Monday, January 4, 2021

CRDB KUWAFIKIA WANANCHI LUDEWA, MPANGO WAKAMILIKA

Denis Mwoleka meneja wa benki ya CRDB kanda ya kusini akieleza namna walivyojipanga kufungua tawi la CRDB katika wilaya ya Ludewa ili kukuza uchumi na uwekezji katika wilaya hiyo.
Joseph Kamonga Mbunge wa jimbo la Ludea mkoani Njombe wakati akiomba taasisi za kifedha kuwekeza katika jimbo hilo kutokana na fursa za kiuchumi zinazopatikana Ludewa.
Baadhi ya wafanyabiashara waliofika katika sherehe za CRDB za kuaga mwaka 2020 na kuukaribisha mwaka 2021,sherehe zilizofanyika katika ukumbi wa Green City mjini Makambako.

Na Amiri Kilagalila, Njombe

 

MBUNGE wa jimbo la Ludewa mkoani Njombe wakili Joseph Kamonga ametoa

wito kwa wawekezaji kuwekeza katika sekta mbalimbali kama vile uvuvi na madini katika jimbo hilo ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi katika Wilaya ya Ludewa yenye utajiri mwingi wa madini ya Chuma na makaa ya Mawe.

Kamonga akiwa katika sherehe za benki ya CRDB tawi la Makambako za kuukaribisha mwaka 2021, amesema wilaya ya Ludewa ina fursa nyingi hivyo ni wakati wa makampuni mbalimbali kuwekeza wilayani humo ikiwemo taasisi za kifedha kusogeza huduma kwa kuwa wananchi wake wamekuwa na jitihada za kutafuta maendeleo hususani pia katika kilimo huku kukiwa na uhaba wa taasisi za kifedha.

“Ludewa kuna fursa nyingi,kuna uwekezaji kwenye Kilimo,uwekezaji kwenye ufugaji kuna uvuvi kwenye ziwa Nyasa lakini vile vile ndio inaongoza kwa rasilimali nyingi za madini kwa mkoa wa Njombe.”Alisema Kamonga.

Aliongeza kuwa,  “Hizo ni fursa ambazo CRDB mnaweza mkazitumia kama mtaji kwa ajili ya kuanzisha tawi na mimi nipo tayari kuwapa ushirikiano wote.”aliongeza  Kamonga.

Kufuatia wito huo benki ya CRDB imeahidi kusogeza huduma katika wilaya hiyo ambapo kupitia meneja wa kanda wa benki hiyo Denis Mwoleka amesema wanatambua umuhimu wa wilaya hiyo kuwa na tawi la CRDB katika uwekezaji,hivyo ameahidi kusogeza huduma kwa kuwa mpango umekamilika.

“Nashukuru sana mbunge wa Ludewa na sisi tayari mchakato unaendelea kwa ajili ya kuleta tawi la CRDB Ludewa,nikuhakikishie ni kitu ambacho kipo kwenye mpango wetu ndani ya mwaka huu.tunashukuru sana pia kwa ushirikiano wa serikali kwasababu CRDB huwezi kuitenganisha na serikali.”alisema Denis Mwoleka.

Mkuu wa wilaya ya Njombe Ruth Msafiri kwa niaba ya mkuu wa Mkoa ndiye aliyekuwa mgeni wa heshima katika sherehe hiyo,amesema taasisi za kifedha zimekuwa na mchango mkubwa  katika uchumi wa taifa hususani kwa wananchi wa mkoa wa Njombe kupitia mikopo inayowasaidia kuendesha biashara.

“Mwezi wa saba tarehe moja benki kuu ya Dunia ilitangaza nchi yetu kuwa imetoka kwenye uchumi ulio nyuma na tegemezi na kuingia rasmi kwenye uchumi wa viwanda,huo ulikuwa ushindi mkubwa,ili tuendelee kufanikiwa niombe tuzidi kuwa na mshikamano na upendo.”alisema Ryth Msafiri.

 

No comments :

Post a Comment