Monday, January 4, 2021

NIC YATOA MILIONI 14. 7 KUFANIKISHA MAPINDUZI CUP

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo Omar Hassan King akimkaribisha Waziri Tabia Maulid Mwita
kwenye mkutano na viongozi wa Shirika la Bima la Taifa Tanzania (NIC)
uliofanyika Ofisi ya Wizara Migombani.


Baadhi ya waalikwa walioshiriki mkutano wa Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na viongozi wa Shirika la Bima la
Taifa (NIC) wakifuatilia mkutano huo uliofanyika Ofisini kwa Waziri
Migombani.


SHIRIKA la Bima la Taifa Tanzania (NIC) limetoa mchango wa shilingi
14, 700,000 kwa ajili ya kufanikisha mashindano ya soka ya Kombe la
Mapinduzi ya mwaka huu yanayotarajiwa kuanza tarehe 5.1.2021 katika
kiwanja cha Amani, Mjini Zanzibar.

Mkurugenzi Mtendaji wa NIC Dkt. Elirehema Doriye alimueleza Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita kwamba
wameamua kuyapa msukumo mashindano hayo baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukaribisha Mashirika, Wafanyabiashara na wadau wa michezo kuchangia mashindano hayo.

Alisema lengo la mchango huo ni kusaidia gharama za uendeshaji wa
mashindano na zawadi ya mchezaji bora kwenye michuano hiyo
inayoshirikisha timu tisa, nne kutoka Zanzibar na tano kutoka Tanzania
Bara.

Mkurugenzi Doriye alimuahidi Waziri Tabia Maulid Mwita kwamba NIC
itaendelea kuwa washirika wa karibu wa mashindano ya Kombe la
Mapinduzi kwa miaka mengine ijayao.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Wizarani kwake
Migombani, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid
Mwita alilishukuru Shirika la Bima la Taifa Tanzania kwa msaada huo na
ahadi walizotoa kwa miaka ijayo katika kuendesha mashindano hayo.

 Alisema mchango wa shilingi milioni 14 na laki saba waliotoa
utasaidia sana katika kufanikisha mashindano ya mwaka huu ambayo
yemekua endelevu tokea yalipoanzishwa kitaifa mwaka 2007.

Waziri Tabia aliwaeleza viongozi wa Shirika la Bima la Taifa Tanzania
kuwa Serikali imeazimia kuimarisha michezo mbali mbali ikiwemo Ligi
kuu ya Zanzibar na michango ya wadau inahitajika katika kufanikisha
lengo hilo.

Aliahidi kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na Shirika hilo na
amewakaribisha kutumia vyombo vya Habari vilivyochini ya Wizira hiyo
katika kuimarisha shughuli zao za kibiashara.

 

No comments :

Post a Comment