Wednesday, January 20, 2021

DAWASA YAKABIDHIWA MRADI, KUFIKIA DESEMBA 2021 WANANCHI KUPATA HUDUMA YA MAJI


Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso akikata utepe kuashiria uzinduzi wa uendelezaji wa ujenzi wa Mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe.
Waziri wa Maji pamoja na wataalamu Mbalimbali wakikagua mtambo wa kutibu maji katika mradi wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe.
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso akiwasha mashine ya kuunganisha mabomba wakati wa Hafla fupi ya kukabidhi mradi kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA.)

WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso amewataka wataalam wa manunuzi kuhakikisha watoa huduma na wakandarasi watakaosimamia mradi waa

maji  wanakuwa bora ili kufikisha huduma ya maji kwa wananchi kama ilvyopangwa.

Hayo ameyasema wakati wa makabidhiano ya mradi wa maji Same-Mwanga-Korogwe kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA.)

DAWASA imepewa kazi ya kukamilisha mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe baada ya wakandarasi wa awali kampuni za M.A Kharafi & Sons na BADR East African Enterprises Ltd kusuasua katika utekelezaji wa mradi na kusitishiwa mkataba mwezi Desemba 2020.

Mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe utazalisha zaidi ya lita milioni 65 kwa siku na  utakuwa na tanki lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni tisa na ujenzi huo utahusisha pia  ulazaji wa mabomba yenye urefu wa jumla ya kilomita 265. 

Waziri  Aweso  amesema Serikali itasimamia haki na madai ya malipo ya wafanyakazi waliofanya kazi na kampuni hizo, na haitamvumilia mkandarasi mzembe au mtaalam atakayechelewesha mradi wa maji kukamilika kwa wakati. 

Aweso, amesema katika kukamilisha mradi huo baadhi ya kazi kama ufungaji wa mifumo na mitambo ya umeme (electro mechanical) zitafanywa na wakandarasi na utaratibu wa kuwapata umeshaanza ili kila jambo lifanyike kwa wakati na kukamilika

Naye Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi. Anthony Sanga amesema Serikali ya awamu ya tano imejipanga katika kuhakikisha tatizo la maji linaisha, na wataalam wake wamejipanga kuchukua miradi yote ambayo wakandarasi watalegalega katika kuzingatia mikataba ya kazi.

 Amesema, Pamoja na hilo, ametoa onyo kwa wakandarasi wanaozidisha gharama za miradi kwa sababu watapoteza sifa za kutekeleza miradi hiyo.

Kwa upannde wa  Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi. Cyprian Luhemeja amewahakikishia viongozi wa mkoa wa Kilimanjaro kuwa kazi ya kukamilisha mradi huo wanaimudu, na kuahidi kazi itakamilishwa ifikapo tarehe 19 Desemba, 2021. 

Kukamilika kwa Mradi  mwishoni mwa mwaka huu utafikisha kiwango cha upatikanaji huduma ya maji kwa asilimia 100 katika maeneo husika.

 

No comments :

Post a Comment