Friday, January 15, 2021

BILIONI 11 ZAOKOLEWA CHAKULA CHA WAFUNGWA

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya  Nchi, Khamis Hamza Chilo(watatu kushoto), akimsikiliza   Kamishna Jenerali wa Magereza, Suleiman Mzee (kulia) akimpa maelezo ya mashine ya kukatia chuma,leo  wakati naibu waziri huyo alipotembela Mradi wa Ujenzi wa Kiwanda cha Samani cha jeshi hilo kinachojengwa Msalato jijini Dodoma.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya  Nchi, Khamis Hamza Chilo, akizungumza wakati  alipotembela leo Mradi wa Ujenzi  wa Kiwanda cha Samani cha Jeshi la Magereza kinachojengwa Msalato jijini Dodoma.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya  Nchi, Khamis Hamza Chilo, akimwagilia mti aliopanda wakati wa ziara ya kutembelea Makao Makuu Mapya ya Jeshi la Magereza nchini yaliyopo Msalato, jijini Dodoma.Kushoto ni Kamishna Jenerali wa Magereza, Suleiman Mzee akiongoza viongozi wa jeshi hilo kushuhudia tukio hilo leo.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya  Nchi, Khamis Hamza Chilo(watatu kushoto), akimsikiliza Mrakibu Msaidizi wa Magereza, Jumanne Malema  akimpa maelezo ya mashine ya kupindia

vyuma, leo  wakati naibu waziri huyo alipotembela Mradi wa Ujenzi wa Kiwanda cha Samani cha jeshi hilo kinachojengwa Msalato jijini Dodoma.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

***********************************************

Na Mwandishi Wetu

Jeshi la Magereza nchini limeokoa jumla ya Shilingi Bilioni 11, ikiwa ni gharama ya chakula cha wafungwa tangu lianze kujitegemea kwa chakula ikiwa  ni maelekezo ya Rais  Dkt. John Pombe Magufuli ya kulitaka jeshi hilo litumie nguvu kazi ya wafungwa ilionao kuzalisha chakula.

Akizungumza leo katika ziara ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,iliyofanyika katika Makao Makuu Mapya ya Jeshi hilo ,Msalato jijini Dodoma, Kamishna Jenerali wa Magereza, Suleiman Mzee amesema walikuwa wanatumia Shilingi Bilioni Moja kila mwezi kulipa wazabuni wa chakula waliokuwa wanaliuzia chakula  jeshi hilo.

“Sasa hivi tunajitegemea asilimia kubwa kwa chakula, Serikali kabla ya mwezi wa tatu mwaka jana kila mwezi kulikua kuna deni la Bilioni Moja, lakini baada ya mwezi huo wa tatu sasa tunaokoa kiasi hicho cha fedha shilingi bilioni moja na mpaka sasa tuna miezi kumi na moja tunajilisha wenyewe kupitia shirika la magereza” alisema CGP Mzee

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Naibu Waziri, Khamis Hamza Chilo alilipongeza Jeshi la Magereza kwa kutekeleza vyema agizo la Rais Magufuli ikiwa sambamba na ujengaji wa kiwanda kikubwa cha samani ambapo mpaka kukamilika kwake kitagharimu shilingi Bilioni 1,101,743,123/=

“Niwapongeze kwa hatua mbalimbali za maendeleo ambazo zingine nimeshuhudia mwenyewe,lakini kubwa kuweza kujitegemea kwa chakula cha wafungwa hali iliyopelekea kuokoa kiasi kikubwa cha fedha ambacho kinabaki humu humu ndani na mnakitumia kwa shughuli zingine za maendeleo hongereni sana” alisema Naibu Waziri Chilo.

 

No comments :

Post a Comment