyakazi wa EPZA alipofanya ziara katika taasisi hiyo akiambatana na Naibu Waziri wa Viwanda Exaud Kigahe  pamoja na baadhi ya wakurugenzi wa Wizara ya Viwanda na Biashara.

Aidha Waziri Mwambe pia ameiagiza EPZA kuyaendeleza na kuyatunza maeneo yote inayoyamiliki ambayo imeshayalipia kwa ajili ya ujenzi wa viwanda pamoja na kufuatilia madeni yote inayowadai wapangaji wake ili fedha hiyo itumike katika kuendeleza maeneo ya viwanda na kufikia malengo iliyojiwekea ambayo hayajafikiwa hadi sasa.

Vilevile Waziri Mwambe  amewaasa watumishi wa EPZA kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kuepuka vitendo vya rushwa wanapowahudumia wafanyabiashara pamoja na kujieendeleza katika taauma zao ili kuendana na wakati,  kuweza kutoa huduma bora katika uwigo mpana wa biashara na kuongeza idadi ya wafanyabiashara  wanaowahudumia.

Naye Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara amesisitiza EPZA kuyaendeleza maeneo inayoyamiliki ili kuepusha migogoro ya ardhi na wananchi wanaovamia maeneo hayo pamoja na kutunza maeneo  kwa ajili ya ujenzi wa viwanda kwa kizazi kijacho.

Aidha, Naibu Waziri ameiasa EPZA kushirikiana na TAMISEMI katika kuelimisha wananchi faida za maeneo ya EPZA yaliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda huku akiishauri kutumia fursa zinazojitokeza katika kuendeleza miundombinu katika maeneo hayo hususani barabara, maji na umeme.

 

No comments :

Post a Comment